1 Timotheo 6:1-10
1 Timotheo 6:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wale wote walio chini ya kongwa la utumwa inawapasa kuwahesabu mabwana zao kuwa wanastahili heshima yote, ili jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu. Wale watumwa ambao wana mabwana waaminio, haiwapasi kupunguza heshima yao kwa sababu wao ni ndugu. Badala yake, wawatumikie hata vizuri zaidi, kwa sababu wale wanaonufaika na huduma yao ni waaminio, ambao ni wapenzi wao. Fundisha mambo haya na uwahimize kuyafuata. Ikiwa mtu yeyote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, huyo amejivuna wala hajui kitu chochote. Yeye amejaa tamaa ya mabishano na ugomvi kuhusu maneno ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya, na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida. Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.
1 Timotheo 6:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Watumwa wote wanapaswa kuwaheshimu wakuu wao ili kusiwe na sababu ya watu kulitukana jina la Mungu na mafundisho yetu. Watumwa ambao wakuu wao ni Wakristo wasiwadharau kwani ni ndugu zao. Badala yake, wanapaswa kuwatumikia hata vizuri zaidi, maana hao wanaopata faida kutokana na kazi yao ni waumini ambao wanawapenda. Unapaswa kufundisha na kuhubiri mambo haya. Mtu yeyote anayefundisha kinyume cha mambo haya, na ambaye hakubaliani na maneno ya kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo na mafundisho ya uchaji wa Mungu, huyo amejaa majivuno na wala hajui chochote. Ni mtu wa kupenda ubishi na magombano juu ya maneno matupu, na hiyo husababisha wivu, ugomvi, matusi, shuku mbaya, na ubishi usio na kikomo kutoka kwa watu ambao akili zao zimeharibika, na ambao hawana tena ukweli. Wanadhani dini ni njia ya kujipatia utajiri. Kweli kumcha Mungu humfanya mtu awe tajiri sana, ikiwa anatosheka na vitu alivyo navyo. Maana hatukuleta kitu chochote hapa duniani, wala hatutachukua chochote. Kwa hiyo basi, kama tunacho chakula na mavazi, tunapaswa kuridhika navyo. Lakini wale wanaotaka kutajirika huanguka katika majaribu, na kunaswa katika mtego wa tamaa nyingi mbaya za kipumbavu, ambazo huwavuta mpaka kwenye uharibifu na maangamizi. Kwa maana kupenda sana fedha ni chanzo cha uovu wote. Watu wengine wametamani sana kupata fedha hata wakatangatanga mbali na imani, na wameivunja mioyo yao kwa huzuni nyingi.
1 Timotheo 6:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wote walio chini ya nira ya utumwa, wawachukulie bwana zao kama wanaostahili heshima yote, ili jina la Mungu na mafundisho yetu yasitukanwe. Na wale walio na bwana waaminio wasiwadharau kwa kuwa ni ndugu; bali afadhali wawatumikie, kwa sababu hao wapatao faida ya kazi yao wamekuwa wenye imani na kupendwa. Mambo hayo uyafundishe na kuyahimiza. Mtu awaye yote akitoa mafundisho mengine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa, amejivuna; wala hafahamu neno lolote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matusi, na shuku mbaya; na kuzozana miongoni mwa watu waliopotoka katika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida. Lakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na mtego, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, zinazowaingiza watu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.
1 Timotheo 6:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wo wote walio chini ya kongwa, hali ya utumwa, na wawahesabie bwana zao kuwa wamestahili heshima yote, jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu. Na wale walio na bwana waaminio wasiwadharau kwa kuwa ni ndugu; bali afadhali wawatumikie, kwa sababu hao waishirikio faida ya kazi yao wamekuwa wenye imani na kupendwa. Mambo hayo uyafundishe na kuonya. Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa, amejivuna; wala hafahamu neno lo lote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya; na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida. Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.