1 Timotheo 2:1-7
1 Timotheo 2:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwanza kabisa, nawasihi muombe dua, msali na kumshukuru Mungu kwa ajili ya watu wote, kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema. Jambo hili ni jema na lampendeza Mungu Mwokozi wetu, ambaye anataka watu wote waokolewe na wapate kuujua ukweli. Maana yuko Mungu mmoja, na pia yuko mmoja anayewapatanisha watu na Mungu, binadamu Kristo Yesu, ambaye alijitoa mwenyewe kuwakomboa watu wote. Huo ulikuwa uthibitisho, wakati ufaao ulipowadia, kwamba Mungu anataka kuwaokoa watu wote. Kwa sababu hiyo mimi nilitumwa niwe mtume na mwalimu wa watu wa mataifa, niutangaze ujumbe wa imani na ukweli. Nasema ukweli; sisemi uongo!
1 Timotheo 2:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake. Nami kwa ajili ya huo niliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli.
1 Timotheo 2:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake. Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli.
1 Timotheo 2:1-7 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Awali ya yote, nasihi kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote: kwa ajili ya wafalme na wale wote walio katika mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu. Jambo hili ni jema, tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu, anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli. Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Al-Masihi Isa, aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake ufaao. Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Al-Masihi wala sisemi uongo), mwalimu wa watu wa Mataifa katika imani na kweli.