Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 24:1-22

1 Samueli 24:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Shauli aliporudi kutoka kupigana na Wafilisti, aliambiwa kuwa Daudi yuko kwenye mbuga za Engedi. Kisha Shauli aliwachukua askari 3,000 wateule waliokuwa bora zaidi katika nchi yote ya Israeli, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake katika Miamba ya Mbuzimwitu. Shauli alipokuwa anasafiri, alifika kwenye pango moja lililokuwa karibu na zizi la kondoo, akaingia humo pangoni ili kujisaidia. Daudi na watu wake walikuwa wameketi ndani kabisa ya pango hilo. Watu wa Daudi wakamwambia, “Ile siku aliyokuambia Mwenyezi-Mungu kuwa atakuja kumtia adui yako mikononi mwako nawe umtendee utakavyoona inafaa, leo imefika.” Ndipo Daudi alipomwendea Shauli polepole kutoka nyuma, akakata pindo la vazi lake. Daudi akaanza kufadhaika moyoni kwa sababu alikata pindo la vazi la Shauli kwa siri. Akawaambia watu wake, “Mwenyezi-Mungu anizuie nisimtendee kitendo kama hiki bwana wangu aliyepakwa mafuta na Mwenyezi-Mungu. Nisiunyoshe mkono wangu dhidi ya mtu ambaye Mwenyezi-Mungu amempaka mafuta.” Kwa maneno hayo, Daudi akawashawishi watu wake wasimdhuru Shauli; aliwakataza wasimshambulie. Kisha Shauli akasimama, akatoka pangoni akaendelea na safari yake. Baadaye, Daudi naye akainuka, akatoka pangoni na kumwita Shauli, “Bwana wangu mfalme!” Mfalme Shauli alipoangalia nyuma, Daudi aliinama hadi chini, akamsujudia Shauli. Kisha akamwambia, “Kwa nini unawasikiliza watu wanaokuambia, ‘Angalia! Daudi anataka kukudhuru?’ Sasa tazama, leo umejionea kwa macho yako mwenyewe; ulipokuwa pangoni Mwenyezi-Mungu alikutia mikononi mwangu. Baadhi ya watu wangu waliniambia nikuue, lakini nilikuhurumia. Nikasema sitanyosha mkono wangu dhidi ya bwana wangu kwani yeye ameteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta. Tazama, baba yangu, angalia pindo hili la vazi lako mikononi mwangu; kwa kulikata pindo la vazi lako bila kukuua, unaweza sasa kujua kwa hakika kwamba mimi si mwovu wala mhaini. Mimi sijatenda dhambi dhidi yako ingawa wewe unaniwinda uniue. Mwenyezi-Mungu na aamue kati yangu, na wewe. Yeye akulipize kisasi lakini mimi kamwe sitanyosha mkono wangu dhidi yako. Kumbuka methali ya kale isemayo, ‘Kwa muovu hutoka uovu’; lakini sitanyosha mkono dhidi yako. Sasa wewe mfalme wa Israeli angalia mtu unayetaka kumwua! Je, unamfuatilia nani? Unamfuatilia mbwa mfu! Unakifuatilia kiroboto! Basi, Mwenyezi-Mungu na awe mwamuzi kati yangu na wewe. Yeye na aliangalie jambo hili, anitetee na kuniokoa mikononi mwako.” Daudi alipomaliza kusema, Shauli akasema, “Je, hiyo ni sauti yako mwanangu Daudi?” Shauli akalia kwa sauti. Kisha akamwambia Daudi, “Wewe una haki kuliko mimi; umenilipa mema, hali mimi nimekulipa maovu. Leo, umeonesha jinsi ulivyo mwema kwangu. Hukuniua ijapokuwa Mwenyezi-Mungu alinitia mikononi mwako. Je, mtu akimkamata adui yake atamwacha aende salama? Kwa lile ulilonitendea, Mwenyezi-Mungu na akupe tuzo jema! Sasa nimejua ya kwamba hakika utakuwa mfalme wa Israeli, na ufalme wa Israeli utaimarishwa chini yako. Lakini niapie kwa jina la Mwenyezi-Mungu kuwa hutawakatilia mbali wazawa wangu, wala kufutilia mbali jina langu katika jamaa ya baba yangu.” Daudi akamwapia Shauli. Kisha Shauli akarudi nyumbani kwake, lakini Daudi na watu wake wakaenda kwenye ngome.

1 Samueli 24:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa, Sauli aliporudi baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu. Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kwenda haja. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia BWANA, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yoyote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri. Lakini baadaye, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA, neno hili, kuunyosha mkono wangu juu yake, kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo, asiwaruhusu kumshambulia Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake. Daudi naye akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita Sauli, akisema, Bwana wangu, mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama uso wake hadi chini, akamsujudia. Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru? Tazama, leo hivi macho yako yameona jinsi BWANA alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata. BWANA atuamue, mimi na wewe, na BWANA anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa juu yako. Kama vile walivyosema watu wa kale katika mithali yao, Katika waovu hutoka uovu; ila mkono wangu hautakuwa juu yako. Na mfalme wa Israeli ametoka ili kumfuatia nani? Unamwinda nani? Ni kuwinda mbwa mfu, au kiroboto. Basi BWANA atuamue, akatuhukumu mimi na wewe, akaone, akanitetee neno langu, akaniokoe kutokana na mkono wako. Ikawa, Daudi alipokwisha kumwambia Sauli maneno hayo Sauli alisema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Naye Sauli akapaza sauti yake, akalia. Akamwambia Daudi, Wewe u mwenye haki kuliko mimi; maana wewe umenitendea mema, nami nimekutenda mabaya. Nawe umeonesha leo jinsi ulivyonitendea mema, kwani BWANA aliponitia mikononi mwako, hukuniua. Maana mtu akimwona adui yake, je! Atamwacha aende zake salama? Basi BWANA na akulipe mema kwa haya uliyonitendea leo. Na sasa, angalia, ninajua ya kuwa hakika utakuwa mfalme, na ufalme wa Israeli utafanyika imara mkononi mwako. Basi sasa, uniapie kwa BWANA, ya kwamba hutawakatilia mbali wazao wangu baada yangu, wala hutaliharibu jina langu katika ukoo wa baba yangu. Naye Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akaenda zake kwao; lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.

1 Samueli 24:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa, Sauli aliporudi baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu. Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia BWANA, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yo yote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri. Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA, neno hili, kuunyosha mkono wangu juu yake, kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo, asiwaache kumwondokea Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake. Daudi naye akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita Sauli, akisema, Bwana wangu, mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama uso wake hata nchi, akamsujudia. Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru? Tazama, leo hivi macho yako yameona jinsi BWANA alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata. BWANA atuamue, mimi na wewe, na BWANA anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa juu yako. Kama vile walivyosema watu wa kale katika mithali yao, Katika waovu hutoka uovu; ila mkono wangu hautakuwa juu yako. Na mfalme wa Israeli ametoka ili kumfuatia nani? Unamwinda nani? Ni kuwinda mbwa mfu, au kiroboto. Basi BWANA atuamue, akatuhukumu mimi na wewe, akaone, akanitetee neno langu, akaniokoe na mkono wako. Ikawa, Daudi alipokwisha kumwambia Sauli maneno hayo Sauli alisema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Naye Sauli akapaza sauti yake, akalia. Akamwambia Daudi, Wewe u mwenye haki kuliko mimi; maana wewe umenitendea mema, nami nimekutenda mabaya. Nawe umeonyesha leo jinsi ulivyonitendea mema, kwani BWANA aliponitia mikononi mwako, hukuniua. Maana mtu akimwona adui yake, je! Atamwacha aende zake salama? Basi BWANA na akulipe mema kwa haya uliyonitendea leo. Na sasa, angalia, najua ya kuwa hakika utakuwa mfalme, na ufalme wa Israeli utafanyika imara mkononi mwako. Basi sasa, uniapie kwa BWANA, ya kwamba hutawakatilia mbali wazao wangu baada yangu, wala hutaliharibu jina langu katika mbari ya baba yangu. Naye Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akaenda zake kwao; lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.

1 Samueli 24:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya Sauli kurudi kuwafuatia Wafilisti, akaambiwa kwamba, “Daudi yuko katika Jangwa la En-Gedi.” Basi Sauli akachukua watu hodari 3,000 kutoka Israeli yote kwenda kumsaka Daudi na watu wake karibu na Majabali ya Mbuzi-Mwitu. Akaja mpaka kwenye mazizi ya kondoo kando ya njia, hapo palikuwa na pango, na Sauli akaingia ndani kujipumzisha. Daudi na watu wake walikuwa wamo mle pangoni kwa ndani zaidi. Watu wa Daudi wakasema, “Hii ndiyo siku aliyonena BWANA akikuambia, ‘Nitamtia adui yako mikononi mwako ili wewe umtendee utakavyo.’ ” Basi Daudi akanyemelea bila kuonekana na kukata upindo wa joho la Sauli. Baada ya hilo, dhamiri ya Daudi ikataabika kwa kukata upindo wa joho la Sauli. Akawaambia watu wake, “BWANA na apishie mbali nisije nikafanya jambo kama hilo kwa bwana wangu, yeye ambaye ni mpakwa mafuta wa BWANA, au kuinua mkono wangu dhidi yake; kwani yeye ni mpakwa mafuta wa BWANA.” Kwa maneno haya Daudi akawaonya watu wake na hakuwaruhusu wamshambulie Sauli. Naye Sauli akaondoka pangoni na kwenda zake. Ndipo Daudi naye akatoka pangoni na kumwita Sauli akisema, “Mfalme, bwana wangu!” Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama na kusujudu uso wake mpaka nchi. Akamwambia Sauli, “Kwa nini unasikiliza wakati watu wanapokuambia, ‘Daudi amenuia kukudhuru’? Leo umeona kwa macho yako mwenyewe jinsi BWANA alivyokutia mikononi mwangu huko pangoni. Watu wengine walisisitiza nikuue, lakini nilikuacha, nikisema, ‘Sitainua mkono wangu dhidi ya bwana wangu, kwa sababu yeye ni mpakwa mafuta wa BWANA.’ Tazama, baba yangu, ona kipande hiki cha joho lako mkononi mwangu! Nilikata upindo wa joho lako lakini sikukuua. Basi ujue na kutambua kuwa sina hatia ya kutenda mabaya wala ya kuasi. Wewe sijakukosea, lakini wewe unaniwinda mimi ili kuuondoa uhai wangu. BWANA na ahukumu kati yangu na wewe. Naye BWANA alipize mabaya unayonitendea, lakini mkono wangu hautakugusa. Kama msemo wa kale usemavyo, ‘Kutoka kwa watenda maovu hutoka matendo maovu,’ kwa hiyo mkono wangu hautakugusa wewe. “Je, mfalme wa Israeli ametoka dhidi ya nani? Ni nani unayemfuatia? Je, ni mbwa mfu? Ni kiroboto? BWANA na awe mwamuzi wetu, yeye na aamue kati yetu. Yeye na anitetee shauri langu; anihesabie haki kwa kuniokoa mkononi mwako.” Daudi alipomaliza kusema haya, Sauli akamuuliza, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Ndipo Sauli akalia kwa sauti kuu, akisema, “Wewe ni mwenye haki kuliko mimi; umenitendea mema, lakini mimi nimekutendea mabaya. Sasa umeniambia juu ya mema uliyonitendea. BWANA alinitia mikononi mwako, lakini wewe hukuniua. Je, mtu ampatapo adui yake, humwacha aende zake bila kumdhuru? BWANA na akulipe mema kwa jinsi ulivyonitenda leo. Ninajua kwamba hakika utakuwa mfalme na ya kwamba ufalme wa Israeli utakuwa imara mikononi mwako. Sasa niapie kwa BWANA kwamba hutakatilia mbali uzao wangu wala kulifuta jina langu kutoka jamaa ya baba yangu.” Basi Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akarudi zake nyumbani, lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.