1 Samueli 9:3-20
1 Samueli 9:3-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na punda za Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kishi akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao. Naye akapita kati ya nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita na kati ya nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita kati ya nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita kati ya nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata. Hata walipofika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye, Haya, na turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri sisi. Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu mwenye kuheshimiwa; yote asemayo hutukia kweli kweli; basi, twende huko; labda yeye aweza kutuambia habari ya safari yetu tunayoiendea. Ndipo Sauli akamwambia mtumishi wake, Lakini angalia, kama tukienda, tumpelekee mtu huyo kitu gani? Maana chakula kimekwisha vyomboni mwetu, wala hapana zawadi ya kumpelekea mtu wa Mungu; tuna nini sisi? Yule mtumishi akamjibu Sauli, akasema, Tazama, mkononi mwangu nina robo ya shekeli ya fedha; nitampa huyo mtu wa Mungu fedha hiyo, atuambie njia yetu. (Hapo zamani katika Israeli, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa Mwonaji.) Basi Sauli akamwambia mtumishi wake, Umesema vema; haya! Twende. Wakaenda mpaka mji ule aliokuwamo mtu wa Mungu. Hata walipokwea kwenda mjini, wakakutana na wasichana, wanatoka kwenda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko? Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu watu wana dhabihu leo katika mahali pa juu; mkiingia mjini tu, mara mtamwona, kabla hajakwea kwenda mahali pa juu ale chakula; maana, watu hawatakula hata yeye atakapokuja; kwa sababu yeye ndiye anayeibarikia dhabihu; kisha hao watu walioalikwa hula. Basi, kweeni sasa; maana wakati huu ndio mtakapomwona. Nao wakakwea kwenda mjini; nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli akawatokea, kwenda mahali pa juu. Basi BWANA alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema, Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia. Hata Samweli alipomwona Sauli, BWANA akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu. Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi? Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako. Na wale punda zako waliopotea siku hizi tatu, usijiudhi kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako?
1 Samueli 9:3-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, punda wa Kishi, baba yake Shauli, walipotea. Hivyo, Kishi akamwambia Shauli, “Mchukue mmoja wa watumishi, uende kuwatafuta punda.” Wakawatafuta kwenye nchi ya milima ya Efraimu na eneo la Shalisha, lakini hawakuwaona huko. Halafu wakafika Shalimu, na huko hawakuwaona. Wakawatafuta katika nchi ya Benyamini, hata hivyo hawakuwapata. Walipofika kwenye nchi ya Sufu, Shauli alimwambia mtumishi wake, “Turudi nyumbani, la sivyo baba yangu ataacha kufikiria juu ya punda, na badala yake atakuwa na wasiwasi juu yetu.” Yule mtumishi akamwambia, “Ngoja kidogo; katika mji huu kuna mtu wa Mungu ambaye anaheshimiwa sana; kila asemalo huwa kweli. Sasa tumwendee, labda anaweza kutuambia jinsi safari yetu itakavyokuwa.” Shauli akamwuliza, “Lakini tukimwendea, tutampa nini? Tazama, mikate katika mifuko yetu imekwisha na hatuna chochote cha kumpa huyo mtu wa Mungu. Tuna nini?” Yule mtumishi akamjibu Shauli, “Ona, mimi nina fedha robo shekeli. Nitampa huyo mtu wa Mungu ili atuambie juu ya safari yetu.” (Hapo awali katika Israeli kama mtu akitaka kumwomba Mungu shauri, alisema, “Haya, njoo, twende kwa mwonaji.” Kwani mtu anayeitwa nabii siku hizi hapo awali aliitwa mwonaji). Shauli akamjibu, “Hilo ni jambo jema; haya, twende.” Hivyo, wakaenda kwenye mji alimokuwa anakaa yule mtu wa Mungu. Walipokuwa wanapanda mlima kuelekea mjini, wakakutana na wasichana waliokuwa wakienda kuteka maji. Wakawauliza wasichana hao, “Je, mwonaji yuko mjini?” Wale wasichana wakawajibu, “Ndiyo, yuko. Tena yuko mbele yenu; mkifanya haraka mtamkuta. Ameingia tu mjini leo, kwa sababu leo watu watatambika huko mlimani. Mara mtakapoingia mjini, mtamkuta kabla hajaenda mahali pa ibada mlimani ili kula. Maana watu hawatakula mpaka kwanza yeye abariki tambiko. Baadaye wale walioalikwa watakula. Hivyo nendeni haraka; mtakutana naye mara.” Hivyo Shauli na mtumishi wake walikwenda mjini. Walipokuwa wanaingia mjini, walimwona Samueli akitoka mjini, na anaelekea mahali pa juu. Jana yake, kabla Shauli hajafika mjini hapo, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia hivi Samueli: “Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya kabila la Benyamini, nawe utampaka mafuta kuwa mtawala wa watu wangu Israeli. Yeye atawaokoa watu wangu kutoka kwa Wafilisti, kwani nimeyaona mateso ya watu wangu na kilio chao kimenifikia.” Samueli alipomwona tu Shauli, Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Huyu ndiye yule mtu niliyekuambia. Yeye ndiye atakayewatawala watu wangu.” Hapo Shauli alimwendea Samueli aliyekuwa karibu na lango la mji na kumwuliza, “Nakuomba unioneshe nyumba ya mwonaji.” Samueli akamjibu; “Mimi ndiye mwonaji. Nitangulieni kwenda mahali pa juu kwani leo mtakula pamoja nami. Kesho asubuhi maswali yote uliyo nayo nitayajibu. Kuhusu wale punda waliopotea siku tatu zilizopita, msiwe na wasiwasi juu yao; wamekwisha patikana. Lakini ni nani yule ambaye Waisraeli wanamtaka sana? Je, si wewe na jamaa yote ya baba yako?”
1 Samueli 9:3-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na punda wa Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kishi akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, chukua mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao. Naye akapita katika nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita katika nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita katika nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita katika nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata. Walipofika katika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye, Hebu turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri sisi. Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu anaheshimiwa; yote asemayo hutukia hakika; basi, twende huko; labda yeye anaweza kutuambia kuhusu safari yetu tunayoiendea. Ndipo Sauli akamwambia mtumishi wake, Lakini tukienda, tumpelekee mtu huyo kitu gani? Maana chakula kimekwisha vyomboni mwetu, wala hapana zawadi ya kumpelekea mtu wa Mungu; tuna nini sisi? Yule mtumishi akamjibu Sauli, akasema, Tazama, mkononi mwangu nina fedha robo ya shekeli; nitampa huyo mtu wa Mungu fedha hiyo, atuambie njia yetu. (Hapo zamani katika Israeli, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa Mwonaji.) Basi Sauli akamwambia mtumishi wake, Umesema vema; haya! Twende. Wakaenda mpaka mji ule aliokuwamo mtu wa Mungu. Walipokuwa wakikwea mjini, wakakutana na wasichana, waliokuwa wakienda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko? Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu watu wana dhabihu leo katika mahali pa juu; mkiingia mjini tu, mara mtamwona, kabla hajakwea kwenda mahali pa juu ale chakula; maana, watu hawatakula hadi yeye atakapokuja; kwa sababu yeye ndiye anayeibariki dhabihu; ndipo hao watu walioalikwa hula. Basi, kweeni sasa; maana wakati huu ndio mtakapomwona. Nao wakakwea kwenda mjini; nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli akawatokea, kwenda mahali pa juu. Basi BWANA alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema, Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikia. Hata Samweli alipomwona Sauli, BWANA akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia juu zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu. Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi? Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako. Na wale punda wako waliopotea siku hizi tatu, usisumbuke kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako?
1 Samueli 9:3-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi punda wa Kishi baba yake Sauli walipotea, naye Kishi akamwambia mwanawe Sauli, “Mchukue mmoja wa watumishi mwende pamoja naye kuwatafuta punda.” Hivyo akapita katika nchi ya vilima ya Efraimu na katika eneo la Shalisha, lakini hawakuwapata. Wakaendelea katika sehemu ya Shaalimu, lakini punda hawakuwepo huko. Kisha wakapita katika nchi ya Benyamini, lakini hawakuwapata. Walipofika sehemu ya Sufu, Sauli akamwambia mtumishi aliyekuwa pamoja naye, “Njoo, sisi na turudi, au baba yangu ataacha kufikiria juu ya punda na kuanza kufadhaika kutuhusu sisi.” Lakini mtumishi akajibu, “Tazama, katika mji huu yupo mtu wa Mungu, anayeheshimiwa sana na kila kitu asemacho hutokea kweli. Sasa na twende huko. Huenda atatuambia twende njia ipi.” Sauli akamwambia mtumishi wake, “Kama tukienda, tutampa nini huyo mtu? Chakula kimekwisha kwenye mifuko yetu. Hatuna zawadi ya kumpelekea huyo mtu wa Mungu. Je tuna nini?” Mtumishi akamjibu Sauli tena, akasema, “Tazama, nina fedha robo shekeli. Hiyo nitampa huyo mtu wa Mungu ili aweze kutuambia twende kwa njia ipi.” (Zamani katika Israeli, kama mtu alikwenda kuuliza neno kwa Mungu, angalisema, “Njoo na twende kwa mwonaji,” kwa sababu nabii wa sasa alikuwa akiitwa mwonaji.) Sauli akamwambia mtumishi wake, “Vyema, njoo na twende.” Basi wakaenda mjini alipokuwepo huyo mtu wa Mungu. Walipokuwa wakipanda mlima kwenda mjini, wakakutana na baadhi ya wasichana wanakuja kuchota maji, nao wakawauliza, “Je, mwonaji yuko?” Wakajibu, “Yuko, yu mbele yenu amewatangulia, sasa fanyeni haraka, ndiyo tu amekuja mjini kwetu leo, kwa kuwa watu wana dhabihu huko mahali pa juu. Mara tu mwingiapo mjini, mtamkuta kabla hajapanda kwenda mahali pa juu kula. Watu hawataanza kula mpaka atakapofika kwa sababu ni lazima kwanza yeye abariki dhabihu, ndipo wale walioalikwa watakapokula. Pandeni sasa, mtamkuta kwa wakati huu.” Wakapanda mjini, nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli alikuwa akija kuelekea walikokwenda mahali pa juu. Basi siku moja kabla Sauli hajaja, BWANA alikuwa amemfunulia Samweli jambo hili: “Kesho wakati kama huu nitakupelekea mtu kutoka nchi ya Benyamini. Umtie mafuta awe kiongozi juu ya watu wangu Israeli, ndiye atakayewakomboa watu wangu na mkono wa Wafilisti. Nimewaangalia watu wangu, kwa kuwa kilio chao kimenifikia.” Samweli alipomwona Sauli, BWANA akamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekuambia habari zake, kwamba yeye atawatawala watu wangu.” Sauli akamkaribia Samweli langoni na kumuuliza, “Tafadhali, je, waweza kuniambia mahali nyumba ya mwonaji ilipo?” Samweli akamjibu Sauli, “Mimi ndiye mwonaji, panda utangulie mbele yangu mpaka mahali pa juu, kwa kuwa leo itakupasa kula pamoja nami na asubuhi nitakuruhusu uende na nitakuambia yale yote yaliyo moyoni mwako. Kuhusu wale punda uliowapoteza siku tatu zilizopita, usifadhaike kwa habari yao; wamepatikana. Ni kwa nani ambaye shauku yote ya Israeli imeelekea, kama si kwako na jamaa yote ya baba yako?”