1 Timotheo 5:9-16
1 Timotheo 5:9-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Usimtie katika orodha ya wajane mjane yeyote ambaye hajatimiza miaka sitini. Tena awe amepata kuolewa mara moja tu, na awe mwenye sifa nzuri: Aliyewalea watoto wake vizuri, aliyewakaribisha wageni nyumbani kwake, aliyewaosha miguu watu wa Mungu, aliyewasaidia watu wenye taabu, na aliyejitolea kufanya mambo mema. Usiwaandikishe wajane vijana, kwani kama tamaa zao za maumbile zikizidi kuwa na nguvu zaidi kuliko kujitolea kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena, na wataonekana kukosa uaminifu kuhusu ahadi yao ya pale awali. Wajane kama hao huanza kupoteza wakati wao wakizurura nyumba hata nyumba; tena ubaya zaidi ni kwamba huanza kuwasengenya watu, na kujitia katika mambo ya watu wengine, huku wakisema mambo ambayo hawangepaswa kusema. Kwa hiyo ningependelea wajane vijana waolewe, wapate watoto na kutunza nyumba zao ili maadui zetu wasipewe nafasi ya kusema mambo maovu juu yetu. Kwa maana wajane wengine wamekwisha potoka na kumfuata Shetani. Lakini kama mama Mkristo anao wajane katika jamaa yake, yeye anapaswa kuwatunza na si kuliachia kanisa mzigo huo, ili kanisa liweze kuwatunza wajane wale waliobaki peke yao kabisa.
1 Timotheo 5:9-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja; na awe ameshuhudiwa kwa matendo mema; katika kulea watoto, kuwa mkaribishaji, kuwaosha watakatifu miguu, kuwasaidia wateswao, na kujitolea kutenda wema katika hali zote. Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa; nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza. Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizungukazunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa. Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, watunze nyumba zao; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu. Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani. Mwanamke aaminiye, akiwa na jamaa walio wajane wa kweli, na awasaidie mwenyewe, kanisa lisilemewe; ili liwasaidie wale walio wajane kweli kweli.
1 Timotheo 5:9-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja; naye ameshuhudiwa kwa matendo mema; ikiwa amelea watoto, ikiwa amekaribisha wageni, ikiwa amewaosha watakatifu miguu, ikiwa amewasaidia wateswao, ikiwa amefuata kwa bidii kila tendo jema. Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa; nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza. Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizunguka-zunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa. Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu. Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani. Mwanamke aaminiye, akiwa ana wajane, na awasaidie mwenyewe, Kanisa lisilemewe; ili liwasaidie wale walio wajane kweli kweli.
1 Timotheo 5:9-16 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Mjane yeyote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na amekuwa mke wa mume mmoja; awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna. Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Al-Masihi, watataka kuolewa tena. Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza. Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema. Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu. Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani. Lakini kama mwanamke yeyote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kundi la waumini, ili lile kundi liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.