1 Samueli 21:1-15
1 Samueli 21:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Daudi alikwenda kwa kuhani Ahimeleki huko Nobu. Ahimeleki akatoka kumlaki huku akiwa anatetemeka, akamwuliza, “Kwa nini umekuja hapa peke yako?” Daudi akamjibu, “Niko hapa kutokana na amri ya mfalme. Aliniambia nisimweleze mtu yeyote juu ya kile ambacho amenituma. Nimeagana na watu wangu kwamba tukutane mahali fulani. Je, una kitu chochote? Nakuomba mikate mitano au chochote kilichoko.” Kuhani Ahimeleki akamwambia, “Hapa sina mkate wa kawaida. Ninayo tu ile mikate mitakatifu. Mnaweza kupewa mikate hiyo ikiwa watu wako hawajalala na wanawake hivi karibuni.” Daudi akamwambia, “Kwa hakika, daima ninapokwenda kwa ajili ya shughuli maalumu, wanawake wamekuwa mbali nasi! Ikiwa miili ya vijana wangu ni mitakatifu tuwapo kwenye shughuli za kawaida, je, si zaidi katika shughuli hii maalumu?” Hivyo kuhani Ahimeleki akampa mikate mitakatifu, kwani hapakuwa na mikate mingine isipokuwa hiyo ya kuwekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu, ikabadilishwa na mikate mipya kutoka mekoni. Basi kulikuwa hapo siku hiyo mtumishi mmoja wa Shauli ambaye alikuwa amezuiliwa mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mtumishi huyo aliitwa Doegi, Mwedomu, msimamizi wa wachungaji wa Shauli. Basi, Daudi akamwambia Ahimeleki, “Je, una upanga au mkuki ambao unaweza kunipatia? Kwa kuwa shughuli za mfalme zilinilazimu niondoke haraka, nami niliondoka bila upanga wangu wala silaha nyingine yoyote.” Ahimeleki akamjibu, “Ninao ule upanga wa Mfilisti Goliathi uliyemuua kwenye bonde la Ela; uko nyuma ya kizibao cha kuhani umefungwa katika kitambaa. Ikiwa unataka kuuchukua huo basi, uchukue kwani hakuna upanga mwingine hapa.” Daudi akamwambia, “Hakuna upanga mwingine kama huo; nakuomba unipe.” Siku hiyo, Daudi alimkimbia Shauli, akaenda kwa mfalme Akishi wa Gathi. Watumishi wa mfalme wakamwambia Akishi, “Huyu si Daudi, mfalme wa nchi ya Israeli? Je, si huyu ambaye walikuwa wakiimbiana juu yake katika ngoma, wakisema, ‘Shauli ameua maelfu yake na Daudi ameua makumi elfu yake?’” Maneno hayo Daudi hakuweza kuyasahau, akaanza kumwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi. Hivyo, akabadilisha tabia yake, akijifanya mwendawazimu, akawa anakwaruzakwaruza kwenye malango ya mji, na mate yake akayaacha yatiririke kwenye ndevu zake. Akishi akawaambia watumishi wake, “Mnajua kuwa mtu huyu ni mwendawazimu; kwa nini mmemleta kwangu? Je, nawahitaji wendawazimu zaidi? Kwa nini mnaniletea mwendawazimu aje kunisumbua na vitendo vya wendawazimu? Je, mtu huyu ataingia nyumbani kwangu?”
1 Samueli 21:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Daudi akaenda Nobu kwa Ahimeleki, kuhani. Ahimeleki akaenda kumlaki Daudi, akitetemeka, akamwambia, Kwa nini uko peke yako, wala hapana mtu pamoja nawe? Daudi akamwambia Ahimeleki, kuhani, Mfalme ameniagiza shughuli, akaniambia, Asijue mtu awaye yote habari ya shughuli hii ninayokutuma, wala ya neno hili ninalokuamuru; nami nimewaagiza vijana waende mahali fulani. Kuna nini basi, chini ya mkono wako? Nipe mkononi mwangu mikate mitano, au chochote ulicho nacho hapa. Yule kuhani akamjibu Daudi, akasema, Hapana mikate ya kawaida chini ya mkono wangu, ila mikate mitakatifu; ikiwa wale vijana wamejitenga na wanawake. Naye Daudi akamjibu kuhani, akamwambia, Hakika tumejitenga na wanawake siku hizi tatu; napo nilipotoka, vyombo vya vijana hawa vilikuwa vitakatifu, ingawa ilikuwa safari ya kawaida; basi leo je! Vyombo vyetu havitakuwa vitakatifu zaidi? Ndipo kuhani akampa ile mikate mitakatifu; kwa maana hapakuwa na mikate ila ile ya wonyesho, nayo imekwisha kuondolewa mbele za BWANA, ili itiwe mikate ya moto siku ile ilipoondolewa. Basi siku ile palikuwapo na mtu mmoja wa watumishi wa Sauli, amezuiwa hapo mbele za BWANA jina lake akiitwa Doegi, Mwedomi, mkubwa wa wachungaji wa Sauli. Tena Daudi akamwambia Ahimeleki, Na hapa chini ya mkono wako, je! Hapana mkuki, au upanga? Kwa maana sikuleta upanga, wala silaha zangu, kwa sababu ile shughuli ya mfalme ilitaka haraka. Yule kuhani akasema, Upanga wa Goliathi, yule Mfilisti, uliyemwua katika bonde la Ela, tazama, upo hapa, umefungwa ndani ya nguo nyuma ya naivera; ukipenda kuuchukua, haya! Uchukue, maana hapa hapana mwingine ila huo tu. Daudi akasema, Hapana mwingine kama ule; haya! Nipe. Basi Daudi akaondoka, akakimbia siku ile, kwa hofu ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi. Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, Je! Huyu siye yule Daudi, mfalme wa nchi? Je! Hawakuimbiana habari zake katika ngoma zao, kusema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Naye Daudi akayatia maneno hayo moyoni mwake, akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi. Akaubadilisha mwenendo wake mbele yao, akajifanya mwenye wazimu mikononi mwao, akakunakuna katika mbao za mlango, na kuyaacha mate yake kuanguka juu ya ndevu zake. Ndipo huyo Akishi akawaambia watumishi wake, Angalieni, mnaona ya kuwa mtu huyu ana wazimu; basi, maana yake nini kumleta kwangu? Je! Mimi nina haja ya watu wenye wazimu, hata mmemleta kiumbe huyu ili aoneshe wazimu wake machoni pangu? Je! Huyu ataingia nyumbani mwangu?
1 Samueli 21:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Daudi akaenda Nobu kwa Ahimeleki, kuhani. Ahimeleki akaenda kumlaki Daudi, akitetemeka, akamwambia, Kwani wewe kuwa peke yako, wala hapana mtu pamoja nawe? Daudi akamwambia Ahimeleki, kuhani, Mfalme ameniagiza shughuli, akaniambia, Asijue mtu awaye yote habari ya shughuli hii ninayokutuma, wala ya neno hili ninalokuamuru; nami nimewaagiza vijana waende mahali fulani. Kuna nini basi, chini ya mkono wako? Nipe mkononi mwangu mikate mitano, au cho chote ulicho nacho hapa. Yule kuhani akamjibu Daudi, akasema, Hapana mikate ya sikuzote chini ya mkono wangu, ila mikate mitakatifu; ikiwa wale vijana wamejitenga na wanawake. Naye Daudi akamjibu kuhani, akamwambia, Hakika tumejitenga na wanawake siku hizi tatu; napo nilipotoka, vyombo vya vijana hawa vilikuwa vitakatifu, ingawa ilikuwa safari ya sikuzote; basi leo je! Vyombo vyetu havitakuwa vitakatifu zaidi? Ndipo kuhani akampa ile mikate mitakatifu; kwa maana hapakuwa na mikate ila ile ya Wonyesho, nayo imekwisha kuondolewa mbele za BWANA, ili itiwe mikate ya moto siku ile ilipoondolewa. Basi siku ile palikuwapo na mtu mmoja wa watumishi wa Sauli, amezuiwa hapo mbele za BWANA jina lake akiitwa Doegi, Mwedomi, mkubwa wa wachungaji wa Sauli. Tena Daudi akamwambia Ahimeleki, Na hapa chini ya mkono wako, je! Hapana mkuki, au upanga? Kwa maana sikuleta upanga, wala silaha zangu, kwa sababu ile shughuli ya mfalme ilitaka haraka. Yule kuhani akasema, upanga wa Goliathi, yule Mfilisti, uliyemwua katika bonde la Ela, tazama, upo hapa, umefungwa ndani ya nguo nyuma ya naivera; ukipenda kuuchukua, haya! Uchukue, maana hapa hapana mwingine ila huo tu. Daudi akasema, Hapana mwingine kama ule; haya! Nipe. Basi Daudi akaondoka, akakimbia siku ile, kwa hofu ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi. Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, Je! Huyu siye yule Daudi, mfalme wa nchi? Je! Hawakuimbiana habari zake katika ngoma zao, kusema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Naye Daudi akayatia maneno hayo moyoni mwake, akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi. Akaubadilisha mwenendo wake mbele yao, akajifanya mwenye wazimu mikononi mwao, akakuna-kuna katika mbao za mlango, na kuyaacha mate yake kuanguka juu ya ndevu zake. Ndipo huyo Akishi akawaambia watumishi wake, Angalieni, mwaona ya kuwa mtu huyu ana wazimu; basi, maana yake nini kumleta kwangu? Je! Mimi nina haja ya watu wenye wazimu, hata mmemleta kiumbe hiki ili aonyeshe wazimu wake machoni pangu? Je! Huyu ataingia nyumbani mwangu?
1 Samueli 21:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Daudi akaenda Nobu, kwa Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akatetemeka alipokutana naye, akamuuliza, “Kwa nini uko peke yako? Kwa nini hukufuatana na mtu yeyote?” Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, akisema, “Mfalme ameniagiza shughuli fulani na kuniambia, ‘Mtu yeyote asijue chochote kuhusu kazi yako wala maagizo yako!’ Kuhusu watu wangu, nimewaambia tukutane mahali fulani. Sasa basi, una nini mkononi? Nipatie mikate mitano au chochote unachoweza kupata.” Lakini kuhani akamjibu Daudi, “Sina mkate wowote wa kawaida kwa sasa. Hata hivyo, ipo hapa mikate iliyowekwa wakfu, iwapo watu wamejitenga na wanawake.” Daudi akajibu, “Hakika tumejitenga na wanawake kwa siku hizi chache kama kawaida ya ninapotoka kwenda kwenye shughuli. Navyo vyombo vya wale vijana huwa ni vitakatifu hata kwenye safari ya kawaida, si zaidi sana leo vyombo vyao vitakuwa ni vitakatifu?” Hivyo kuhani akampa ile mikate iliyowekwa wakfu, kwa kuwa hapakuwepo mikate mingine isipokuwa hiyo ya Wonyesho iliyokuwa imeondolewa hapo mbele za BWANA na kubadilishwa na mingine yenye moto siku ile ilipoondolewa. Basi siku hiyo palikuwepo na mmoja wa watumishi wa Sauli, aliyezuiliwa mbele za BWANA; alikuwa Doegi Mwedomu, kiongozi wa wachunga wanyama wa Sauli. Daudi akamuuliza Ahimeleki, “Je, unao mkuki au upanga hapa? Sikuleta upanga wala silaha nyingine yoyote, kwa sababu shughuli ya mfalme ilikuwa ya haraka.” Kuhani akajibu, “Upanga wa Goliathi Mfilisti, ambaye ulimuua katika Bonde la Ela, upo hapa, umefungiwa katika kitambaa nyuma ya kisibau. Kama unauhitaji, uchukue, hakuna upanga mwingine hapa ila huo tu.” Daudi akasema, “Hakuna upanga mwingine kama huo. Nipatie huo.” Siku ile Daudi akamkimbia Sauli na kwenda kwa Akishi mfalme wa Gathi. Lakini watumishi wa Akishi wakamwambia, “Je, huyu si ndiye Daudi mfalme wa nchi? Je, huyu si ndiye yule ambaye wanaimba katika ngoma zao wakisema: “ ‘Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake’?” Daudi akayaweka maneno haya moyoni naye akamwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi. Basi akajifanya mwendawazimu mbele yao; naye alipokuwa mikononi mwao, alitenda kama kichaa, akikwaruza kwa kutia alama juu ya milango ya lango na kuachia udelele kutiririka kwenye ndevu zake. Akishi akawaambia watumishi wake, “Tazameni mtu huyu! Ana wazimu! Kwa nini mnamleta kwangu? Je, mimi nimepungukiwa na wenda wazimu kiasi kwamba mmeniletea mtu huyo hapa aendelee kufanya hivi mbele yangu? Je, ilikuwa ni lazima mtu huyo aje nyumbani kwangu?”