1 Petro 5:1-5
1 Petro 5:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi mzee miongoni mwenu wazee wenzangu, mimi ambaye nilishuhudia mateso ya Kristo na kushiriki ule utukufu utakaofunuliwa, nawasihini mlichunge lile kundi la Mungu mlilokabidhiwa; mlitunze si kwa kulazimika, bali kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo si kwa tamaa ya fedha, bali kwa moyo wenu wote. Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa hilo kundi. Na wakati Mchungaji Mkuu atakapotokea, nyinyi mtapokea taji ya utukufu isiyofifia. Kadhalika nanyi vijana mnapaswa kujiweka chini ya mamlaka ya wazee. Nyinyi nyote mnapaswa kuwa na unyenyekevu mpate kutumikiana; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwajalia neema wanyenyekevu.”
1 Petro 5:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana wa wale walio chini ya utunzaji wao, bali iweni mifano kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtalipokea taji la utukufu, lile lisilokauka. Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.
1 Petro 5:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka. Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.
1 Petro 5:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa wazee waliomo miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo, na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa: lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi. Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtapokea taji ya utukufu isiyoharibika. Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa, “Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”