Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 25:1-39

1 Samueli 25:1-39 Biblia Habari Njema (BHN)

Sasa, Samueli alifariki; nao Waisraeli wote wakakusanyika ili kumwombolezea. Wakamzika nyumbani kwake huko Rama. Kisha Daudi akaenda zake kwenye nyika za Parani. Kulikuwa na mtu mmoja huko mjini Maoni ambaye alikuwa na biashara ya kondoo mjini Karmeli. Huko Karmeli alifuga kondoo wake na kuwakata manyoya. Alikuwa tajiri sana. Alikuwa na kondoo 3,000 na mbuzi 1,000. Mtu huyo aliitwa Nabali na mkewe aliitwa Abigaili. Abigaili alikuwa mwanamke mwenye akili na mzuri. Lakini Nabali alikuwa mtu wa chuki na duni; tena alikuwa wa ukoo wa Kalebu. Basi, Daudi akiwa huko nyikani alisikia kwamba Nabali alikuwa anawakata kondoo wake manyoya huko Karmeli. Hivyo, akawatuma vijana kumi, akawaambia, “Nendeni kwa Nabali huko Karmeli mkampelekee salamu zangu. Mtamwambia kwamba Daudi anakusalimu hivi: ‘Amani iwe kwako, kwa jamaa yako na yote uliyo nayo. Nimesikia kwamba unawakata manyoya kondoo wako nataka ujue kwamba wachungaji wako walikuwa pamoja nasi, nasi hatukuwadhuru. Tena muda wote walipokuwa pamoja nasi mjini Karmeli, hawakukosa chochote. Ukiwauliza, watakuambia. Sasa nakuomba vijana wangu hawa wapate kibali mbele yako, kwani tumefika wakati wa sikukuu. Tafadhali uwapatie chochote ulicho nacho watumishi wako hawa nami mwanao Daudi.’” Wale vijana wa Daudi walikwenda na kumwambia Nabali kama walivyoagizwa na Daudi. Halafu wakasubiri kidogo. Kisha Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Daudi ni nani? Mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumishi wengi wanaowakimbia mabwana zao. Je, nichukue mikate yangu, maji yangu na nyama niliyowachinjia wakata-manyoya ya kondoo wangu na kuwapa watu ambao sijui hata wanakotoka?” Basi, wale vijana wa Daudi walirudi na kumwambia Daudi walivyojibiwa. Hivyo Daudi akawaambia watu wake, “Kila mtu na ajifunge upanga wake kiunoni.” Kila mtu akajifunga upanga wake, na Daudi pia akajifunga upanga wake; watu wapatao 400 wakamfuata Daudi na watu 200 wakabaki na mizigo. Kijana mmoja wa Nabali, akamwambia Abigaili, mkewe Nabali, “Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani ili kumsalimu bwana wetu. Lakini yeye aliwatukana. Lakini watu hao walikuwa wema sana kwetu, hawakutudhuru; na wakati wote tulipokuwa nao huko nyikani hatukukosa chochote. Kwetu, walikuwa kama ukuta wa ulinzi usiku na mchana muda wote tulipokuwa tunawachunga kondoo. Sasa fikiria juu ya jambo hili na uamue la kufanya. Jambo hili laweza kuleta madhara kwa bwana wetu na jamaa yake yote. Yeye ni mtu mbaya na hakuna anayeweza kuzungumza naye.” Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate 200, viriba viwili vya divai, kondoo watano walioandaliwa vizuri, kilo kumi na saba za bisi, vishada 100 vya zabibu kavu, mikate ya tini 200, na vitu hivi vyote akavipakia juu ya punda. Akamwambia yule kijana wake, “Tangulia! Mimi nitakufuata.” Lakini hakumwambia mumewe lolote. Alipokuwa anateremka, amepanda punda wake, na kukingwa na mlima upande mmoja, akakutana kwa ghafla na Daudi na watu wake wakiwa wanaelekea upande anakotoka. Daudi alikuwa akifikiri, “Mimi nimekuwa nikilinda mali yote ya Nabali nyikani bila faida yoyote na hakuna kitu chake chochote kilichopotea, naye amenilipa mabaya kwa mema niliyomtendea. Mungu na aniue mimi ikiwa kesho asubuhi nitakuwa sijawaua wanaume wake wote.” Abigaili alipomwona tu Daudi, akashuka mara moja kutoka juu ya punda wake, na kuinama mbele ya Daudi hadi uso wake ukagusa chini. Alijitupa miguuni pa Daudi na kumwambia, “Bwana wangu, hatia yote na iwe juu yangu tu. Nakuomba niongee nawe mimi mtumishi wako. Nakuomba usikilize maneno ya mtumishi wako. Usimfikirie Nabali ambaye ni mtu mbaya kwani lilivyo jina lake Nabali, ndivyo naye alivyo. Yeye anaitwa Nabali; na kweli yeye ni mtu mpumbavu. Bwana wangu, wale vijana wako ulipowatuma, mimi mtumishi wako sikuwaona. Sasa bwana wangu, naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, na vile ulivyo hai, kwamba kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekuzuia usilipize kisasi kwa kumwaga damu na kujipatia lawama, waache adui zako na wale wote wanaokutakia mabaya wawe wapumbavu kama Nabali. Bwana wangu, nakuomba upokee zawadi hii niliyokuletea, na uwape vijana wanaokufuata. Nakuomba unisamehe mimi mtumishi wako. Mwenyezi-Mungu atakupa jamaa imara kwa sababu, wewe bwana wangu, unapigana vita vya Mwenyezi-Mungu. Wakati wote wa maisha yako usipatikane na baa lolote. Kukitokea watu wakikufuatilia na kutaka kuyaangamiza maisha yako, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atayasalimisha maisha yako pamoja na walio hai. Lakini maisha ya adui zako atayatupilia mbali, kama vile mtu atupavyo jiwe kwa kombeo. Baada ya Mwenyezi-Mungu kukutendea mema yote aliyokuahidi, na kukuteua kuwa mtawala wa Israeli, wewe bwana wangu, hutakuwa na sababu ya kujuta wala kuhukumiwa na dhamiri kutokana na kumwaga damu bila sababu kwa kujilipiza kisasi. Lakini, bwana wangu, Mwenyezi-Mungu atakapokuwa amekutendea wema huo, nakuomba unikumbuke mimi mtumishi wako.” Daudi akamwambia Abigaili, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliyekutuma leo kukutana nami. Mtukuze Mwenyezi-Mungu aliyekupa busara kwa kunizuia kuwa na hatia ya umwagaji damu na kujilipiza kisasi mimi mwenyewe. Kwa hakika, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, amenizuia nisikudhuru. Usingefanya haraka kuja kukutana nami, kwa hakika, kesho asubuhi hakuna mwanamume yeyote wa Nabali angesalia.” Kisha, Daudi akapokea vitu vyote ambavyo Abigaili alikuwa amemletea, akamwambia Abigaili, “Rudi nyumbani kwako kwa amani. Tazama, mimi nimeyasikia uliyoyasema, na ombi lako nimelipokea.” Abigaili aliporudi nyumbani, alimkuta Nabali akifanya karamu kubwa nyumbani kwake kama ya kifalme. Nabali alikuwa ameburudika sana moyoni kwani alikuwa amelewa sana. Hivyo hakumwambia lolote mpaka asubuhi. Asubuhi, Abigaili alipoona mumewe divai imemtoka, alimweleza mambo yote, na papo hapo Nabali akapooza, akawa kama jiwe. Siku kumi baadaye, Mwenyezi-Mungu alimpiga Nabali akafa. Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, alisema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amemlipiza kisasi Nabali kwa kunitukana, naye Mwenyezi-Mungu ameniepusha mimi mtumishi wake kutenda maovu. Mwenyezi-Mungu amempatiliza Nabali kwa uovu wake.” Kisha Daudi alituma watu ili wamposee Abigaili awe mke wake.

1 Samueli 25:1-39 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Akafa Samweli; nao Israeli wote wakakusanyika, wakamwomboleza, wakamzika nyumbani mwake huko Rama. Kisha Daudi akaondoka, akashuka mpaka nyikani mwa Maoni. Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa tajiri sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu moja; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo wake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa mkosa adabu na mwovu; naye alikuwa wa ukoo wa Kalebu. Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa akiwakata manyoya kondoo wake. Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mkampe salamu zangu; na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo wako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli. Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, chochote kitakachokujia mkononi, uwape watumishi wako na mwanao Daudi. Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali kama walivyoambiwa na Daudi, kisha wakanyamaza. Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumishi wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake! Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao kondoo wangu manyoya, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi? Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia kama walivyoambiwa. Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wakiwa kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao. Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, akasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana. Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu chochote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako malishoni; watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo. Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye. Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliotayarishwa, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia moja vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda. Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali. Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kuteremka akiwa amekingwa na mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta. Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu chochote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema. Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mmoja wa kiume, kutakapopambazuka. Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifudifudi, akainama mpaka chini. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma. Basi sasa, bwana wangu, aishivyo BWANA, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa BWANA amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali. Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu. Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika BWANA atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya BWANA; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote. Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na BWANA, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya kombeo. Tena itakuwa, hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli; hili halitakuwa kikwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako. Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki; na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe. Kwa kuwa ni kweli, aishivyo BWANA, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba usingalifanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mmoja wa kiume, kutakapopambazuka. Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimelikubali ombi lako. Kisha Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hadi kulipopambazuka. Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe. Tena ikawa, yapata siku kumi baadaye, BWANA alimpiga huyo Nabali, hadi akafa. Naye Daudi aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, alisema, Na ahimidiwe BWANA ambaye amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumishi wake asitende maovu; tena uovu wake Nabali BWANA amemrudishia juu ya kichwa chake mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe.

1 Samueli 25:1-39 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Akafa Samweli; nao Israeli wote wakakusanyika, wakamwomboleza, wakamzika nyumbani mwake huko Rama. Kisha Daudi akaondoka, akashuka mpaka nyikani mwa Maoni. Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu. Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya kondoo zake. Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie; na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli. Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi. Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali sawasawa na maneno hayo yote kwa jina la Daudi, kisha wakanyamaza. Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake! Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi? Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia sawasawa na maneno hayo yote. Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wapata kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao. Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, kasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana. Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni; watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo. Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye. Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda. Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali. Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kutelemka penye sitara ya mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta. Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu cho chote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema. Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi. Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma. Basi sasa, bwana wangu, aishivyo BWANA, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa BWANA amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali. Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu. Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika BWANA atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya BWANA; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote. Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na BWANA, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya teo. Tena itakuwa, hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli; hili halitakuwa kwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako. Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki; na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe. Kwa kuwa ni kweli, aishivyo BWANA, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba hungefanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi. Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako. Kisha Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hata kulipopambazuka. Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe. Tena ikawa, yapata siku kumi baadaye, BWANA alimpiga huyo Nabali, hata akafa. Naye aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, Daudi alisema, Na ahimidiwe BWANA ambaye amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumwa wake asitende maovu; tena uovu wake Nabali BWANA amemrudishia juu ya kichwa chake mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe.

1 Samueli 25:1-39 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi Samweli akafa, nao Israeli wote wakakusanyika na kumwombolezea; wakamzika nyumbani kwake huko Rama. Kisha Daudi akateremka kwenye Jangwa la Maoni. Mtu mmoja huko Maoni, aliyekuwa na makao huko Karmeli, alikuwa tajiri sana. Alikuwa na mbuzi elfu moja na kondoo elfu tatu, aliokuwa akiwakata manyoya huko Karmeli. Jina la mtu huyo lilikuwa Nabali, naye mkewe aliitwa Abigaili. Alikuwa mwanamke mwenye busara na mzuri wa sura, lakini mumewe, ambaye alikuwa wa ukoo wa Kalebu, alikuwa mwenye hasira na mchoyo katika utendaji wake. Daudi alipokuwa huko jangwani, akasikia kuwa Nabali alikuwa anakata kondoo manyoya. Basi akatuma vijana kumi na kuwaambia, “Pandeni kwa Nabali huko Karmeli, mkamsalimie kwa jina langu. Mwambieni: ‘Amani iwe kwako! Amani iwe kwako pamoja na wa nyumbani mwako! Pia amani iwe pamoja na vyote ulivyo navyo! “ ‘Nasikia kuwa huu ni wakati wa kukata kondoo manyoya. Wachunga mifugo wako walipokuwa pamoja nasi, hatukuwatendea mabaya na wakati wote waliokuwa huko Karmeli hakuna chochote chao kilipotea. Waulize watumishi wako nao watakuambia. Kwa hiyo uwatendee wema vijana wangu, kwani tumekuja wakati wa furaha. Tafadhali wape watumishi wako na mwanao Daudi chochote kitakachokuja mkononi mwako kwa ajili yao.’ ” Watu wa Daudi walipofika wakampa Nabali ujumbe huu kwa jina la Daudi. Kisha wakangojea. Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Huyu Daudi ni nani? Huyu mwana wa Yese ni nani? Watumishi wengi wanakimbia kutoka kwa bwana zao siku hizi. Kwa nini nichukue mkate wangu, maji yangu na nyama niliyochinja kwa ajili ya wakata manyoya wangu, na kuwapa watu ambao hakuna anayejua wanakotoka?” Watu wa Daudi wakageuka na kurudi. Walipofika, wakaarifu kila neno. Daudi akawaambia watu wake, “Jifungeni panga zenu!” Basi wakajifunga panga zao, naye Daudi akajifunga upanga wake. Watu kama mia nne hivi wakapanda pamoja na Daudi, na watu mia mbili wakabaki na vifaa. Mmoja wa watumishi akamwambia Abigaili, mkewe Nabali: “Daudi alituma wajumbe kutoka jangwani kumpa bwana wetu salamu zake, lakini akawavurumishia matukano. Hata hivyo watu hawa walikuwa wema sana kwetu. Hawakututendea mabaya, na wakati wote tulipokuwa nje huko mashambani karibu nao, hatukupotewa na kitu chochote. Usiku na mchana walikuwa ukuta wakituzunguka wakati wote tulipokuwa tukichunga kondoo zetu karibu nao. Sasa fikiri juu ya jambo hili na uone unaweza kufanya nini, kwa sababu maafa yanakaribia juu ya bwana wetu na nyumba yake yote. Yeye ni mtu mwovu kiasi kwamba hakuna mtu awezaye kuzungumza naye.” Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate mia mbili, viriba viwili vya divai, kondoo watano waliochinjwa vipimo vitano vya bisi, vishada mia moja vya zabibu kavu, mikate mia mbili ya tini, akavipakia juu ya punda. Kisha akawaambia watumishi wake, “Tangulieni; mimi nitakuja nyuma yenu.” Lakini hakumwambia Nabali mumewe. Ikawa alipokuwa amepanda punda wake kwenye bonde la mlima, tazama, Daudi na watu wake wakawa wanateremka kumwelekea, naye akakutana nao. Daudi alikuwa amesema, “Ilikuwa ni kazi bure kuchunga kwangu kote mali za huyu mtu huko jangwani hivi kwamba hakuna chochote chake kilichopotea. Yeye amenilipa baya kwa ajili ya wema. BWANA na amshughulikie Daudi, tena kwa ukali, ikiwa kesho asubuhi nitambakizia mwanaume hata mmoja aliye hai miongoni mwa watu wake wote!” Abigaili alipomwona Daudi, akashuka haraka kwenye punda wake, akainama kifudifudi uso wake mpaka nchi mbele ya Daudi. Akamwangukia miguuni pake na kusema: “Bwana wangu, kosa hili na liwe juu yangu mwenyewe. Tafadhali mruhusu mtumishi wako aseme nawe. Sikia kile mtumishi wako atakachosema. Bwana wangu na asimjali huyo mtu mwovu Nabali. Yeye anafanana na jina lake; jina lake ni Mpumbavu, nao upumbavu huenda pamoja naye. Lakini kwangu mimi, mtumishi wako, sikuwaona hao watu waliotumwa na bwana wangu. “Basi sasa, kwa kuwa BWANA amekuzuia, wewe bwana wangu, kutokumwaga damu na kutolipiza kisasi kwa mikono yako mwenyewe, hakika kama BWANA aishivyo na kama uishivyo, maadui zako na wote wanaokusudia kumdhuru bwana wangu wawe kama Nabali. Nayo zawadi hii ambayo mtumishi wako amemletea bwana wangu, wapewe watu wanaofuatana nawe. Tafadhali samehe kosa la mtumishi wako, kwa kuwa BWANA kwa hakika ataifanya imara nyumba ya ufalme kwa bwana wangu, kwa sababu anapigana vita vya BWANA. Hata ingawa yuko mtu anayekufuatia kuuondoa uhai wako, usiruhusu baya lolote kuonekana kwako siku zote za maisha yako, uhai wa bwana wangu utafungwa salama kwenye furushi la walio hai na BWANA Mungu wako. Lakini uhai wa adui zako atavurumishwa kama vile jiwe kutoka kwenye kombeo. BWANA atakapokuwa ameshamtendea bwana wangu kila kitu chema alichoahidi kumhusu yeye na kumweka kuwa kiongozi wa Israeli, bwana wangu hatakuwa na dhamiri inayolemewa na mzigo kwa kumwaga damu kusiko na sababu, au kujilipizia kisasi yeye mwenyewe. BWANA atakapomletea bwana wangu mafanikio, umkumbuke mtumishi wako.” Daudi akamwambia Abigaili, “Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli aliyekutuma kunilaki leo. Ubarikiwe kwa uamuzi wako mzuri na kwa kunizuia nisimwage damu leo na kulipiza kisasi kwa mikono yangu. La sivyo, hakika kama BWANA, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye amenizuia nisiwadhuru, kama usingekuja haraka kunilaki, hakuna hata mwanaume mmoja wa Nabali angeachwa hai kufikia mapambazuko.” Ndipo Daudi akapokea kutoka mkononi mwake kile alichokuwa amemletea, naye akasema, “Nenda nyumbani kwako kwa amani; nimesikia maneno yako na kukujalia ombi lako.” Abigaili alipokwenda kwa Nabali, alikuwa ndani ya nyumba yake akifanya karamu kama ile ya mfalme. Naye alikuwa ana furaha nyingi, akiwa amelewa sana. Kwa hiyo Abigaili hakumwambia mumewe kitu chochote mpaka asubuhi yake. Basi asubuhi, Nabali alipokuwa amelevuka, mkewe akamwambia mambo yote, nao moyo wake ukazimia, akawa kama jiwe. Baada ya siku kumi, BWANA akampiga Nabali, naye akafa. Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, akasema, “Ahimidiwe BWANA, ambaye amenitetea shauri langu dhidi ya Nabali kwa kuwa alinitendea kwa dharau. Amemzuia mtumishi wake asitende mabaya na BWANA ameuleta ubaya wa Nabali juu ya kichwa chake mwenyewe.” Kisha Daudi akatuma ujumbe kwa Abigaili kumwomba awe mke wake.