1 Samueli 25:1-22
1 Samueli 25:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Sasa, Samueli alifariki; nao Waisraeli wote wakakusanyika ili kumwombolezea. Wakamzika nyumbani kwake huko Rama. Kisha Daudi akaenda zake kwenye nyika za Parani. Kulikuwa na mtu mmoja huko mjini Maoni ambaye alikuwa na biashara ya kondoo mjini Karmeli. Huko Karmeli alifuga kondoo wake na kuwakata manyoya. Alikuwa tajiri sana. Alikuwa na kondoo 3,000 na mbuzi 1,000. Mtu huyo aliitwa Nabali na mkewe aliitwa Abigaili. Abigaili alikuwa mwanamke mwenye akili na mzuri. Lakini Nabali alikuwa mtu wa chuki na duni; tena alikuwa wa ukoo wa Kalebu. Basi, Daudi akiwa huko nyikani alisikia kwamba Nabali alikuwa anawakata kondoo wake manyoya huko Karmeli. Hivyo, akawatuma vijana kumi, akawaambia, “Nendeni kwa Nabali huko Karmeli mkampelekee salamu zangu. Mtamwambia kwamba Daudi anakusalimu hivi: ‘Amani iwe kwako, kwa jamaa yako na yote uliyo nayo. Nimesikia kwamba unawakata manyoya kondoo wako nataka ujue kwamba wachungaji wako walikuwa pamoja nasi, nasi hatukuwadhuru. Tena muda wote walipokuwa pamoja nasi mjini Karmeli, hawakukosa chochote. Ukiwauliza, watakuambia. Sasa nakuomba vijana wangu hawa wapate kibali mbele yako, kwani tumefika wakati wa sikukuu. Tafadhali uwapatie chochote ulicho nacho watumishi wako hawa nami mwanao Daudi.’” Wale vijana wa Daudi walikwenda na kumwambia Nabali kama walivyoagizwa na Daudi. Halafu wakasubiri kidogo. Kisha Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Daudi ni nani? Mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumishi wengi wanaowakimbia mabwana zao. Je, nichukue mikate yangu, maji yangu na nyama niliyowachinjia wakata-manyoya ya kondoo wangu na kuwapa watu ambao sijui hata wanakotoka?” Basi, wale vijana wa Daudi walirudi na kumwambia Daudi walivyojibiwa. Hivyo Daudi akawaambia watu wake, “Kila mtu na ajifunge upanga wake kiunoni.” Kila mtu akajifunga upanga wake, na Daudi pia akajifunga upanga wake; watu wapatao 400 wakamfuata Daudi na watu 200 wakabaki na mizigo. Kijana mmoja wa Nabali, akamwambia Abigaili, mkewe Nabali, “Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani ili kumsalimu bwana wetu. Lakini yeye aliwatukana. Lakini watu hao walikuwa wema sana kwetu, hawakutudhuru; na wakati wote tulipokuwa nao huko nyikani hatukukosa chochote. Kwetu, walikuwa kama ukuta wa ulinzi usiku na mchana muda wote tulipokuwa tunawachunga kondoo. Sasa fikiria juu ya jambo hili na uamue la kufanya. Jambo hili laweza kuleta madhara kwa bwana wetu na jamaa yake yote. Yeye ni mtu mbaya na hakuna anayeweza kuzungumza naye.” Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate 200, viriba viwili vya divai, kondoo watano walioandaliwa vizuri, kilo kumi na saba za bisi, vishada 100 vya zabibu kavu, mikate ya tini 200, na vitu hivi vyote akavipakia juu ya punda. Akamwambia yule kijana wake, “Tangulia! Mimi nitakufuata.” Lakini hakumwambia mumewe lolote. Alipokuwa anateremka, amepanda punda wake, na kukingwa na mlima upande mmoja, akakutana kwa ghafla na Daudi na watu wake wakiwa wanaelekea upande anakotoka. Daudi alikuwa akifikiri, “Mimi nimekuwa nikilinda mali yote ya Nabali nyikani bila faida yoyote na hakuna kitu chake chochote kilichopotea, naye amenilipa mabaya kwa mema niliyomtendea. Mungu na aniue mimi ikiwa kesho asubuhi nitakuwa sijawaua wanaume wake wote.”
1 Samueli 25:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akafa Samweli; nao Israeli wote wakakusanyika, wakamwomboleza, wakamzika nyumbani mwake huko Rama. Kisha Daudi akaondoka, akashuka mpaka nyikani mwa Maoni. Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa tajiri sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu moja; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo wake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa mkosa adabu na mwovu; naye alikuwa wa ukoo wa Kalebu. Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa akiwakata manyoya kondoo wake. Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mkampe salamu zangu; na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo wako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli. Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, chochote kitakachokujia mkononi, uwape watumishi wako na mwanao Daudi. Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali kama walivyoambiwa na Daudi, kisha wakanyamaza. Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumishi wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake! Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao kondoo wangu manyoya, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi? Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia kama walivyoambiwa. Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wakiwa kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao. Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, akasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana. Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu chochote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako malishoni; watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo. Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye. Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliotayarishwa, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia moja vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda. Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali. Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kuteremka akiwa amekingwa na mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta. Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu chochote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema. Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mmoja wa kiume, kutakapopambazuka.
1 Samueli 25:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi Samweli akafa, nao Israeli wote wakakusanyika na kumwombolezea; wakamzika nyumbani kwake huko Rama. Kisha Daudi akateremka kwenye Jangwa la Maoni. Mtu mmoja huko Maoni, aliyekuwa na makao huko Karmeli, alikuwa tajiri sana. Alikuwa na mbuzi elfu moja na kondoo elfu tatu, aliokuwa akiwakata manyoya huko Karmeli. Jina la mtu huyo lilikuwa Nabali, naye mkewe aliitwa Abigaili. Alikuwa mwanamke mwenye busara na mzuri wa sura, lakini mumewe, ambaye alikuwa wa ukoo wa Kalebu, alikuwa mwenye hasira na mchoyo katika utendaji wake. Daudi alipokuwa huko jangwani, akasikia kuwa Nabali alikuwa anakata kondoo manyoya. Basi akatuma vijana kumi na kuwaambia, “Pandeni kwa Nabali huko Karmeli, mkamsalimie kwa jina langu. Mwambieni: ‘Amani iwe kwako! Amani iwe kwako pamoja na wa nyumbani mwako! Pia amani iwe pamoja na vyote ulivyo navyo! “ ‘Nasikia kuwa huu ni wakati wa kukata kondoo manyoya. Wachunga mifugo wako walipokuwa pamoja nasi, hatukuwatendea mabaya na wakati wote waliokuwa huko Karmeli hakuna chochote chao kilipotea. Waulize watumishi wako nao watakuambia. Kwa hiyo uwatendee wema vijana wangu, kwani tumekuja wakati wa furaha. Tafadhali wape watumishi wako na mwanao Daudi chochote kitakachokuja mkononi mwako kwa ajili yao.’ ” Watu wa Daudi walipofika wakampa Nabali ujumbe huu kwa jina la Daudi. Kisha wakangojea. Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Huyu Daudi ni nani? Huyu mwana wa Yese ni nani? Watumishi wengi wanakimbia kutoka kwa bwana zao siku hizi. Kwa nini nichukue mkate wangu, maji yangu na nyama niliyochinja kwa ajili ya wakata manyoya wangu, na kuwapa watu ambao hakuna anayejua wanakotoka?” Watu wa Daudi wakageuka na kurudi. Walipofika, wakaarifu kila neno. Daudi akawaambia watu wake, “Jifungeni panga zenu!” Basi wakajifunga panga zao, naye Daudi akajifunga upanga wake. Watu kama mia nne hivi wakapanda pamoja na Daudi, na watu mia mbili wakabaki na vifaa. Mmoja wa watumishi akamwambia Abigaili, mkewe Nabali: “Daudi alituma wajumbe kutoka jangwani kumpa bwana wetu salamu zake, lakini akawavurumishia matukano. Hata hivyo watu hawa walikuwa wema sana kwetu. Hawakututendea mabaya, na wakati wote tulipokuwa nje huko mashambani karibu nao, hatukupotewa na kitu chochote. Usiku na mchana walikuwa ukuta wakituzunguka wakati wote tulipokuwa tukichunga kondoo zetu karibu nao. Sasa fikiri juu ya jambo hili na uone unaweza kufanya nini, kwa sababu maafa yanakaribia juu ya bwana wetu na nyumba yake yote. Yeye ni mtu mwovu kiasi kwamba hakuna mtu awezaye kuzungumza naye.” Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate mia mbili, viriba viwili vya divai, kondoo watano waliochinjwa vipimo vitano vya bisi, vishada mia moja vya zabibu kavu, mikate mia mbili ya tini, akavipakia juu ya punda. Kisha akawaambia watumishi wake, “Tangulieni; mimi nitakuja nyuma yenu.” Lakini hakumwambia Nabali mumewe. Ikawa alipokuwa amepanda punda wake kwenye bonde la mlima, tazama, Daudi na watu wake wakawa wanateremka kumwelekea, naye akakutana nao. Daudi alikuwa amesema, “Ilikuwa ni kazi bure kuchunga kwangu kote mali za huyu mtu huko jangwani hivi kwamba hakuna chochote chake kilichopotea. Yeye amenilipa baya kwa ajili ya wema. BWANA na amshughulikie Daudi, tena kwa ukali, ikiwa kesho asubuhi nitambakizia mwanaume hata mmoja aliye hai miongoni mwa watu wake wote!”
1 Samueli 25:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akafa Samweli; nao Israeli wote wakakusanyika, wakamwomboleza, wakamzika nyumbani mwake huko Rama. Kisha Daudi akaondoka, akashuka mpaka nyikani mwa Maoni. Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu. Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya kondoo zake. Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie; na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli. Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi. Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali sawasawa na maneno hayo yote kwa jina la Daudi, kisha wakanyamaza. Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake! Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi? Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia sawasawa na maneno hayo yote. Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wapata kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao. Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, kasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana. Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni; watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo. Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye. Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda. Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali. Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kutelemka penye sitara ya mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta. Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu cho chote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema. Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi.