Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Petro 4:1-19

1 Petro 4:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Maadamu Kristo aliteseka kimwili, nanyi pia mnapaswa kujiimarisha kwa nia hiyo yake; maana mtu akisha teseka kimwili hahusiki tena na dhambi. Tangu sasa, basi, maisha yaliyowabakia kuishi hapa duniani yanapaswa kuongozwa na matakwa ya Mungu, sio na tamaa za kibinadamu. Wakati uliopita mlikuwa na muda mrefu wa kufanya mambo wanayofanya watu wasiomjua Mungu. Mliishi maisha ya anasa, ubinafsi, ulevi, ugomvi, kunywa mno na ya ibada haramu za sanamu. Sasa, watu hao wasiomjua Mungu wanashangaa wanapoona kwamba hamwandamani nao tena katika hali ya kuishi vibaya, na hivyo wanawatukaneni. Lakini watapaswa kutoa hoja juu ya jambo hilo mbele yake Mungu aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa! Ndiyo maana Habari Njema ilihubiriwa hata kwa hao waliokufa, ili baada ya kuhukumiwa katika maisha yao ya kimwili kama wengine, waishi kwa ajili ya Mungu kwa njia ya Roho. Mwisho wa vitu vyote umekaribia. Kwa hiyo mnapaswa kuwa na utaratibu na kukesha ili muweze kusali. Zaidi ya yote pendaneni kwa moyo wote, maana upendo hufunika dhambi nyingi. Muwe na ukarimu nyinyi kwa nyinyi bila kunung'unika. Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine kama wakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu. Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina. Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida. Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili muweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa. Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa nanyi. Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu ambaye anapaswa kuteseka kwa sababu ni mwuaji, mwizi, mhalifu au mwovu. Lakini kama mtu akiteseka kwa sababu ni Mkristo, basi, asione aibu, bali amtukuze Mungu, kwa sababu mtu huyo anaitwa kwa jina la Kristo. Wakati wa hukumu umefika, na hukumu hiyo inaanza na watu wake Mungu mwenyewe. Ikiwa hukumu hiyo inaanzia kwetu sisi, basi, mwisho wake utakuwa namna gani kwa wale wasioamini Habari Njema ya Mungu? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa; itakuwaje basi, kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi?” Kwa hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa.

Shirikisha
Soma 1 Petro 4

1 Petro 4:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni silaha ya nia ile ile; kwa maana yeye aliyeteswa katika mwili ameachana na dhambi. Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani. Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuishi katika uzinzi, tamaa, ulevi, na karamu za kula na kunywa vileo kupindukia, na ibada haramu ya sanamu; mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana. Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa. Maana kwa ajili hiyo hata hao waliokufa walihubiriwa Injili, ili kwamba wahukumiwe katika mwili kama wahukumiwavyo wanadamu; bali wawe hai katika roho kama Mungu alivyo hai. Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala. Zaidi ya yote iweni na bidii kubwa katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi. Mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung'unika; kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu. Mtu akisema, na aseme kama asemaye maneno halisi ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina. Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili pia katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe. Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia. Lakini pasiwe na hata mmoja wenu atakayeteseka kwa kuwa mwuaji, mwizi, mhalifu au hata mfitini. Lakini ikiwa mtu yeyote miongoni mwenu anateseka kwa sababu ni Mkristo, asione haya, bali amtukuze Mungu maana ana jina hili. Kwa maana wakati umefika wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu; na ikianza kwetu sisi, mwisho wao wasioitii Injili ya Mungu utakuwaje? Na mwenye haki akiokoka kwa shida, yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi ataonekana wapi? Basi wao wateswao kwa mapenzi ya Mungu na wamwekee amana roho zao, katika kutenda mema, kama kwa Muumba mwaminifu.

Shirikisha
Soma 1 Petro 4

1 Petro 4:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni silaha ya nia ile ile; kwa maana yeye aliyeteswa katika mwili ameachana na dhambi. Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani. Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali; mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana. Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa. Maana kwa ajili hiyo hata hao waliokufa walihubiriwa Injili, ili kwamba wahukumiwe katika mwili kama wahukumiwavyo wanadamu; bali wawe hai katika roho kama Mungu alivyo hai. Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala. Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi. Mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung’unika; kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu. Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina. Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe. Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia. Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine. Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo. Kwa maana wakati umefika wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu; na ikianza kwetu sisi, mwisho wao wasioitii injili ya Mungu utakuwaje? Na mwenye haki akiokoka kwa shida, yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi ataonekana wapi? Basi wao wateswao kwa mapenzi ya Mungu na wamwekee amana roho zao, katika kutenda mema, kama kwa Muumba mwaminifu.

Shirikisha
Soma 1 Petro 4

1 Petro 4:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia iyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki ya kuishi hapa duniani kwa tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi kwa mapenzi ya Mungu. Maana wakati uliopita mmekwisha kutumia muda wa kutosha katika maisha yenu mkifanya yale ambayo wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu. Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika huo wingi wa maisha ya ufisadi, nao huwatukana ninyi. Lakini itawapasa wao kutoa hesabu mbele zake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa. Kwa kuwa hii ndiyo sababu Injili ilihubiriwa hata kwa wale waliokufa, ili wahukumiwe sawasawa na wanadamu wengine katika mwili, lakini katika roho waishi kulingana na Mungu aishivyo. Mwisho wa mambo yote umekaribia. Kwa hiyo kuweni na akili tulivu na kiasi, mkikesha katika kuomba. Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko. Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu. Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen. Wapenzi, msione ajabu kwa yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata. Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Kristo, ili mpate kufurahi zaidi wakati utukufu wake utakapofunuliwa. Kama mkitukanwa kwa ajili ya jina la Kristo, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu na wa Mungu anakaa juu yenu. Lakini asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu anayeteswa kwa kuwa ni muuaji, au mwizi, au mhalifu wa aina yoyote, au anayejishughulisha na mambo ya watu wengine. Lakini kama ukiteseka kwa kuwa Mkristo, usihesabu jambo hilo kuwa ni aibu, bali mtukuze Mungu kwa sababu umeitwa kwa jina hilo. Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanzia katika nyumba ya Mungu. Basi kama ikianzia kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje? Basi, “Ikiwa ni vigumu kwa mwenye haki kuokoka, itakuwaje kwa mtu asiyemcha Mungu na mwenye dhambi?” Kwa hiyo, wale wanaoteswa kulingana na mapenzi ya Mungu, wajikabidhi kwa Muumba wao aliye mwaminifu, huku wakizidi kutenda mema.

Shirikisha
Soma 1 Petro 4