Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Petro 3:1-22

1 Petro 3:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Nanyi wake, jiwekeni chini ya mamlaka ya waume zenu, ili kama wako waume wowote wasioamini neno la Mungu, wapate kuamini kwa kuuona mwenendo wenu. Haitakuwa lazima kwenu kusema neno, kwani wataona jinsi mwenendo wenu ulivyo safi na wa kumcha Mungu. Katika kujipamba kwenu msitegemee mambo ya njenje, kama vile mitindo ya kusuka nywele, kujivalia vitu vya dhahabu na nguo maridadi. Bali, uzuri wenu unapaswa kutokana na hali ya ndani ya utu wa kweli, uzuri usioharibika wa wema na utulivu wa roho, ambao ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu. Ndivyo walivyojipamba hapo kale wanawake waadilifu waliomtumainia Mungu; walijiweka chini ya mamlaka ya waume zao. Sara kwa mfano alimtii Abrahamu na kumwita yeye bwana. Nyinyi mmekuwa sasa binti zake kama mkitenda mema bila kuogopa tisho lolote. Kadhalika nanyi waume, katika kuishi na wake zenu mnapaswa kutambua kwamba wao ni dhaifu na hivyo muwatendee kwa heshima; maana nao pia watapokea pamoja nanyi zawadi ya uhai anaowapeni Mungu. Hapo sala zenu hazitatiliwa kizuizi. Mwisho nasema hivi: Mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikira moja; mnapaswa kupendana kindugu, kuwa wapole na wanyenyekevu nyinyi kwa nyinyi. Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana nyinyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Anayetaka kufurahia maisha, na kuona siku za fanaka, ajizuie asiseme mabaya aepe kusema uongo. Ajiepushe na uovu, atende mema, atafute amani na kuizingatia. Maana Bwana huwatazama kwa wema waadilifu na kuzisikiliza sala zao. Lakini huwapa kisogo watu watendao maovu.” Ni nani atakayeweza kuwadhuru nyinyi kama mkizingatia kutenda mema? Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi. Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu, lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima. Muwe na dhamiri njema, kusudi mnapotukanwa, wale wanaosema ubaya juu ya mwenendo wenu mwema kama Wakristo, waone aibu. Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, kama Mungu akipenda, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu. Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke nyinyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho; na kwa maisha yake ya kiroho alikwenda kuwahubiria wale roho waliokuwa kifungoni. Hao ndio wale waliokataa kumtii Mungu alipowangoja kwa saburi wakati Noa alipokuwa anatayarisha ile safina. Ndani ya chombo hicho ni watu wachache tu, yaani watu wanane, waliookolewa katika maji, ambayo yalikuwa mfano wa ubatizo unaowaokoa nyinyi sasa. Ubatizo si shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Huwaokoeni kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi.

Shirikisha
Soma 1 Petro 3

1 Petro 3:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama kunao wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno, kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu. Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi. Badala yake, kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa moyoni, yaani uzuri usioharibika wa roho ya upole na utulivu, ambayo ni ya thamani sana machoni pa Mungu. Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao, kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, hata akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema, bila kuogopa jambo lolote. Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu, na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha neema cha uzima, ili kusiwepo na chochote cha kuzuia maombi yenu. Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, na mwe wasikitivu na wanyenyekevu. Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka. Kwa maana, “Yeyote apendaye uzima na kuona siku njema, basi auzuie ulimi wake usinene mabaya, na midomo yake isiseme hila. Mtu huyo lazima aache uovu, akatende mema; lazima aitafute amani na kuifuatilia sana. Kwa maana macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake yako makini kusikiliza maombi yao. Bali uso wa Bwana uko kinyume na watendao maovu.” Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye juhudi katika kutenda mema? Lakini mmebarikiwa hata kama ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.” Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu yeyote atakayewauliza kuhusu sababu ya tumaini lililomo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima, mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo waaibike kwa ajili ya masingizio yao. Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema, kama kuteseka huko ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu. Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili ya wasio haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho. Baada ya kufanywa hai, alikwenda na kuzihubiria roho zilizokuwa kifungoni: roho hizo ambazo zamani hazikutii, wakati ule uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Noa, wakati wa kujenga safina, ambamo watu wachache tu, yaani watu wanane, waliokolewa ili wasiangamie kwa gharika. Nayo maji hayo ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia: si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu, kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo. Yeye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu; nao malaika, mamlaka na nguvu zote wametiishwa chini yake.

Shirikisha
Soma 1 Petro 3

1 Petro 3:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu. Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao. Kama vile Sara alivyomtii Abrahamu, akamwita bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, pasipo kutishwa na hofu yoyote. Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; maana wao pia ni warithi wa neema ya uzima, ili maombi yenu yasizuiliwe na chochote. Neno la mwisho ni hili; muwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka. Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme uongo. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana uko juu ya watenda mabaya. Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini hata mkiteswa kwa sababu ya kutenda haki, mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa heshima. Nanyi muwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; akauawa kimwili, lakini akahuishwa kiroho, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiria; watu wasiotii hapo zamani, wakati Mungu alipowavumilia kwa subira, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo. Naye yuko katika mkono wa kulia wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.

Shirikisha
Soma 1 Petro 3

1 Petro 3:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu. Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao. Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote. Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe. Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka. Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya. Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri; watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo. Naye yupo mkono wa kuume wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.

Shirikisha
Soma 1 Petro 3

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha