Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 8:12-21

1 Wafalme 8:12-21 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Ndipo Sulemani akasema, “Mwenyezi Mungu alisema kwamba ataishi katika giza nene; naam, hakika nimekujengea Hekalu zuri sana, mahali pako pa kuishi milele.” Kusanyiko lote la Israeli walipokuwa wamesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki. Kisha akasema: “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mkono wake mwenyewe ametimiza alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema, ‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Israeli kutoka Misri, sikuchagua mji katika kabila lolote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo na Jina langu liwe humo, bali nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’ “Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako. Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni mwili wako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’ “Mwenyezi Mungu ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu, na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Nimetenga nafasi humo kwa ajili ya Sanduku la Agano, ambalo ndani yake kuna lile Agano la Mwenyezi Mungu alilofanya na baba zetu alipowatoa Misri.”