2 Mambo ya Nyakati 20:1-6
2 Mambo ya Nyakati 20:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya muda, majeshi ya Moabu na Amoni pamoja na baadhi ya Wameuni, waliivamia Yuda. Watu kadhaa walikuja wakamwambia mfalme Yehoshafati, “Jeshi kubwa limekuja kukushambulia kutoka Edomu, ngambo ya Bahari ya Chumvi. Tayari wamekwisha teka Hasason-tamari.” (Hili ni jina lingine la Engedi). Yehoshafati akashikwa na woga, akamwomba Mwenyezi-Mungu amwongoze. Akatangaza watu wote nchini Yuda wafunge. Watu wakaja Yerusalemu kutoka miji yote ya Yuda, wakakusanyika ili kumwomba Mwenyezi-Mungu awasaidie. Yehoshafati akasimama katikati ya kusanyiko la watu wa Yuda na Yerusalemu mbele ya ua mpya wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaomba kwa sauti akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zetu, wewe ndiwe Mungu uliye mbinguni! Wewe unazitawala falme zote duniani; unao uwezo na nguvu, wala hakuna awezaye kukupinga.
2 Mambo ya Nyakati 20:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya hayo, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani. Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng'ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio Engedi). Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza watu wote kufunga katika Yuda yote. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute BWANA; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta BWANA. Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa BWANA, mbele ya ua mpya; akasema, Ee BWANA, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu yeyote kusimama kinyume chako.
2 Mambo ya Nyakati 20:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani. Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng’ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi). Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute BWANA; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta BWANA. Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa BWANA, mbele ya ua mpya; akasema, Ee BWANA, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama kinyume chako.
2 Mambo ya Nyakati 20:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ikawa baada ya jambo hili, Wamoabu na Waamoni, pamoja na baadhi ya Wameuni wakaja ili wapigane vita na Yehoshafati. Watu fulani wakaja wakamwambia Yehoshafati, “Jeshi kubwa linakuja dhidi yako kutoka Edomu tokea ngʼambo ile nyingine ya Bahari. Tayari liko Hasason-Tamari” (yaani En-Gedi). Yehoshafati akaogopa, akaazimu kumtafuta BWANA, na akatangaza kwa Yuda wote kufunga. Watu wa Yuda wakakusanyika pamoja ili kutafuta msaada kutoka kwa BWANA. Wakaja kutoka kila mji wa Yuda ili kumtafuta. Kisha Yehoshafati akasimama katika kusanyiko la Yuda na Yerusalemu katika Hekalu la BWANA, mbele ya ua mpya, akasema: “Ee BWANA, Mungu wa baba zetu, si wewe ndiwe uliye Mungu mbinguni? Si wewe ndiwe utawalaye juu ya falme zote za mataifa? Uweza na nguvu viko mkononi mwako, wala hakuna yeyote awezaye kushindana nawe.