Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 24:2-11

1 Samueli 24:2-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Shauli aliwachukua askari 3,000 wateule waliokuwa bora zaidi katika nchi yote ya Israeli, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake katika Miamba ya Mbuzimwitu. Shauli alipokuwa anasafiri, alifika kwenye pango moja lililokuwa karibu na zizi la kondoo, akaingia humo pangoni ili kujisaidia. Daudi na watu wake walikuwa wameketi ndani kabisa ya pango hilo. Watu wa Daudi wakamwambia, “Ile siku aliyokuambia Mwenyezi-Mungu kuwa atakuja kumtia adui yako mikononi mwako nawe umtendee utakavyoona inafaa, leo imefika.” Ndipo Daudi alipomwendea Shauli polepole kutoka nyuma, akakata pindo la vazi lake. Daudi akaanza kufadhaika moyoni kwa sababu alikata pindo la vazi la Shauli kwa siri. Akawaambia watu wake, “Mwenyezi-Mungu anizuie nisimtendee kitendo kama hiki bwana wangu aliyepakwa mafuta na Mwenyezi-Mungu. Nisiunyoshe mkono wangu dhidi ya mtu ambaye Mwenyezi-Mungu amempaka mafuta.” Kwa maneno hayo, Daudi akawashawishi watu wake wasimdhuru Shauli; aliwakataza wasimshambulie. Kisha Shauli akasimama, akatoka pangoni akaendelea na safari yake. Baadaye, Daudi naye akainuka, akatoka pangoni na kumwita Shauli, “Bwana wangu mfalme!” Mfalme Shauli alipoangalia nyuma, Daudi aliinama hadi chini, akamsujudia Shauli. Kisha akamwambia, “Kwa nini unawasikiliza watu wanaokuambia, ‘Angalia! Daudi anataka kukudhuru?’ Sasa tazama, leo umejionea kwa macho yako mwenyewe; ulipokuwa pangoni Mwenyezi-Mungu alikutia mikononi mwangu. Baadhi ya watu wangu waliniambia nikuue, lakini nilikuhurumia. Nikasema sitanyosha mkono wangu dhidi ya bwana wangu kwani yeye ameteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta. Tazama, baba yangu, angalia pindo hili la vazi lako mikononi mwangu; kwa kulikata pindo la vazi lako bila kukuua, unaweza sasa kujua kwa hakika kwamba mimi si mwovu wala mhaini. Mimi sijatenda dhambi dhidi yako ingawa wewe unaniwinda uniue.

1 Samueli 24:2-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu. Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kwenda haja. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia BWANA, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yoyote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri. Lakini baadaye, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA, neno hili, kuunyosha mkono wangu juu yake, kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo, asiwaruhusu kumshambulia Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake. Daudi naye akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita Sauli, akisema, Bwana wangu, mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama uso wake hadi chini, akamsujudia. Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru? Tazama, leo hivi macho yako yameona jinsi BWANA alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata.

1 Samueli 24:2-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi Sauli akachukua watu hodari 3,000 kutoka Israeli yote kwenda kumsaka Daudi na watu wake karibu na Majabali ya Mbuzi-Mwitu. Akaja mpaka kwenye mazizi ya kondoo kando ya njia, hapo palikuwa na pango, na Sauli akaingia ndani kujipumzisha. Daudi na watu wake walikuwa wamo mle pangoni kwa ndani zaidi. Watu wa Daudi wakasema, “Hii ndiyo siku aliyonena BWANA akikuambia, ‘Nitamtia adui yako mikononi mwako ili wewe umtendee utakavyo.’ ” Basi Daudi akanyemelea bila kuonekana na kukata upindo wa joho la Sauli. Baada ya hilo, dhamiri ya Daudi ikataabika kwa kukata upindo wa joho la Sauli. Akawaambia watu wake, “BWANA na apishie mbali nisije nikafanya jambo kama hilo kwa bwana wangu, yeye ambaye ni mpakwa mafuta wa BWANA, au kuinua mkono wangu dhidi yake; kwani yeye ni mpakwa mafuta wa BWANA.” Kwa maneno haya Daudi akawaonya watu wake na hakuwaruhusu wamshambulie Sauli. Naye Sauli akaondoka pangoni na kwenda zake. Ndipo Daudi naye akatoka pangoni na kumwita Sauli akisema, “Mfalme, bwana wangu!” Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama na kusujudu uso wake mpaka nchi. Akamwambia Sauli, “Kwa nini unasikiliza wakati watu wanapokuambia, ‘Daudi amenuia kukudhuru’? Leo umeona kwa macho yako mwenyewe jinsi BWANA alivyokutia mikononi mwangu huko pangoni. Watu wengine walisisitiza nikuue, lakini nilikuacha, nikisema, ‘Sitainua mkono wangu dhidi ya bwana wangu, kwa sababu yeye ni mpakwa mafuta wa BWANA.’ Tazama, baba yangu, ona kipande hiki cha joho lako mkononi mwangu! Nilikata upindo wa joho lako lakini sikukuua. Basi ujue na kutambua kuwa sina hatia ya kutenda mabaya wala ya kuasi. Wewe sijakukosea, lakini wewe unaniwinda mimi ili kuuondoa uhai wangu.

1 Samueli 24:2-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu. Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia BWANA, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yo yote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri. Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA, neno hili, kuunyosha mkono wangu juu yake, kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo, asiwaache kumwondokea Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake. Daudi naye akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita Sauli, akisema, Bwana wangu, mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama uso wake hata nchi, akamsujudia. Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru? Tazama, leo hivi macho yako yameona jinsi BWANA alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata.