1 Wathesalonike 5:1-8
1 Wathesalonike 5:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira ya mambo haya yatakapotukia. Maana nyinyi wenyewe mwajua kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku. Watu watakapokuwa wanasema: “Kila kitu ni shwari na salama”, ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo. Lakini nyinyi, ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi. Nyinyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza. Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi. Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku. Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma.
1 Wathesalonike 5:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini, ndugu, kuhusu nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua hakika ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwizi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafla, kama vile uchungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. Bali ninyi, ndugu, hamko gizani, hata siku ile iwapate kama mwizi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.
1 Wathesalonike 5:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.
1 Wathesalonike 5:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia, kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajapo usiku. Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka. Bali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi. Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku. Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi. Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku. Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo.