1 Samueli 15:17-23
1 Samueli 15:17-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha makabila ya Israeli? Naye BWANA akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli. Kisha BWANA akakutuma safarini, akasema, Nenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hadi watakapoangamia. Mbona basi hukuitii sauti ya BWANA, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA? Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya BWANA, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa. Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng'ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, huko Gilgali. Naye Samweli akasema, Je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikiza ushauri kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama uovu na kuabudu vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.
1 Samueli 15:17-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Samueli akamwambia, “Ingawa unajiona kuwa wewe si maarufu, je, wewe si kiongozi wa makabila ya Israeli? Mwenyezi-Mungu alikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli. Mwenyezi-Mungu alipokutuma alikuambia, ‘Nenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hadi umewaua wote!’ Kwa nini basi, hukuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu? Kwa nini mkakimbilia nyara na hivyo kutenda jambo ovu mbele ya Mwenyezi-Mungu?” Shauli akajibu, “Nimetii sauti ya Mwenyezi-Mungu. Nilikwenda kule alikonituma Mwenyezi-Mungu; nimemleta Agagi mfalme wa Waamaleki, na nimewaangamiza kabisa Waamaleki. Lakini watu walichukua nyara: Kondoo, ng'ombe na vitu vyote bora vilivyotolewa viangamizwe ili kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, huko Gilgali.” Ndipo Samueli akamwambia, “Je, Mwenyezi-Mungu anapendelea zaidi dhabihu za kuteketezwa na matambiko, kuliko kuitii sauti yake? Tazama, kumtii yeye ni bora kuliko matambiko na kumsikiliza kuliko kumtambikia mafuta ya beberu. Uasi ni sawa na dhambi ya kupiga ramli, na kiburi ni sawa na uovu na kuabudu vinyago. Kwa sababu umeikataa amri ya Mwenyezi-Mungu, naye amekukataa kuwa mfalme.”
1 Samueli 15:17-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye BWANA akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli. Kisha BWANA akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia. Mbona, basi, hukuitii sauti ya BWANA, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA? Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya BWANA, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa. Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng’ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, huko Gilgali. Naye Samweli akasema, je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.
1 Samueli 15:17-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Samweli akamwambia, “Ingawa zamani ulijiona mdogo machoni pako mwenyewe, Je, hukuwa kiongozi wa kabila za Israeli? BWANA alikutia mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli. Naye akakutuma kwa kazi maalum, akisema, ‘Nenda ukaangamize kabisa wale watu waovu, wale Waamaleki, upigane nao vita mpaka utakapowaangamiza kabisa.’ Kwa nini hukumtii BWANA? Kwa nini ulivamia nyara na kufanya uovu machoni pa BWANA?” Sauli akasema, “Lakini nilimtii BWANA. Nilikamilisha ile kazi ambayo BWANA alinituma. Niliwaangamiza Waamaleki kabisa na kumleta Agagi mfalme wao. Askari walichukua kondoo na ngʼombe kutoka kwenye nyara, zile ambazo ni nzuri sana zimewekwa wakfu kwa Mungu, ili zitolewe dhabihu kwa BWANA Mungu wako huko Gilgali.” Lakini Samweli akajibu: “Je, BWANA anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu kama vile kuitii sauti ya BWANA? Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu, nako kusikia ni bora kuliko mafuta ya kondoo dume. Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi, nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu. Kwa sababu umelikataa neno la BWANA, naye amekukataa wewe kuendelea kuwa mfalme.”