1 Wathesalonike 2:3-8
1 Wathesalonike 2:3-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana maonyo yetu siyo ya ukosefu, wala ya uchafu, wala ya hila; bali kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu. Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wo wote, kama mjuavyo, wala maneno ya juujuu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi. Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine tulipokuwa tukiweza kuwalemea kama mitume wa Kristo; bali tulikuwa wapole katikati yenu, kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe. Vivyo hivyo nasi tukiwatumaini kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu.
1 Wathesalonike 2:3-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Jambo tunalosisitiza kwenu si jambo linalotegemea uongo au nia mbaya; wala hatupendi kumdanganya mtu yeyote. Sisi twanena daima kama atakavyo Mungu kwani yeye alituona kwamba tunafaa, akatukabidhi hii Habari Njema. Si nia yetu kuwapendeza watu hata kidogo, bali twataka kumpendeza Mungu ambaye anajua mioyo yetu mpaka ndani. Maana kama mjuavyo, sisi hatukutumia maneno ya kubembeleza wala hatukutumia maneno ya kijanja ya kuficha ubinafsi fulani; Mungu ni shahidi! Hatukutafuta sifa kutoka kwa watu, wala kutoka kwenu, wala kutoka kwa mtu yeyote, ingawa sisi tukiwa mitume wa Kristo, tungeweza kudai mambo fulani kwenu. Lakini sisi tulikuwa wapole kati yenu kama alivyo mama kwa watoto wake. Tuliwapenda nyinyi sana hata tukawa tayari kuwashirikisha si tu Habari Njema ya Mungu, bali pia na maisha yetu. Ndivyo mlivyokuwa wapenzi wetu!
1 Wathesalonike 2:3-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana maonyo yetu siyo ya ukosefu, wala ya uchafu, wala ya hila; bali kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu. Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wowote, kama mjuavyo, wala maneno ya juu juu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi. Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine, ingawa tungeweza kuwalemea kama Mitume wa Kristo; bali tulikuwa wapole katikati yenu, kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe. Hivyo ndivyo nasi tukiwajali kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu.
1 Wathesalonike 2:3-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa maana himizo letu halikutokana na hila wala nia mbaya au udanganyifu. Kinyume chake, tulinena kama watu tuliokubaliwa na Mungu tukakabidhiwa Injili. Sisi hatujaribu kuwapendeza wanadamu bali kumpendeza Mungu, yeye ayachunguzaye mawazo ya ndani sana ya mioyo yetu. Kama mjuavyo, hatukuja kwenu kwa maneno ya kujipendekeza au maneno yasiyo ya kweli ili kuficha tamaa mbaya: Mungu ndiye shahidi yetu. Wala hatukuwa tunatafuta sifa kutoka kwa wanadamu, wala kutoka kwenu au kwa mtu mwingine awaye yote. Kama mitume wa Kristo tungaliweza kuwa mzigo kwenu, lakini tulikuwa wapole katikati yenu, kama mama anayewatunza watoto wake wadogo. Tuliwapenda sana kiasi kwamba tulifurahia kushirikiana nanyi, si Injili ya Mungu tu, bali hata maisha yetu, kwa sababu mlikuwa wa thamani mno kwetu.