1 Samueli 19:1-10
1 Samueli 19:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi. Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anakusudia kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha; na mimi nitatoka nje na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, nami nitazungumza na babangu habari zako; nami nikiona neno lolote nitakuambia. Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana. Kwa kuwa alihatarisha maisha yake, na kumpiga yule Mfilisti, naye BWANA akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure? Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo BWANA, yeye hatauawa. Basi Yonathani akamwita Daudi, naye Yonathani akamjulisha mambo hayo yote. Kisha Yonathani akamleta Daudi kwa Sauli, naye alikuwa akihudumu mbele yake, kama hapo awali. Baada ya hayo kulikuwa na vita tena; naye Daudi akatoka, naye akapigana na Wafilisti, naye akawaua kwa uuaji mkuu; nao wakakimbia mbele yake. Tena ikawa, roho mbaya kutoka kwa BWANA ilimjia Sauli, hapo alipoketi ndani ya nyumba yake, akiwa na mkuki wake mkononi mwake; naye Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake. Sauli akajaribu kumpiga Daudi hadi ukutani kwa mkuki wake, ila yeye akaponyoka kutoka mbele ya Sauli, nao huo mkuki akaupiga ukutani; naye Daudi akakimbia, akaokoka usiku ule.
1 Samueli 19:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi. Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha; na mimi nitatoka nje na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, nami nitazungumza na babangu habari zako; nami nikiona neno lo lote nitakuambia. Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana. Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti, naye BWANA akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure? Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo BWANA, yeye hatauawa. Basi Yonathani akamwita Daudi, naye Yonathani akamjulisha mambo hayo yote. Kisha Yonathani akamleta Daudi kwa Sauli, naye alikuwa akihudhuria mbele yake, kama kwanza. Baada ya hayo kulikuwa na vita tena; naye Daudi akatoka, naye akapigana na Wafilisti, naye akawaua kwa uuaji mkuu; nao wakakimbia mbele yake. Tena ikawa, roho mbaya kutoka kwa BWANA ilimjilia Sauli, hapo alipoketi ndani ya nyumba yake, akiwa na mkuki wake mkononi mwake; naye Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake. Sauli akajaribu kumpiga Daudi hata ukutani kwa mkuki wake, ila yeye akaponyoka kutoka mbele ya Sauli, nao huo mkuki akaupiga ukutani; naye Daudi akakimbia, akaokoka usiku ule.
1 Samueli 19:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sauli akamwambia mwanawe Yonathani na watumishi wake wote wamuue Daudi. Lakini Yonathani mwana wa Sauli alimpenda sana Daudi. Yonathani akamwonya Daudi, akisema, “Baba yangu Sauli anatafuta nafasi ya kukuua. Ujilinde kesho asubuhi, nenda mahali pa siri na ukae huko. Nitatoka na kukaa na baba yangu shambani mahali uliko. Nitazungumza naye juu yako, nami nitakueleza nitakachogundua.” Yonathani akanena mema juu ya Daudi kwa Sauli baba yake na kumwambia, “Mfalme asitende mabaya kwa mtumishi wake Daudi; hajakukosea, aliyoyafanya yamekuwa ya faida sana kwako. Alihatarisha maisha yake alipomuua yule Mfilisti. BWANA akajipatia ushindi mkubwa kwa ajili ya Israeli wote, nawe uliuona na ukafurahi. Kwa nini basi utende mabaya kwa mtu asiye na hatia kama Daudi kwa kumuua bila sababu?” Sauli akamsikiliza Yonathani na kuapa hivi: “Hakika kama BWANA aishivyo, Daudi hatauawa.” Basi Yonathani akamwita Daudi na kumweleza mazungumzo yote. Akamleta kwa Sauli, naye Daudi akawa pamoja na Sauli kama kwanza. Vita vilitokea tena, naye Daudi akatoka na kupigana na Wafilisti. Akawapiga kwa nguvu nyingi hata wakakimbia mbele yake. Lakini roho mbaya iliyoachiwa nafasi na BWANA ikaja juu ya Sauli alipokuwa ameketi katika nyumba yake akiwa na mkuki mkononi mwake. Daudi alipokuwa anampigia kinubi, Sauli akajaribu kumchomea Daudi ukutani kwa huo mkuki wake, lakini Daudi akauhepa huo mkuki wa Sauli ukakita ukutani. Usiku ule ule Daudi akakimbia na kuokoka.
1 Samueli 19:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Shauli alimweleza mwanawe Yonathani na maofisa wake juu ya mpango wake wa kumwua Daudi. Lakini Yonathani, mwanawe Shauli, alimpenda sana Daudi. Kwa hiyo, akamwambia, “Baba yangu anakusudia kukuua. Hivyo, jihadhari. Kesho asubuhi, jifiche mahali pa siri, ukae hapo. Mimi nitakuja na kusimama karibu na baba yangu huko shambani mahali utakapokuwa. Hapo nitaongea naye juu yako, na kitu chochote nitakachogundua kutoka kwake, nitakueleza.” Yonathani alimsifu Daudi mbele ya baba yake, akamwambia, “Usitende dhambi dhidi ya mtumishi wako Daudi kwani yeye hajatenda dhambi yoyote dhidi yako; matendo yake yote anapokutumikia daima yamekuwa mema kwako. Alipomuua yule Mfilisti Goliathi, alihatarisha maisha yake, naye Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli ushindi mkubwa. Wewe ulipoona jambo lile ulifurahi. Kwa nini unataka kutenda dhambi kwa kumwaga damu isiyo na hatia kwa kumwua Daudi bila sababu?” Shauli alimsikiliza Yonathani, kisha akaapa, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, sitamuua Daudi.” Hivyo, Yonathani akamwita Daudi na kumweleza mambo hayo yote. Yonathani akampeleka Daudi kwa Shauli, na Daudi akamtumikia Shauli kama hapo awali. Baadaye kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Waisraeli. Daudi alitoka akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na waliosalia wakamkimbia. Kisha, roho mbaya kutoka kwa Mwenyezi-Mungu alimjia Shauli alipokuwa amekaa nyumbani kwake akiwa ameshika mkuki mkononi, wakati ambapo Daudi alikuwa akipiga kinubi. Shauli alijaribu kumchoma Daudi kwa mkuki huo, Lakini Daudi alikwepa mkuki wa Shauli na mkuki ukapiga ukuta. Daudi akakimbia na kutoroka.