1 Wafalme 8:22-66
1 Wafalme 8:22-66 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Solomoni alisimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, naye, akiwa mbele ya jumuiya yote ya Waisraeli, aliinua mikono yake juu, akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu mwingine kama wewe, juu mbinguni, ama chini duniani! Wewe u mwaminifu, kwani umetimiza agano lako na kuwaonesha fadhili zako watumishi wako wanaoishi wakikutii kwa moyo wao wote. Umetimiza ahadi uliyoitoa kwa mtumishi wako Daudi baba yangu; naam, yale uliyonena umeyatimiza leo kwa uwezo wako mwenyewe. Kwa hiyo, sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninakuomba pia utimize ile ahadi uliyomwahidi mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ukisema: ‘Siku zote utakuwa na mzawa wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, iwapo wazawa wako watakuwa waangalifu kuhusu mwenendo wao mbele yangu kama wewe ulivyofanya mbele yangu.’ Basi, ee Mungu wa Israeli, nakusihi utimize hayo yote uliyomwahidi mtumishi wako, Daudi baba yangu. “Lakini, ee Mungu, kweli utakaa duniani? Ikiwa hata mbingu zenyewe wala mbingu za juu sana hazikutoshi, itakutoshaje nyumba hii ambayo nimeijenga? Hata hivyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mimi mtumishi wako nakuomba unisikie na kunitimizia ombi langu ninaloomba leo. Ichunge nyumba hii usiku na mchana, mahali ambapo umesema, ‘Hapo ndipo watu watakapoliheshimu jina langu;’ unisikie ninapokuja mahali hapa kuomba. Sikia maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watu wako Israeli wanapoomba wakielekea mahali hapa. Usikie maombi kutoka huko mbinguni; na ukisha sikia, utusamehe. “Mtu akimkosea mwenzake, naye akaletwa apate kuapa mbele ya madhabahu yako katika nyumba hii, naye akiapa, tafadhali wewe usikie kutoka huko mbinguni, uchukue hatua na kuwahukumu watumishi wako. Aliye na hatia umwadhibu kadiri ya makosa yake, asiye na hatia umwachilie na kumpatia tuzo kadiri ya uadilifu wake. “Ikiwa watu wako Waisraeli, wameshindwa na adui zao kwa sababu ya dhambi walizotenda dhidi yako, nao wakitubu kwako na kulikiri jina lako, wakiomba msamaha wako kwa unyenyekevu katika nyumba hii, basi, uwasikie kutoka huko mbinguni, uwasamehe watu wako Israeli dhambi zao, halafu uwarudishe katika nchi uliyowapa babu zao. “Mvua isiponyesha kwa sababu wametenda dhambi dhidi yako, wakiomba wakielekea mahali hapa na kulikiri jina lako, pia wakiziacha dhambi zao unapowaonya, tafadhali, uwasikie kutoka huko mbinguni, na usamehe dhambi za watumishi wako, watu wako Israeli, huku ukiwafundisha kufuata njia nyofu; ukanyeshe mvua katika nchi yako hii ambayo uliwapa watu wako iwe mali yako. “Iwapo kuna njaa nchini, au tauni, ukame, ugonjwa wa mimea, nzige au viwavi; au ikiwa watu wako wamezingirwa na adui zao katika mji wao wowote ule; ikiwa kuna pigo lolote au ugonjwa wowote, tafadhali, usikie maombi yoyote yatakayoombwa na watu wako, Israeli, au yatakayoombwa na mtu yeyote au watu wako wote wa Israeli; kila mtu akijua taabu za moyoni mwake, akikuomba huku akinyosha mikono yake kuelekea kwenye nyumba hii. Basi, usikie huko kwako mbinguni, utoe msamaha na kuchukua hatua; pia umtendee kila mtu kadiri anavyostahili (kwani ni wewe tu ujuaye mawazo ya mioyo ya wanadamu wote); ili wakutii wakati wote wanapoishi katika nchi uliyowapa babu zetu. “Vivyo hivyo, wakati mgeni asiye mmoja wa watu wako Israeli akija kutoka nchi ya mbali kwa ajili ya jina lako (maana watu wa mataifa mengine watasikia sifa zako na kuhusu nguvu na uwezo wako), mtu huyo akija na kuomba katika nyumba hii, nakusihi umsikie kutoka huko mbinguni, na umjalie huyo mgeni yote atakayokuomba; kusudi watu wote ulimwenguni wapate kujua jina lako na kukutii kama wafanyavyo watu wako, Israeli, na wapate kufahamu kwamba nyumba hii ambayo nimeijenga, inajulikana kwa jina lako. “Watu wako wakienda vitani kupigana na adui yao kokote kule utakakowapeleka, nao wakikuomba wakielekea mji uliouchagua na nyumba niliyoijenga kwa ajili ya jina lako, nakusihi usikie sala yao na maombi yao huko mbinguni, uwapatie ushindi vitani. “Ikiwa watatenda dhambi dhidi yako maana hakuna mtu asiyetenda dhambi, nawe ukiwakasirikia na kuwaacha washindwe na adui, hata wapelekwe mateka mpaka nchi ya adui iliyoko mbali au karibu; kama watakapokuwa huko uhamishoni watajirudi moyoni na kutubu na kukuomba msamaha, wakisema, ‘Tumetenda dhambi; tumepotoka na kufanya maovu;’ pia wakati huo watakapokuwa katika nchi ya adui zao, wakitubu kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote, na kama watakuomba wakielekea nchi yao ambayo uliwapatia babu zao, wakielekea mji huu ambao uliuchagua na nyumba hii ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako, basi, nakusihi kutoka huko mbinguni uliko usikie sala yao na ombi lao uwapatie haki zao. Uwasamehe watu wako dhambi walizotenda dhidi yako na uasi wao, uwahurumie mbele ya adui zao, ili nao wapate kuwahurumia, maana ni watu wako, na ni mali yako; watu ambao uliwatoa Misri kutoka katika tanuri ya chuma. “Uangalie ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako, Israeli, uwasikie kila wanapokuomba. Kwa sababu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu uliwatenga na watu wa mataifa mengine duniani, ili wawe mali yako – kama ulivyotangaza kwa njia ya Mose, mtumishi wako, wakati ule ulipowatoa babu zetu katika nchi ya Misri.” Solomoni alipomaliza kusema sala hiyo yote na ombi lake kwa Mwenyezi-Mungu aliinuka kutoka pale mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, mahali alipokuwa amepiga magoti akiinua mikono yake juu. Alisimama, akawabariki Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika hapo, akisema kwa sauti kubwa, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewapatia starehe watu wake Israeli, kulingana na ahadi yake. Ametimiza ahadi zake zote njema alizozitoa kupitia kwa mtumishi wake Mose. Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, awe nasi, kama alivyokuwa na babu zetu; tunaomba asituache, wala asitutupe. Yeye aelekeze mioyo yetu kwake, ili tufuate njia zake, tukishika amri zake, maongozi yake na maagizo yake aliyowapa babu zetu. Basi, maneno yangu haya ambayo ni ombi langu mbele ya Mwenyezi-Mungu, yawe karibu na Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mchana na usiku, naye amjalie mtumishi wake, na watu wake Israeli, ili wafanikiwe katika haja zao za kila siku. Nayo mataifa yote ulimwenguni yatajua kwamba kweli Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu; wala hakuna mwingine. Nanyi, muwe waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mkifuata masharti yake na kutii amri zake zote kama mnavyofanya hivi leo.” Kisha, mfalme Solomoni na Waisraeli wote waliokuwa pamoja naye walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko. Naye Solomoni alimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za amani: Ng'ombe 22,000 na kondoo 120,000. Hivyo ndivyo mfalme na watu wote wa Israeli walivyoiweka wakfu nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Siku hiyohiyo, mfalme aliiweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwani hapo ndipo alipotolea sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba haikutosha sadaka hizo zote. Naye Solomoni kwa muda wa siku saba na siku saba zaidi, yaani kwa siku kumi na nne, alifanya sikukuu pamoja na Waisraeli wote; nao walitoka tangu kiingilio cha Hamathi, hadi mto wa Misri. Katika siku ya nane, Solomoni aliwaaga watu; nao wakamtakia baraka mfalme, wakaenda kwao wakishangilia na kufurahi kwa sababu ya wema ambao Mwenyezi-Mungu aliuonesha kwa Daudi, mtumishi wake, na kwa watu wake Israeli
1 Wafalme 8:22-66 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake mbinguni. Akasema Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote. Umemtimizia mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo. Na sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umtimizie mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli machoni pangu, kama watoto wako wakiangalia njia zao, ili kuenenda mbele zangu kama wewe ulivyoenenda. Sasa, Ee Mungu wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu. Lakini Mungu je? Hakika atakaa juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga! Lakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee BWANA, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo. Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa. Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe. Ikiwa mtu amemkosa mwenzake, na kupewa sharti ya kiapo aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako, katika nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimpatiliza mtu mbaya, kwa kuleta njia yake juu ya kichwa chake; na kumpa mwenye haki haki yake, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake. Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea tena kwako, na kulikiri jina lako wakikuomba na kukusihi katika nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni, ukawaachilie watu wako Israeli dhambi yao, ukawarejeshe tena katika nchi uliyowapa baba zao. Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, wakati ule utakapowatesa; basi, usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; unapowafundisha njia iliyo njema, iwapasayo kuiendea; ukanyeshe mvua katika nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi wao. Ikiwa kuna njaa katika nchi, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewazingira katika mji wao wowote ule; au ukiwapo msiba wowote, au ugonjwa wowote; maombi yoyote au dua yoyote ikifanywa na mtu yeyote, au na watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu maradhi ya moyo wake, na kuikunjua mikono yake kuielekea nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe, ukatende, ukampe kila mtu kwa kadiri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu wote); ili wakuche wewe siku zote watakazoishi katika nchi uliyowapa baba zetu. Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako; (maana watasikia habari za jina lako kuu, na za mkono wako ulio hodari, na za mkono wako ulionyoshwa); atakapokuja na kuomba kuielekea nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukatende kwa kadiri ya yote atakayokuomba mgeni huyo; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe kama watu wako Israeli, nao wajue ya kuwa nyumba hii, niliyoijenga, imeitwa kwa jina lako. Ikiwa watu wako watoka kwenda kupigana na adui zao, kwa njia yoyote utakayowapeleka, wakikuomba, BWANA, kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi, uyasikie huko mbinguni maombi yao na dua yao, ukaitetee haki yao. Ikiwa wamekutenda dhambi, (maana hakuna mtu asiyetenda dhambi), hata ukawaghadhibikia, ukawatia katika mikono ya adui zao, wawachukue mateka mpaka nchi ya adui zao, iliyo mbali au iliyo karibu; basi, wakijirudia nafsi zao katika nchi ile watakayochukuliwa mateka, wakitubu, na kukusihi katika nchi ya hao waliowachukua mateka, wakisema, Tumekosa, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu; watakaporejea kwako kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya adui zao, waliowachukua mateka, wakikuomba, kwa kuikabili nchi yao, uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi, uyasikie maombi yao na dua yao, huko mbinguni, makao yako, ukaitetee haki yao; ukawasamehe watu wako waliokutenda dhambi, na makosa yao yote waliyokukosa; ukawape kuonewa huruma mbele yao waliowachukua mateka, ili wapate kuwahurumia. Kwa kuwa ni watu wako, na urithi wako, uliowatoa katika Misri, toka katikati ya tanuri ya chuma. Macho yako na yafumbuke, na kuielekea dua ya mtumwa wako, na dua za watu wako Israeli, ukawasikilize kila wakati watakapokulilia. Kwa maana uliwatenga na watu wote wa dunia, wawe urithi wako, kama ulivyonena kwa mdomo wa Musa, mtumishi wako, hapo ulipowatoa baba zetu katika Misri, Ee Bwana MUNGU. Hata ikawa, Sulemani alipokwisha kumwomba BWANA maombi hayo, na dua hiyo yote, akasimama na kuondoka hapo mbele ya madhabahu ya BWANA, hapo alipokuwa amepiga magoti, na kuikunjua mikono yake kuelekea mbinguni. Akasimama, na kuwabariki mkutano wote wa Israeli kwa sauti kuu, akasema, Na ahimidiwe BWANA, aliyewapa watu wake Israeli kustarehe, vile vile kama yote aliyoyaahidi. Halikukosa kupatikana neno lolote katika ahadi yake njema, aliyoahidi kwa mkono wa Musa, mtumishi wake. BWANA, Mungu wetu, na akae nasi, kama alivyokaa na baba zetu; asituache, wala asitutupe; aielekeze mioyo yetu kwake, ili tuende katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na sheria zake, na hukumu zake, alizowaamuru baba zetu. Na maneno yangu haya, niliyoyaomba mbele za BWANA, na yawe karibu na BWANA, Mungu wetu, mchana na usiku, ili aitetee haki ya mtumishi wake, na haki ya watu wake Israeli, kwa kadiri ya haja zao za kila siku. Watu wote wa ulimwengu wajue ya kuwa BWANA ndiye Mungu; hakuna mwingine. Mioyo yenu na iwe kamili kwa BWANA, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo. Ndipo mfalme, na Israeli wote pamoja naye, wakatoa sadaka mbele za BWANA. Sulemani akatoa sadaka za amani, alizomtolea BWANA, ng'ombe elfu ishirini na mbili, na kondoo elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na wana wa Israeli wote walivyoiweka wakfu nyumba ya BWANA. Siku ile ile mfalme akaitakasa behewa ya katikati iliyokuwa mbele ya nyumba ya BWANA; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za BWANA ilikuwa ndogo, haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta ya sadaka za amani. Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, kutoka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, mbele za BWANA, Mungu wetu, siku saba na siku saba, yaani siku kumi na nne. Hata siku ya nane akaagana na watu, nao wakambarikia mfalme, wakaenda hemani kwao, wakifurahi na kuchangamka moyoni kwa wema wote BWANA aliomfanyia Daudi mtumishi wake, na Israeli watu wake.
1 Wafalme 8:22-66 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake mbinguni. Akasema Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote. Umemtimizia mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo. Na sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli machoni pangu, kama watoto wako wakiangalia njia zao, ili kuenenda mbele zangu kama wewe ulivyoenenda. Sasa, Ee Mungu wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu. Lakini Mungu je? Atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga! Walakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee BWANA, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo. Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa. Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe. Ikiwa mtu amemkosa mwenzake, na kupewa sharti ya kiapo aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako, katika nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimpatiliza mtu mbaya, kwa kuleta njia yake juu ya kichwa chake; na kumpa mwenye haki haki yake, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake. Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea tena kwako, na kulikiri jina lako wakikuomba na kukusihi katika nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni, ukawaachilie watu wako Israeli dhambi yao, ukawarejeze tena katika nchi uliyowapa baba zao. Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, wakati ule utakapowatesa; basi, usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; unapowafundisha njia iliyo njema, iwapasayo kuiendea; ukanyeshe mvua juu ya nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi wao. Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao; au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote; maombi yo yote au dua yo yote ikifanywa na mtu awaye yote, au na watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu maradhi ya moyo wake, na kuikunjua mikono yake kuielekea nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe, ukatende, ukampe kila mtu kwa kadiri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu wote); ili wakuche wewe siku zote watakazoishi katika nchi uliyowapa baba zetu. Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako; (maana watasikia habari za jina lako kuu, na za mkono wako ulio hodari, na za mkono wako ulionyoshwa); atakapokuja na kuomba kuielekea nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukatende kwa kadiri ya yote atakayokuomba mgeni huyo; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe kama watu wako Israeli, nao wajue ya kuwa nyumba hii, niliyoijenga, imeitwa kwa jina lako. Ikiwa watu wako watoka kwenda kupigana na adui zao, kwa njia yo yote utakayowapeleka, wakikuomba, BWANA, kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi, uyasikie huko mbinguni maombi yao na dua yao, ukaitetee haki yao. Ikiwa wamekutenda dhambi, (maana hakuna mtu asiyetenda dhambi), hata ukawaghadhibikia, ukawatia katika mikono ya adui zao, wawachukue mateka mpaka nchi ya adui zao, iliyo mbali au iliyo karibu; basi, wakijirudia nafsi zao katika nchi ile watakayochukuliwa mateka, wakitubu, na kukusihi katika nchi ya hao waliowachukua mateka, wakisema, Tumekosa, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu; watakaporejea kwako kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya adui zao, waliowachukua mateka, wakikuomba, kwa kuikabili nchi yao, uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi, uyasikie maombi yao na dua yao, huko mbinguni, makao yako, ukaitetee haki yao; ukawasamehe watu wako waliokutenda dhambi, na makosa yao yote waliyokukosa; ukawape kuonewa huruma mbele yao waliowachukua mateka, ili wapate kuwahurumia. Kwa kuwa ni watu wako, na urithi wako, uliowatoa katika Misri, toka katikati ya tanuu ya chuma. Macho yako na yafumbuke, na kuielekea dua ya mtumwa wako, na dua za watu wako Israeli, ukawasikilize kila wakati watakapokulilia. Kwa maana uliwatenga na watu wote wa dunia, wawe urithi wako, kama ulivyonena kwa mdomo wa Musa, mtumishi wako, hapo ulipowatoa baba zetu katika Misri, Ee Bwana MUNGU. Hata ikawa, Sulemani alipokwisha kumwomba BWANA maombi hayo, na dua hiyo yote, akasimama na kuondoka hapo mbele ya madhabahu ya BWANA, hapo alipokuwa amepiga magoti, na kuikunjua mikono yake kuelekea mbinguni. Akasimama, na kuwabariki mkutano wote wa Israeli kwa sauti kuu, akasema, Na ahimidiwe BWANA, aliyewapa watu wake Israeli kustarehe, vile vile kama yote aliyoyaahidi. Halikukosa kupatikana neno lo lote katika ahadi yake njema, aliyoahidi kwa mkono wa Musa, mtumishi wake. BWANA, Mungu wetu, na akae nasi, kama alivyokaa na baba zetu; asituache, wala asitutupe; aielekeze mioyo yetu kwake, ili tuende katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na sheria zake, na hukumu zake, alizowaamuru baba zetu. Na maneno yangu haya, niliyoyaomba mbele za BWANA, na yawe karibu na BWANA, Mungu wetu, mchana na usiku, ili aitetee haki ya mtumishi wake, na haki ya watu wake Israeli, kwa kadiri ya haja zao za kila siku. Watu wote wa ulimwengu wajue ya kuwa BWANA ndiye Mungu; hakuna mwingine. Mioyo yenu na iwe kamili kwa BWANA, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo. Ndipo mfalme, na Israeli wote pamoja naye, wakatoa sadaka mbele za BWANA. Sulemani akatoa sadaka za amani, alizomtolea BWANA, ng’ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na wana wa Israeli wote walivyoifanya wakfu nyumba ya BWANA. Siku ile ile mfalme akaitakasa behewa ya katikati iliyokuwa mbele ya nyumba ya BWANA; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za BWANA ilikuwa ndogo, haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta ya sadaka za amani. Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, kutoka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, mbele za BWANA, Mungu wetu, siku saba na siku saba, yaani siku kumi na nne. Hata siku ya nane akaagana na watu, nao wakambarikia mfalme, wakaenda hemani kwao, wakifurahi na kuchangamka moyoni kwa wema wote BWANA aliomfanyia Daudi mtumishi wake, na Israeli watu wake.
1 Wafalme 8:22-66 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Solomoni akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA machoni pa kusanyiko lote la Israeli, akakunjua mikono yake kuelekea mbinguni na kusema: “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe juu mbinguni wala chini duniani, wewe unayetunza Agano lako la upendo na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote. Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo. “Sasa BWANA, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, kama wanao wakiangalia yote wayafanyayo kuenenda mbele zangu kama vile ulivyofanya.’ Sasa, Ee Mungu wa Israeli, acha neno lako lile ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litimie. “Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga! Hata hivyo sikiliza dua ya mtumishi wako na maombi yake kwa huruma, Ee BWANA Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambayo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo. Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwako humo,’ ili kwamba upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa. Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia kutoka mbinguni, mahali pa makao yako na usikiapo, samehe. “Mtu anapomkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili, basi, sikia kutoka mbinguni na ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimhukumu yule mwenye hatia na kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie mwenye haki kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kuwa haki kwake. “Wakati watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, watakapokugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili, basi usikie kutoka mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao. “Wakati mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka dhambi zao kwa sababu umewaadhibu, basi usikie kutoka mbinguni na usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi. “Wakati njaa au tauni vikija juu ya nchi, au koga au kawa, nzige au panzi, au wakati adui atakapowazingira katika mji wao wowote, maafa ya namna yoyote au ugonjwa wowote unaoweza kuwajia, wakati dua au maombi yatakapofanywa na mmojawapo wa watu wako Israeli, kila mmoja akitambua taabu za moyo wake mwenyewe, naye akainyoosha mikono yake kuelekea Hekalu hili: basi usikie kutoka mbinguni, katika makao yako. Usamehe na utende, umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote), ili wakuogope kwa wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu. “Kwa habari ya mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako, kwa maana watu watasikia juu ya Jina lako kuu na juu ya mkono wako wenye nguvu na mkono wako ulionyooshwa, atakapokuja na kuomba kuelekea Hekalu hili, basi na usikie kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, ukafanye lolote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli nao wapate pia kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako. “Wakati watu wako watakapokwenda vitani dhidi ya adui zao, popote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa BWANA kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, basi usikie dua na maombi yao kutoka mbinguni, ukawatetee haki yao. “Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu yeyote ambaye hatendi dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi yake mwenyewe, mbali au karibu; na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya wale waliowashinda na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa, tumetenda uovu’; kama wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako; basi kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, usikie dua yao na maombi yao na kuitetea haki yao. Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako; uwasamehe makosa yote waliyoyatenda dhidi yako, ukawafanye wale waliowashinda kuwaonea huruma; kwa maana ni watu wako na urithi wako, uliowatoa Misri, kutoka kwenye lile tanuru la kuyeyushia chuma. “Macho yako na yafumbuke juu ya ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako Israeli, nawe uwasikilize wakati wowote wanapokulilia. Kwa maana uliwachagua wao kutoka mataifa yote ya ulimwengu kuwa urithi wako mwenyewe, kama ulivyotangaza kupitia mtumishi wako Mose wakati wewe, Ee BWANA Mwenyezi, ulipowatoa baba zetu kutoka Misri.” Wakati Solomoni alipomaliza dua hizi zote na maombi kwa BWANA, akainuka kutoka mbele ya madhabahu ya BWANA, mahali alipokuwa amepiga magoti, mikono yake ikawa imekunjuliwa kuelekea juu mbinguni. Akasimama na kubariki kusanyiko lote la Israeli kwa sauti kubwa akisema: “Ahimidiwe BWANA, aliyewapa pumziko watu wake Israeli kama vile alivyokuwa ameahidi. Hakuna hata neno moja lililopunguka kati ya ahadi zote nzuri alizozitoa kupitia mtumishi wake Mose. BWANA Mungu wetu na awe pamoja nasi kama alivyokuwa na baba zetu, kamwe asituache wala kutukataa. Yeye na aielekeze mioyo yetu kwake, ili tutembee katika njia zake zote na kuzishika amri na maagizo na masharti aliyowapa baba zetu. Nami maneno yangu haya, ambayo nimeyaomba mbele za BWANA, yawe karibu na BWANA Mungu wetu usiku na mchana, ili kwamba atetee shauri la mtumishi wake na la watu wake Israeli kulingana na hitaji lao la kila siku, ili kwamba mataifa yote ya dunia wajue kwamba BWANA ndiye Mungu na kwamba hakuna mwingine. Lakini ni lazima mwiweke mioyo yenu kikamilifu kwa BWANA Mungu wetu, kuishi kwa maagizo yake na kutii amri zake, kama ilivyo wakati huu.” Kisha mfalme na Israeli wote pamoja naye wakatoa dhabihu mbele za BWANA. Solomoni akatoa dhabihu sadaka za amani kwa BWANA: ngʼombe 22,000, pamoja na kondoo na mbuzi 120,000. Hivyo ndivyo mfalme na Waisraeli wote walivyoweka wakfu Hekalu la BWANA. Siku iyo hiyo mfalme akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la BWANA na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za BWANA ilikuwa ndogo sana kuweza kubeba sadaka hizo za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya sadaka ya amani. Hivyo Solomoni akaiadhimisha sikukuu kwa wakati ule, na Israeli wote pamoja naye. Walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. Wakaiadhimisha mbele za BWANA Mungu wetu kwa siku saba na siku saba zaidi, yaani, jumla siku kumi na nne. Siku iliyofuata, aliwaruhusu watu waondoke. Wakambariki mfalme, kisha wakaenda nyumbani, wakiwa na mashangilio na furaha rohoni kwa ajili ya mambo yote mema ambayo BWANA ametenda kwa ajili ya Daudi mtumishi wake na watu wake Israeli.