Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 22:1-23

1 Samueli 22:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Daudi aliondoka huko akakimbilia kwenye pango karibu na mji wa Adulamu. Kaka zake na ndugu zake wengine waliposikia kwamba alikuwa hapo, wote walikwenda kuungana naye. Watu wote waliokandamizwa au waliokuwa na madeni, au wale ambao hawakuridhika walijumuika na Daudi. Jumla yao ilikuwa watu kama 400, naye akawa kiongozi wao. Kutoka huko, Daudi alikwenda mpaka huko Mizpa nchini Moabu. Akamwambia mfalme wa Moabu, “Nakuomba, baba yangu na mama yangu wakae hapa kwako mpaka nijue Mungu atanifanyia nini.” Basi, Daudi aliwaacha wazazi wake wakae na mfalme wa Moabu; nao wakakaa kwake muda wote ambao Daudi alikuwa ngomeni. Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae hapa ngomeni, ondoka mara moja uende katika nchi ya Yuda.” Basi, Daudi akaondoka, akaenda kwenye msitu wa Herethi. Siku moja, Shauli alikuwa Gibea, amekaa chini ya mkwaju, mlimani, huku akiwa na mkuki wake mkononi na watumishi wake walikuwa wamesimama kandokando yake. Basi akaambiwa kwamba Daudi na watu wake wameonekana. Naye Shauli akawaambia watumishi wake, “Sasa nyinyi watu wa kabila la Benyamini nisikilizeni, je, mnadhani huyu Daudi mwana wa Yese atampa kila mmoja wenu mashamba na mashamba ya mizabibu? Au je, mnadhani atamfamya kila mmoja wenu kamanda wa maelfu au kamanda wa mamia ya majeshi? Kwa nini nyinyi nyote mmekula njama dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu anayeniambia habari hii, wakati mwanangu afanyapo mapatano na mtoto wa Yese. Tena, kwa nini hakuna hata mmoja kati yenu anayesikitika au kunieleza kuwa mwanangu mwenyewe anamchochea mtumishi wangu dhidi yangu akinivizia kama ilivyo leo hii?” Ndipo Doegi, Mwedomu, ambaye alikuwa amesimama karibu na watumishi wa Shauli akasema, “Nilimwona mwana wa Yese akija Nobu kwa kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu. Ahimeleki alimwombea Daudi kwa Mwenyezi-Mungu, akampa chakula na upanga wa yule Mfilisti Goliathi.” Mfalme Shauli akaagiza kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu, pamoja na watu wote wa jamaa ya baba yake ambao walikuwa makuhani huko Nobu waitwe. Wote wakamwendea mfalme Shauli. Shauli akasema, “Sasa sikiliza wewe mwana wa Ahitubu.” Ahimeleki akamjibu, “Naam, bwana.” Shauli akamwambia, “Kwa nini wewe na Daudi mwana wa Yese, mmekula njama dhidi yangu? Kwa nini ulimpatia mikate na upanga, halafu ukamwombea kwa Mungu? Kwa sababu hiyo, leo ameniasi na ananivizia.” Ahimeleki akamjibu, “Kati ya watumishi wako, Daudi ndiye ofisa wa kuaminika kuliko wote. Yeye ni mkwe wako wewe mfalme mwenyewe, kapteni wa kikosi chako cha ulinzi na anaheshimika kuliko wote nyumbani mwako. Leo, sio mara ya kwanza kumwomba Mungu shauri kwa ajili yake. Mfalme, usinishuku mimi wala mtu yeyote katika jamaa ya baba yangu juu ya njama hizo. Mimi mtumishi wako, sijui lolote, liwe kubwa au dogo juu ya jambo hilo.” Lakini mfalme Shauli akamwambia, “Ahimeleki, hakika utauawa, wewe na jamaa yote ya baba yako.” Shauli akawaambia walinzi waliokuwa wamesimama kandokando yake, “Geukeni na kuwaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu, maana wao wanapatana na Daudi; walijua kuwa ametukimbia wala hawakuniarifu.” Lakini walinzi hao hawakuinua mikono yao ili kuwaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu. Kwa hiyo, mfalme Shauli akamwambia Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Doegi, Mwedomu, akaenda na kuwaua makuhani wote. Siku hiyo, Doegi aliua makuhani themanini na watano ambao huvaa vizibao vya kikuhani vya kitani. Kisha aliwaua kwa makali ya upanga wakazi wote wa Nobu, mji wa makuhani, wanaume na wanawake, watoto wadogo na wanyonyao, ng'ombe, punda na kondoo. Lakini Abiathari, mmoja wa watoto wa kiume wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, aliponyoka akakimbilia kwa Daudi. Abiathari alimweleza Daudi kuwa Shauli amewaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu. Naye Daudi akamwambia Abiathari, “Nilijua wazi siku ile nilipomwona Doegi Mwedomu, kuwa atamwambia Shauli. Hivyo, mimi nimesababisha vifo vya watu wa jamaa ya baba yako. Wewe, kaa pamoja nami, wala usiogope. Maana, anayetafuta kuyaangamiza maisha yangu anatafuta hata yako pia. Ukiwa pamoja nami, uko salama kabisa.”

1 Samueli 22:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa ukoo wa baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walikuwa kama watu mia nne. Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali wakubalie baba yangu na mama yangu watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu. Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni. Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, Usikae hapa ngomeni; ondoka, ukaende mpaka nchi ya Yuda. Ndipo Daudi akaondoka, akaenda zake, akakaa katika msitu wa Herethi. Kisha Sauli akasikia ya kwamba Daudi ameonekana, na wale watu waliokuwa pamoja naye. Basi Sauli alikuwa akikaa Gibea, chini ya mkwaju katika mahali palipoinuka, naye alikuwa na mkuki wake mkononi, na watumishi wake wote wakimzunguka. Naye Sauli akawaambia watumishi wake waliomzunguka, Sikieni sasa, enyi Wabenyamini; je! Huyu mwana wa Yese atawapa ninyi kila mmoja mashamba, na mashamba ya mizabibu, atawafanya kuwa wakuu wa watu maelfu, na wakuu wa watu mamia; hata ninyi nyote mkanifitinia, wala hapana mtu anifunuliaye habari hii mwanangu afanyapo agano na mwana wa Yese, wala hapana mmoja wenu anayenisikitikia, wala kunifunulia ya kuwa mwanangu amemchochea mtumishi wangu, anivizie kama hivi leo? Ndipo akajibu Doegi, Mwedomi, aliyesimama karibu na watumishi wa Sauli, akasema, Mimi nilimwona mwana wa Yese akienda Nobu, kwa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu. Naye akamwuliza BWANA kwa ajili yake, akampa vyakula, akampa na ule upanga wa Goliathi, Mfilisti. Ndipo mfalme akatuma watu waende kumwita Ahimeleki, kuhani, mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, hao makuhani, waliokuwako huko Nobu; nao wakaenda kwa mfalme wote pia. Sauli akasema, Sikia sasa, Ewe mwana wa Ahitubu. Naye akaitika, Mimi hapa, bwana wangu. Sauli akamwuliza, Mbona mmefanya fitina juu yangu, wewe na mwana wa Yese? Kwa maana umempa mikate, na upanga, nawe umemwuliza Mungu kwa ajili yake, ili aniasi na kunivizia kama hivi leo? Basi Ahimeleki akamjibu mfalme, akasema, Katika watumishi wako wote ni nani aliye mwaminifu kama Daudi, aliye mkwewe mfalme, tena msiri wako, mwenye heshima nyumbani mwako? Je! Mimi nimeanza leo tu kumwuliza Mungu kwa ajili yake? Hasha! Mfalme asinidhanie mimi, mtumishi wake neno hili, Wala jamaa yote ya baba yangu, kwa maana mimi, mtumishi wako siyajui hayo yote, yaliyopungua au yaliyozidi. Naye mfalme akasema, Kufa utakufa, Ahimeleki, wewe na jamaa yote ya baba yako. Kisha mfalme akawaambia askari walinzi waliosimama karibu naye Geukeni, mkawaue hao makuhani wa BWANA, kwa sababu mkono wao u pamoja na Daudi, na kwa sababu walijua ya kuwa amekimbia, wasiniarifu. Lakini watumishi wa mfalme walikataa kunyosha mkono na kuwaangukia makuhani wa BWANA. Basi mfalme akamwambia Doegi, Geuka wewe, uwaangukie hao makuhani. Basi Doegi, Mwedomi, akageuka, akawaangukia makuhani, akaua siku ile watu themanini na watano wenye kuvaa naivera ya kitani. Kisha akaupiga Nobu, mji wa makuhani, kwa makali ya upanga, wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, na ng'ombe, na punda, na kondoo. Na katika wana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akaokoka mtu mmoja tu, aliyeitwa Abiathari, akamkimbilia Daudi. Naye Abiathari akamweleza Daudi ya kwamba Sauli amewaua makuhani wa BWANA. Daudi akamwambia Abiathari, Siku ile alipokuwako Doegi, Mwedomi, nilijua hakika ya kuwa atamwambia Sauli; mimi nimewapatia watu wote wa jamaa ya baba yako kifo. Kaa wewe pamoja nami, usiogope; kwa maana yeye atafutaye roho yangu, ndiye atafutaye na roho yako; nawe utakaa kwangu salama.

1 Samueli 22:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne. Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali ukubali baba yangu na mama yangu watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu. Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni. Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, Usikae hapa ngomeni; ondoka, ukaende mpaka nchi ya Yuda. Ndipo Daudi akaondoka, akaenda zake, akakaa katika msitu wa Herethi. Kisha Sauli akasikia ya kwamba Daudi ameonekana, na wale watu waliokuwa pamoja naye. Basi Sauli alikuwa akikaa Gibea, chini ya mkwaju katika mahali palipoinuka, naye alikuwa na mkuki wake mkononi, na watumishi wake wote wakimzunguka. Naye Sauli akawaambia watumishi wake waliomzunguka, Sikieni sasa, enyi Wabenyamini; je! Huyu mwana wa Yese atawapa ninyi kila mmoja mashamba, na mashamba ya mizabibu, atawafanya kuwa maakida wa watu elfu, na maakida wa watu mia; hata ninyi nyote mkafanya fitina juu yangu, wala hapana mtu anifunuliaye habari hii mwanangu afanyapo agano na mwana wa Yese, wala hapana mmoja wenu anayenisikitikia, wala kunifunulia ya kuwa mwanangu amemwondokesha mtumishi wangu juu yangu, anivizie kama hivi leo? Ndipo akajibu Doegi, Mwedomi, aliyesimama karibu na watumishi wa Sauli, akasema, Mimi nalimwona mwana wa Yese akienda Nobu, kwa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu. Naye akamwuliza BWANA kwa ajili yake, akampa vyakula, akampa na ule upanga wa Goliathi, Mfilisti. Ndipo mfalme akatuma watu waende kumwita Ahimeleki, kuhani, mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, hao makuhani, waliokuwako huko Nobu; nao wakaenda kwa mfalme wote pia. Sauli akasema, Sikia sasa, Ewe mwana wa Ahitubu. Naye akaitika, Mimi hapa, bwana wangu. Sauli akamwuliza, Mbona mmefanya fitina juu yangu, wewe na mwana wa Yese? Kwa maana umempa mikate, na upanga, nawe umemwuliza Mungu kwa ajili yake, ili aniondokee na kunivizia kama hivi leo? Basi Ahimeleki akamjibu mfalme, akasema, Katika watumishi wako wote ni nani aliye mwaminifu kama Daudi, aliye mkwewe mfalme, tena msiri wako, mwenye heshima nyumbani mwako? Je! Mimi nimeanza leo tu kumwuliza Mungu kwa ajili yake? Hasha! Mfalme asinidhanie mimi, mtumishi wake neno hili, Wala jamaa yote ya baba yangu, kwa maana mimi, mtumishi wako siyajui hayo yote, yaliyopungua au yaliyozidi. Naye mfalme akasema, Kufa utakufa, Ahimeleki, wewe na jamaa yote ya baba yako. Kisha mfalme akawaambia askari walinzi waliosimama karibu naye Geukeni, mkawaue hao makuhani wa BWANA, kwa sababu mkono wao u pamoja na Daudi, na kwa sababu walijua ya kuwa amekimbia, wasiniarifu. Lakini watumishi wa mfalme walikataa kunyosha mkono na kuwaangukia makuhani wa BWANA. Basi mfalme akamwambia Doegi, Geuka wewe, ukawaangukia hao makuhani. Basi Doegi, Mwedomi, akageuka, akawaangukia makuhani, akaua siku ile watu themanini na watano wenye kuvaa naivera ya kitani. Kisha akaupiga Nobu, mji wa makuhani, kwa makali ya upanga, wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, na ng’ombe, na punda, na kondoo. Na katika wana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akaokoka mtu mmoja tu, aliyeitwa jina lake Abiathari, akamkimbilia Daudi. Naye Abiathari akamweleza Daudi ya kwamba Sauli amewaua makuhani wa BWANA. Daudi akamwambia Abiathari, Siku ile alipokuwako Doegi, Mwedomi, nalijua yakini ya kuwa atamwambia Sauli; mimi nimewapatia watu wote wa jamaa ya baba yako kifo. Kaa wewe pamoja nami, usiogope; kwa maana yeye atafutaye roho yangu, ndiye atafutaye na roho yako; nawe utakaa kwangu salama.

1 Samueli 22:1-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Daudi akaondoka Gathi na kukimbilia kwenye pango la Adulamu. Ndugu zake na watu wa nyumba ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Wale wote waliokuwa katika dhiki au waliokuwa na madeni au wale ambao hawakuridhika wakamkusanyikia Daudi, naye akawa kiongozi wao. Watu wapatao 400 walikuwa pamoja naye. Kutoka huko Daudi akaenda Mispa huko Moabu na kumwambia mfalme wa Moabu, “Naomba uwaruhusu baba yangu na mama yangu waje kukaa nawe mpaka nijue nini Mungu atakachonifanyia.” Hivyo akawaacha wazazi wake wakae na mfalme wa Moabu, nao wakakaa naye muda wote ambao Daudi alikuwa ngomeni. Ndipo nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae ngomeni. Nenda katika nchi ya Yuda.” Hivyo Daudi akaondoka na kwenda katika msitu wa Herethi. Basi Sauli akasikia kwamba Daudi na watu wake wameonekana. Sauli akiwa na mkuki mkononi, alikuwa ameketi chini ya mti wa mkwaju kwenye kilima huko Gibea, maafisa wake wote wakiwa wamesimama kumzunguka. Sauli akawaambia, “Sikilizeni enyi watu wa Benyamini! Je, mwana wa Yese atawapa ninyi nyote mashamba na mashamba ya mizabibu? Je, atawafanya ninyi nyote majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia? Je, ndiyo sababu ninyi mkapanga hila mbaya dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu ambaye ameniambia ni lini mwanangu alifanya agano na mwana wa Yese. Hapana hata mmoja wenu anayejishughulisha nami wala anayeniambia kwamba mwanangu amechochea mtumishi wangu kunivizia, kama afanyavyo leo.” Lakini Doegi Mwedomu, ambaye alikuwa akisimama na maafisa wa Sauli, akasema, “Nilimwona mwana wa Yese akija kwa Ahimeleki mwana wa Ahitubu huko Nobu. Ahimeleki akamuuliza BWANA kwa ajili yake; pia akampa vyakula na ule upanga wa Goliathi Mfilisti.” Kisha mfalme akatuma watu wamwite kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, waliokuwa makuhani huko Nobu, nao wote wakaja kwa mfalme. Sauli akasema, “Sikiliza sasa, mwana wa Ahitubu.” Akajibu, “Naam, bwana wangu.” Sauli akamwambia, “Kwa nini umepanga shauri baya dhidi yangu, wewe na mwana wa Yese, ukampa vyakula na upanga, tena hukumuuliza Mungu kwa ajili yake, na kwa sababu hiyo ameasi dhidi yangu na kunivizia, kama afanyavyo leo?” Ahimeleki akamjibu mfalme, “Ni nani miongoni mwa watumishi wako wote aliye mwaminifu kama Daudi, mkwewe mfalme, kiongozi wa walinzi wako na anayeheshimika sana katika watu wa nyumbani mwako? Je, siku hiyo ilikuwa ndiyo ya kwanza kumwomba Mungu kwa ajili yake? La hasha! Mfalme na usiwashutumu watumishi wako wala yeyote wa jamaa ya baba yake, kwa kuwa mtumishi wako hafahamu lolote kabisa kuhusu jambo hili lote.” Lakini mfalme akasema, “Ahimeleki, hakika utakufa, wewe na jamaa yote ya baba yako.” Ndipo mfalme akawaamuru walinzi wake waliokuwa kando yake: “Geukeni na kuwaua makuhani wa BWANA, kwa sababu nao pia wamejiunga na Daudi. Walijua kuwa alikuwa anakimbia, wala hawakuniambia.” Lakini maafisa wa mfalme hawakuwa radhi kuinua mkono kuwaua makuhani wa BWANA. Kisha mfalme akamwagiza Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Hivyo basi Doegi Mwedomu, akageuka na kuwaua. Siku ile aliwaua watu themanini na watano wavaao visibau vya kitani. Pia akaupiga Nobu kwa upanga, mji wa makuhani, wakiwemo wanaume na wanawake, watoto wadogo na wale wanyonyao, ngʼombe wake, punda na kondoo. Lakini Abiathari, mwana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akatoroka, akakimbia na kujiunga na Daudi. Akamwambia Daudi kuwa Sauli amewaua makuhani wa BWANA. Kisha Daudi akamwambia Abiathari: “Siku ile, wakati Doegi Mwedomu alipokuwa pale, nilijua atahakikisha amemwambia Sauli. Mimi ninawajibika kwa vifo vya jamaa ya baba yako yote. Kaa pamoja nami; usiogope. Mtu anayeutafuta uhai wako anautafuta uhai wangu pia. Ukiwa pamoja nami utakuwa salama.”