2 Mambo ya Nyakati 36:15-21
2 Mambo ya Nyakati 36:15-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, mara kwa mara alituma kwao wajumbe wake maana alikuwa na huruma kwa watu wake na makao yake. Lakini wao waliendelea kuwadhihaki wajumbe wa Mungu, wakayapuuza maneno yake na kuwacheka manabii wake mpaka hatimaye ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya watu wake hata kusiwe na namna yoyote ya kutoroka. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu alimleta mfalme wa Wakaldayo ambaye aliwaangamiza vijana wao kwa upanga hata ndani ya mahali patakatifu; wala hakumhurumia mtu yeyote awe mvulana au msichana, mzee au mnyonge. Wote Mwenyezi-Mungu aliwatia mikononi mwake. Alitwaa vyombo vyote vya nyumba ya Mungu vikubwa na vidogo na hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya mfalme na maofisa wake. Alivipeleka vyote mpaka Babuloni. Aliichoma moto nyumba ya Mungu, akaubomoa ukuta wa Yerusalemu, akayachoma moto majumba yote ya kifalme na kuharibu vyombo vyake vyote vya thamani. Watu walionusurika vitani aliwachukua uhamishoni Babuloni. Huko wakawa watumwa wake na wa wazawa wake mpaka mwanzo wa ufalme wa Persia. Hivyo likatimia neno la Mwenyezi-Mungu alilosema nabii Yeremia: “Nchi itabaki tupu bila kulimwa miaka sabini kulingana na muda wa pumziko ambao haukuadhimishwa.”
2 Mambo ya Nyakati 36:15-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA, Mungu wa baba zao, akawapelekea neno kupitia wajumbe wake tena na tena, kwa sababu alikuwa anawahurumia watu wake pamoja na mahali pa maskani yake. Lakini waliwadhihaki wajumbe wa BWANA wakayadharau maneno yake na kuwacheka manabii wake mpaka ghadhabu ya BWANA ikawa kubwa dhidi ya watu wake na hakukuwa na namna ya kuituliza. Mungu akamwinua dhidi yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao wa kiume kwa upanga ndani ya mahali patakatifu, ambaye hakumbakiza kijana mwanaume wala kijana mwanamke, wazee wala vikongwe. Mungu akawatia wote mikononi mwa Nebukadneza. Akavichukua kwenda Babeli vyombo vyote kutoka Hekalu la Mungu, vikubwa na vidogo, hazina za Hekalu la BWANA pamoja na hazina za mfalme na za maafisa wake. Wakalichoma Hekalu la Mungu na kuzibomoa kuta za Yerusalemu, wakachoma moto majumba yote ya kifalme na kuharibu kila kitu chake cha thamani. Wale watu walionusurika kuuawa kwa upanga wakachukuliwa kwenda uhamishoni Babeli. Nao wakawa watumishi wake na wa wanawe mpaka wakati wa utawala wa ufalme wa Uajemi ulifika. Nchi ikaendelea kufurahia pumziko lake la Sabato, wakati wote wa kufanywa kwake ukiwa ilipumzika mpaka ile miaka sabini ilipotimia katika kutimiza neno la BWANA lililonenwa na Yeremia.
2 Mambo ya Nyakati 36:15-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye BWANA, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake; lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya BWANA juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya. Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mnyonge; akawatia wote mkononi mwake. Na vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, vikubwa kwa vidogo, na hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za mfalme, na za wakuu wake; vyote pia akavileta Babeli. Wakaiteketeza nyumba ya Mungu, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, wakaviharibu vyombo vyake vyote vya thamani. Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi; ili kulitimiza neno la BWANA kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ukiwa ilishika sabato, kutimiza miaka sabini.
2 Mambo ya Nyakati 36:15-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye BWANA, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake; lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya BWANA juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya. Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mkongwe; akawatia wote mkononi mwake. Na vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, vikubwa kwa vidogo, na hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za mfalme, na za wakuu wake; vyote pia akavileta Babeli. Wakaiteketeza nyumba ya Mungu, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, wakaviharibu vyombo vyake vyote vya thamani. Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi; ili kulitimiza neno la BWANA kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ukiwa ilishika sabato, kutimiza miaka sabini.