Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 13:4-17

1 Samueli 13:4-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Waisraeli wote waliposikia kuwa Shauli alikuwa ameishinda ngome ya kijeshi ya Wafilisti, na kwamba Wafilisti wanawachukia sana Waisraeli, waliitwa kwenda kuungana na Shauli huko Gilgali. Wafilisti walikuwa na magari 30,000, askari 6,000 wapandafarasi na kikosi cha askari wa miguu wengi kama mchanga wa pwani; wote walipanda juu na kupiga kambi yao huko Mikmashi, mashariki ya Beth-aveni. Waisraeli walipoona wako taabuni (maana walikuwa wanashambuliwa vikali), walianza kujificha. Wengine walijificha mapangoni, wengine mashimoni, wengine kwenye miamba, wengine kwenye makaburi na wengine kwenye visima. Wengine walivuka mto Yordani mpaka katika nchi ya Gadi na nchi ya Gileadi. Lakini Shauli alikuwa bado huko Gilgali na watu wote walimfuata wakitetemeka. Shauli alimngoja Samueli kwa muda wa siku saba, kama Samueli alivyosema. Lakini Samueli hakuja huko Gilgali na watu walianza kumwacha Shauli. Basi, Shauli akawaambia watu, “Nileteeni sadaka yenu ya kuteketezwa na zile za amani.” Naye akatolea sadaka ya kuteketezwa. Mara tu alipokuwa anamaliza kutoa sadaka ya kuteketezwa, Samueli aliwasili. Shauli akatoka nje kwenda kumlaki Samueli na kumsalimia. Samueli akamwuliza, “Umefanya nini?” Shauli akamjibu, “Nilipoona watu wananiacha, na wewe hukuja, katika muda wa siku ulizosema, na tena nilipoona Wafilisti wamejipanga tayari kwa vita huko Mikmashi, nikawaza kwamba Wafilisti watakuja kunishambulia huko Gilgali. Tena nilikuwa bado sijaomba fadhili za Mwenyezi-Mungu. Ndipo nilipolazimika kutolea mimi mwenyewe sadaka ya kuteketezwa.” Samueli akamjibu Shauli, “Umefanya kipumbavu. Hukutii aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Kama ungetii, Mwenyezi-Mungu angeudumisha milele ufalme wako juu ya Israeli. Lakini sasa ufalme wako hautadumu kwa kuwa amri aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu hukuitii. Mwenyezi-Mungu amejitafutia mtu mwingine ambaye atamtii kwa moyo wote, na huyo ndiye ambaye amemteua kuwa mtawala juu ya watu wake.” Samueli akaondoka kutoka Gilgali na kwenda huko Gibea katika nchi ya Benyamini. Shauli alipowahesabu watu waliokuwa pamoja naye, aliona wako watu 600 tu. Shauli na Yonathani mwanawe pamoja na watu waliokuwa pamoja nao, walikaa huko Gibea katika nchi ya Benyamini na Wafilisti walipiga kambi huko Mikmashi. Wafilisti walitoka kwenye kambi yao kwenda kuwashambulia wakiwa wako katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra katika nchi ya Shuali.

1 Samueli 13:4-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Waisraeli wote wakasikia habari ya kwamba Sauli ameipiga hiyo ngome ya Wafilisti, na ya kwamba Waisraeli wamepata kuwa makuruhi kwa Wafilisti. Basi hao watu wakakusanyika pamoja kumfuata Sauli huko Gilgali. Nao Wafilisti wakakusanyika ili wapigane na Waisraeli, magari elfu thelathini, na wapanda farasi elfu sita, na watu kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi wao; wakapanda juu, wakapiga kambi yao katika Mikmashi, upande wa mashariki wa Beth-aveni. Hata Waisraeli walipoona ya kuwa wako katika dhiki, (maana watu walifadhaishwa), ndipo hao watu wakajificha katika mapango, na katika vichaka, na katika miamba, na katika mashimo, na katika mabirika. Hata baadhi ya Waebrania walivuka Yordani, wakaingia nchi ya Gadi na Gileadi; lakini Sauli alikuwa angali huko Gilgali, nao watu wote wakamfuata wakitetemeka. Akangoja siku saba, kwa kadiri ya muda uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao watu wakatawanyika mbali naye. Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa. Hata mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu. Samweli akasema, Umefanya nini? Naye Sauli akasema, Ni kwa sababu niliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa; nao Wafilisti wamekusanyika pamoja huko Mikmashi; basi nikasema, Wafilisti watanishukia sasa mpaka Gilgali, kabla sijaomba fadhili za BWANA; kwa hiyo nilijishurutisha, nikatoa sadaka ya kuteketezwa. Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya BWANA, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana BWANA angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele. Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru. Basi Samweli akaondoka, akapanda kutoka Gilgali mpaka Gibea ya Benyamini. Naye Sauli akawahesabu watu waliokuwapo pamoja naye, wakawa kama mia sita. Naye Sauli, na mwanawe Yonathani, na watu waliokuwapo pamoja nao, wakakaa huko Geba ya Benyamini; lakini Wafilisti wakatua katika Mikmashi. Nao watekaji wa nyara wakatoka katika kambi ya hao Wafilisti, vikosi vitatu; kikosi kimoja kikageukia njia iendayo Ofra, mpaka nchi ya Shuali

1 Samueli 13:4-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Waisraeli wote wakasikia habari ya kwamba Sauli ameipiga hiyo ngome ya Wafilisti, na ya kwamba Waisraeli wamepata kuwa makuruhi kwa Wafilisti. Basi hao watu wakakusanyika pamoja kumfuata Sauli huko Gilgali. Nao Wafilisti wakakusanyana ili wapigane na Waisraeli, magari thelathini elfu, na wapanda farasi sita elfu, na watu kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi wao; wakapanda juu, wakapiga kambi yao katika Mikmashi, upande wa mashariki wa Beth-aveni. Hata Waisraeli walipoona ya kuwa wa katika dhiki, (maana watu walifadhaishwa), ndipo hao watu wakajificha katika mapango, na katika vichaka, na katika miamba, na katika mashimo, na katika mabirika. Hata baadhi ya Waebrania walivuka Yordani, wakaingia nchi ya Gadi na Gileadi; lakini Sauli alikuwa akaliko huko Gilgali, nao watu wote wakamfuata wakitetemeka. Akangoja siku saba, kwa kadiri ya muhula uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao watu wakatawanyika mbali naye. Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa. Hata mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu. Samweli akasema, Umefanya nini? Naye Sauli akasema, Ni kwa sababu naliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa; nao Wafilisti wamekusanyika pamoja huko Mikmashi; basi nikasema, Wafilisti watanishukia sasa mpaka Gilgali, kabla sijaomba fadhili za BWANA; kwa hiyo nalijishurutisha, nikatoa sadaka ya kuteketezwa. Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya BWANA, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana BWANA angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele. Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru. Basi Samweli akaondoka, akapanda kutoka Gilgali mpaka Gibea ya Benyamini. Naye Sauli akawahesabu watu waliokuwapo pamoja naye, wapata kama mia sita. Naye Sauli, na mwanawe Yonathani, na watu waliokuwapo pamoja nao, wakakaa huko Geba ya Benyamini; lakini Wafilisti wakatua katika Mikmashi. Nao watekaji wa nyara wakatoka katika marago ya hao Wafilisti, vikosi vitatu; kikosi kimoja kikageukia njia iendayo Ofra, mpaka nchi ya Shuali

1 Samueli 13:4-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hivyo Israeli wote wakasikia habari kwamba: “Sauli ameshambulia ngome ya Wafilisti, nao sasa Israeli wamekuwa harufu mbaya kwa Wafilisti.” Basi watu waliitwa kuungana na Sauli huko Gilgali. Wafilisti wakakusanyika ili kupigana na Israeli, wakiwa na magari ya vita 3,000, waendesha magari ya vita 6,000 na askari wa miguu wengi kama mchanga wa ufuoni mwa bahari. Walipanda na kupiga kambi huko Mikmashi, mashariki ya Beth-Aveni. Watu wa Israeli walipoona kuwa hali yao ni ya hatari na kuwa jeshi lao limesongwa sana, wakajificha katika mapango na katika vichaka, katikati ya miamba, kwenye mashimo na kwenye mahandaki. Hata baadhi ya Waebrania wakavuka Yordani mpaka nchi ya Gadi na Gileadi. Sauli akabaki huko Gilgali, navyo vikosi vyote vilivyokuwa pamoja naye vilikuwa vikitetemeka kwa hofu. Akangoja kwa siku saba, muda uliowekwa na Samweli; lakini Samweli hakuja Gilgali, nao watu wa Sauli wakaanza kutawanyika. Basi akasema, “Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani.” Naye Sauli akatoa sadaka ya kuteketezwa. Mara alipomaliza kutoa hiyo sadaka, Samweli akatokea, naye Sauli akaondoka kwenda kumlaki. Samweli akamuuliza, “Umefanya nini?” Sauli akajibu, “Nilipoona kwamba watu wanatawanyika, na kwamba hukuja wakati uliopangwa na kwamba Wafilisti walikuwa wakikusanyika huko Mikmashi, nikawaza, ‘Sasa Wafilisti watateremka dhidi yangu huko Gilgali nami sijaomba kibali kwa BWANA.’ Hivyo nikalazimika kutoa sadaka ya kuteketezwa.” Samweli akasema, “Umetenda kwa upumbavu. Hukuyashika maagizo ya BWANA Mungu wako aliyokupa. Kama ungelitii, angeudumisha ufalme wako juu ya Israeli kwa wakati wote. Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amemtafuta mtu aupendezaye moyo wake, na amemchagua awe kiongozi wa watu wake, kwa sababu hukuyatii maagizo ya BWANA.” Kisha Samweli akaondoka Gilgali, akapanda Gibea ya Benyamini, naye Sauli akawahesabu watu aliokuwa nao. Jumla yao walikuwa watu 600. Sauli, mwanawe Yonathani na watu waliokuwa pamoja nao walikuwa wakiishi huko Gibea ya Benyamini, wakati Wafilisti wakiwa wamepiga kambi huko Mikmashi. Makundi ya wavamiaji walikuja kutoka kambi ya Wafilisti katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra karibu na Shuali