Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 20:1-27

2 Mambo ya Nyakati 20:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Baada ya hayo, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani. Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng'ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio Engedi). Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza watu wote kufunga katika Yuda yote. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute BWANA; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta BWANA. Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa BWANA, mbele ya ua mpya; akasema, Ee BWANA, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu yeyote kusimama kinyume chako. Si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Abrahamu rafiki yako hata milele? Nao walikaa humo, wamekujengea patakatifu pa jina lako humo, wakisema, Yakitujia mabaya, upanga, hukumu, au tauni, au njaa, tutasimama mbele ya nyumba hii, na mbele zako, (maana jina lako limo katika nyumba hii), na kukulilia katika shida yetu, nawe utasikia na kuokoa. Na sasa, tazama, wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, ambao hukuwaacha Israeli waingie katika nchi yao, walipotoka nchi ya Misri; lakini wakawageukia mbali, wasiwaharibu; tazama, jinsi wanavyotulipa, wakija kututupa toka milki yako, uliyoturithisha. Ee Mungu wetu, je! Hutawahukumu? Maana sisi hatuna uwezo juu ya jamii kubwa hii, wanaotujia juu yetu; wala hatujui tufanyeje; lakini macho yetu yanatazama kwako. Wakasimama Yuda wote mbele za BWANA, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao. Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na Roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu. Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa BWANA yuko pamoja nanyi. Yehoshafati akasujudu; wakaanguka mbele za BWANA Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia BWANA. Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu BWANA, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana. Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa. Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya Waamoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja kushambulia Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwashambulia wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakaanza kuuana wao kwa wao. Hata Yuda walipofika mnara wa ulinzi wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka. Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakakuta miongoni mwao mifugo wengi sana, mali, mavazi na vitu vya thamani, walivyojinyakulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana. Hata siku ya nne wakakusanyika katika bonde la Baraka; maana ndipo walipomtukuza BWANA; kwa hiyo jina lake mahali pale pakaitwa Bonde la Baraka hata leo. Kisha wakarudi, kila mtu wa Yuda na Yerusalemu, na Yehoshafati mbele yao, ili kuurudia Yerusalemu kwa furaha; kwa kuwa BWANA amewafurahisha juu ya adui zao.

2 Mambo ya Nyakati 20:1-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ikawa baada ya jambo hili, Wamoabu na Waamoni, pamoja na baadhi ya Wameuni wakaja ili wapigane vita na Yehoshafati. Watu fulani wakaja wakamwambia Yehoshafati, “Jeshi kubwa linakuja dhidi yako kutoka Edomu tokea ngʼambo ile nyingine ya Bahari. Tayari liko Hasason-Tamari” (yaani En-Gedi). Yehoshafati akaogopa, akaazimu kumtafuta BWANA, na akatangaza kwa Yuda wote kufunga. Watu wa Yuda wakakusanyika pamoja ili kutafuta msaada kutoka kwa BWANA. Wakaja kutoka kila mji wa Yuda ili kumtafuta. Kisha Yehoshafati akasimama katika kusanyiko la Yuda na Yerusalemu katika Hekalu la BWANA, mbele ya ua mpya, akasema: “Ee BWANA, Mungu wa baba zetu, si wewe ndiwe uliye Mungu mbinguni? Si wewe ndiwe utawalaye juu ya falme zote za mataifa? Uweza na nguvu viko mkononi mwako, wala hakuna yeyote awezaye kushindana nawe. Je, si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Abrahamu, rafiki yako, hata milele? Wameishi ndani yake na humo wamekujengea mahali patakatifu kwa ajili ya Jina lako, wakisema: ‘Kama maafa yakitujia, ikiwa ni upanga, hukumu, tauni, au njaa, tutasimama mbele zako, mbele ya Hekalu hili ambalo limeitwa kwa Jina lako na kukulilia katika shida yetu, nawe utatusikia na kutuokoa.’ “Lakini sasa hawa watu wa kutoka Amoni, Moabu na Mlima Seiri, ambao hukuwaruhusu Israeli wazivamie nchi zao wakati walitoka Misri, hivyo wakageukia mbali nao na hawakuwaangamiza, tazama jinsi wanavyotulipa kwa kuja kututupa nje ya milki uliyotupa sisi kuwa urithi. Ee Mungu wetu, je, wewe hutawahukumu? Kwa kuwa sisi hatuna uwezo wa kukabiliana na jeshi hili kubwa linalokuja kutushambulia. Sisi hatujui la kufanya, bali macho yetu yanakutazama wewe.” Watu wote wa Yuda pamoja na wake zao, watoto wao na wadogo wao wakasimama pale mbele za BWANA. Ndipo Roho wa BWANA akaja juu ya mtu mmoja jina lake Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, Mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi mzao wa Asafu alipokuwa amesimama katika kusanyiko. Akasema: “Sikilizeni, enyi Yuda wote nanyi nyote mkaao Yerusalemu, nawe Mfalme Yehoshafati! Hili ndilo BWANA asemalo kwenu, ‘Msiogope wala msifadhaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Kwa maana vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu. Kesho shukeni kukabiliana nao. Watakwea kwa kupandia Genge la Sisi, nanyi mtawakuta mwisho wa bonde, kabla ya Jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita hivi. Kaeni kwenye nafasi zenu, simameni imara na mkaone wokovu BWANA atakaowapatia, enyi Yuda na Yerusalemu. Msiogope, wala msifadhaike. Kesho tokeni mwende mkawakabili, naye BWANA atakuwa pamoja nanyi.’ ” Yehoshafati akainamisha uso wake chini, nao watu wote wa Yuda na Yerusalemu wakaanguka chini ili kuabudu mbele za BWANA. Ndipo baadhi ya Walawi kutoka kwa Wakohathi na kwa wana wa Kora wakasimama na kumsifu BWANA, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana. Asubuhi na mapema wakaondoka kuelekea Jangwa la Tekoa. Walipoanza safari, Yehoshafati akasimama akasema, “Nisikilizeni, enyi Yuda, na watu wa Yerusalemu! Mwaminini BWANA Mungu wenu, hivyo mtathibitika, wasadikini manabii wake nanyi mtafanikiwa. Alipomaliza kushauriana na watu, Yehoshafati akawaweka watu wa kumwimbia BWANA na kumsifu katika utukufu wa utakatifu wake walipokuwa wametangulia mbele ya jeshi, wakisema: “Mshukuruni BWANA kwa kuwa upendo wake wadumu milele.” Walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao dhidi ya watu wa Amoni, Moabu na wale wa Mlima Seiri waliokuwa wamekuja kuishambulia Yuda, nao wakashindwa. Watu wa Amoni na Moabu wakawainukia watu wa Mlima Seiri ili kuwaua na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kumaliza kuwachinja watu wa Seiri, wakaangamizana wao kwa wao. Yuda walipofika katika mnara wa ulinzi wa jangwani, wakaliangalia lile jeshi kubwa, wakaona ni maiti tupu zimetapakaa ardhini, wala hakuna yeyote aliyenusurika. Hivyo Yehoshafati na watu wake wakaenda kujitwalia nyara kutoka kwao, nao wakakuta humo wingi wa mifugo, mali, nguo na vitu vya thamani, ambavyo vilikuwa vingi zaidi ya vile walivyoweza kuchukua. Wakakusanya nyara kwa siku tatu kwa sababu zilikuwa nyingi mno. Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Beraka kwa maana huko ndiko walikomsifu BWANA. Ndiyo sababu linaitwa Bonde la Beraka mpaka leo. Kisha watu wote wa Yuda na Yerusalemu, wakiongozwa na Yehoshafati, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kwa kuwa BWANA alikuwa amewasababisha wafurahi juu ya adui zao.

2 Mambo ya Nyakati 20:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya muda, majeshi ya Moabu na Amoni pamoja na baadhi ya Wameuni, waliivamia Yuda. Watu kadhaa walikuja wakamwambia mfalme Yehoshafati, “Jeshi kubwa limekuja kukushambulia kutoka Edomu, ngambo ya Bahari ya Chumvi. Tayari wamekwisha teka Hasason-tamari.” (Hili ni jina lingine la Engedi). Yehoshafati akashikwa na woga, akamwomba Mwenyezi-Mungu amwongoze. Akatangaza watu wote nchini Yuda wafunge. Watu wakaja Yerusalemu kutoka miji yote ya Yuda, wakakusanyika ili kumwomba Mwenyezi-Mungu awasaidie. Yehoshafati akasimama katikati ya kusanyiko la watu wa Yuda na Yerusalemu mbele ya ua mpya wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaomba kwa sauti akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zetu, wewe ndiwe Mungu uliye mbinguni! Wewe unazitawala falme zote duniani; unao uwezo na nguvu, wala hakuna awezaye kukupinga. Ni wewe ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii wakati watu wako Israeli walipoingia katika nchi hii, ukawapa wazawa wa Abrahamu rafiki yako, iwe yao milele. Nao wamekaa humu, na kukujengea hekalu kwa heshima ya jina lako, wakijua kwamba wakipatwa na maafa yoyote, vita, maradhi mabaya, au njaa, basi watakuja na kusimama mbele ya nyumba hii mbele yako, wakulilie katika shida zao, nawe utawasikiliza na kuwaokoa. Sasa watu wa Amoni, Moabu na wa mlima Seiri, ambao hukuwaruhusu babu zetu washambulie nchi zao walipotoka Misri, wakapitia kandokando wasiwaangamize, tazama, jinsi wanavyotulipa. Wanakuja kututoa katika nchi yako uliyotupa iwe mali yetu. Wewe ndiwe Mungu wetu! Waadhibu, kwani sisi hatuna uwezo wowote mbele ya jeshi kubwa kama hili linalotujia. Hatujui la kufanya ila tunatazamia msaada kutoka kwako.” Wanaume wote wa Yuda, pamoja na wake zao na watoto wao, walikuwa wamesimama hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu. Ndipo Roho wa Mwenyezi-Mungu akamjia mmoja wa Walawi aliyekuwa hapo, jina lake Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, wa ukoo wa Asafu. Yahazieli akasema, “Sikilizeni watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu na mfalme Yehoshafati, Mwenyezi-Mungu awaambia hivi: Msiogope wala msihangaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu. Kesho washambulieni wakati watakapokuwa wakipanda Bonde la Sisi. Mtawakuta mwisho wa bonde, mashariki mwa jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita hivi. Nyinyi jipangeni tu halafu mngojee, na mtaona Mwenyezi-Mungu akiwashinda kwa niaba yenu. Enyi watu wa Yuda na Yerusalemu, msiogope wala msifadhaike. Nendeni vitani, naye Mwenyezi-Mungu atakuwa pamoja nanyi!” Hapo mfalme Yehoshafati akasujudu pamoja na watu wote wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu wakamsujudu na kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Walawi wa ukoo wa Kohathi na Kora, wakasimama na kumsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sauti kubwa sana. Kesho yake, wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda mpaka katika jangwa la Tekoa. Walipokuwa wanaondoka, Yehoshafati alisimama, akawaambia, “Nisikilizeni, enyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu! Mwaminini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nanyi mtakuwa imara. Muwe na imani na manabii wake, nanyi mtafaulu.” Baada ya kushauriana na watu, mfalme alichagua wanamuziki fulani, akawaagiza wajivike mavazi yao rasmi kisha watangulie mbele ya jeshi, wakiimba: “Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, maana fadhili zake zadumu milele!” Wakati walipoanza kuimba na kusifu, Mwenyezi-Mungu aliwavuruga akili wanajeshi wa Amoni, Moabu na wa Mlima Seiri waliokuja kupigana na Yuda. Na wanajeshi hao wakashindwa. Watu wa Amoni na wa Moabu wakawashambulia wenyeji wa mlima Seiri, na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kuwaangamiza wakazi wa mlima Seiri wakaanza kushambuliana wao kwa wao, wakaangamizana. Jeshi la Yuda lilipofika penye mnara wa ulinzi huko jangwani, waliangalia upande wa maadui, wakaona maiti zimetapakaa kila mahali. Hakuna mtu yeyote aliyenusurika. Yehoshafati na wanajeshi wake wakaenda kuchukua nyara wakakuta ng'ombe wengi, mali, nguo na vitu vingine vya thamani. Iliwachukua muda wa siku tatu kusomba nyara hizo, na hata hivyo, hawakuzimaliza kwani zilikuwa nyingi mno. Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Sifa, na kumsifu Mwenyezi-Mungu kwa yote aliyowafanyia. Ndio maana bonde hilo linaitwa Bonde la Sifa hadi hivi leo. Kisha Yehoshafati akawaongoza wanajeshi wake mpaka Yerusalemu kwa shangwe, kwa sababu Mwenyezi-Mungu aliwashinda maadui zao.

2 Mambo ya Nyakati 20:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani. Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng’ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi). Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute BWANA; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta BWANA. Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa BWANA, mbele ya ua mpya; akasema, Ee BWANA, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama kinyume chako. Si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Ibrahimu rafiki yako hata milele? Nao walikaa humo, wamekujengea patakatifu pa jina lako humo, wakisema, Yakitujia mabaya, upanga, hukumu, au tauni, au njaa, tutasimama mbele ya nyumba hii, na mbele zako, (maana jina lako limo katika nyumba hii), na kukulilia katika shida yetu, nawe utasikia na kuokoa. Na sasa, tazama, wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, ambao hukuwaacha Israeli waingie katika nchi yao, walipotoka nchi ya Misri; lakini wakawageukia mbali, wasiwaharibu; tazama, jinsi wanavyotulipa, wakija kututupa toka milki yako, uliyoturithisha. Ee Mungu wetu, je! Hutawahukumu? Maana sisi hatuna uwezo juu ya jamii kubwa hii, wanaotujia juu yetu; wala hatujui tufanyeje; lakini macho yetu yatazama kwako. Wakasimama Yuda wote mbele za BWANA, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao. Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu. Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa BWANA yu pamoja nanyi. Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za BWANA Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia BWANA. Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu BWANA, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana. Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa. Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka. Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakaona kati yao wingi wa mali, na mavazi, na johari za thamani, walivyojivulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana. Hata siku ya nne wakakusanyika katika bonde la Baraka; maana ndipo walipombarikia BWANA; kwa hiyo jina lake mahali pale pakaitwa Bonde la Baraka hata leo. Kisha wakarudi, kila mtu wa Yuda na Yerusalemu, na Yehoshafati mbele yao, ili kuurudia Yerusalemu kwa furaha; kwa kuwa BWANA amewafurahisha juu ya adui zao.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha