1 Wafalme 5:13-18
1 Wafalme 5:13-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme Solomoni alikusanya watu 30,000 kutoka kila mahali nchini Israeli, wafanye kazi za kulazimishwa, akamweka Adoniramu awe msimamizi wao. Aliwagawa watu hao katika makundi matatu ya watu 10,000 kila moja, akayapeleka makundi hayo kwa zamu, mwezi mmoja Lebanoni na miezi miwili nyumbani. Solomoni alikuwa pia na wachukuzi wa mizigo 70,000, na wachongaji mawe milimani 80,000, mbali na maofisa wakuu 3,300 waliosimamia kazi hiyo na wafanyakazi wote. Kwa amri ya mfalme, walichimbua mawe makubwa na ya thamani, ili yachongwe kwa ajili ya kujengea msingi wa nyumba. Basi, hivyo ndivyo wajenzi wa Solomoni na Hiramu na watu wa mji wa Gebali walivyotayarisha mawe na mbao za kujengea nyumba hiyo.
1 Wafalme 5:13-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mfalme Sulemani akakusanya kutoka kila mahali katika Israeli watu wa shokoa nao walikuwa elfu thelathini. Akatuma watu elfu kumi huko Lebanoni kwa zamu kila mwezi. Mwezi mmoja walikaa huko Lebanoni na miezi miwili walikuweko nyumbani kwao. Na Adoramu alikuwa msimamizi wa shokoa. Sulemani alikuwa na wapagazi elfu sabini na wakatao miti milimani elfu themanini; mbali na maafisa wake Sulemani waliokuwa wakuu wa kazi wa watu elfu tatu waliotenda kazi. Mfalme akaamuru, nao wakaleta mawe makubwa, mawe ya thamani, ili wauweke msingi wa nyumba kwa mawe yaliyochongwa. Na waashi wa Sulemani na waashi wa Hiramu na Wagebali wakayachonga, wakaweka tayari miti na mawe ya kuijenga nyumba.
1 Wafalme 5:13-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mfalme Sulemani akafanya shokoa ya Israeli wote; nayo shokoa hiyo ilikuwa ya watu thelathini elfu. Akawatuma Lebanoni kwa mwezi, elfu kumi kwa zamu. Mwezi mmoja walikuwako huko Lebanoni, na miezi miwili wakawako kwao. Na Adoramu alikuwa juu ya shokoa. Sulemani alikuwa na wachukua mizigo sabini elfu, na wakatao miti themanini elfu milimani; mbali na maakida yake Sulemani waliokuwa juu ya kazi, elfu tatu na mia tatu, wasimamizi wa watu waliotenda kazi. Mfalme akaamuru, nao wakaleta mawe makubwa, mawe ya thamani, ili wauweke msingi wa nyumba kwa mawe yaliyochongwa. Na waashi wa Sulemani na waashi wa Hiramu na Wagebali wakayachonga, wakaweka tayari miti na mawe ya kuijenga nyumba.
1 Wafalme 5:13-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mfalme Solomoni akakusanya wafanyakazi 30,000 kutoka Israeli yote. Akawapeleka Lebanoni kwa zamu za watu 10,000 kwa mwezi, hivyo walikaa Lebanoni kwa mwezi mmoja na miezi miwili nyumbani. Adoniramu ndiye alikuwa kiongozi wa shokoa. Solomoni alikuwa na wachukuzi wa mizigo 70,000 na wachonga mawe 80,000 huko vilimani, pamoja na wasimamizi 3,300 ambao walisimamia kazi hiyo na kuwaongoza wafanyakazi. Kwa amri ya mfalme walitoa kwenye machimbo ya mawe, mawe makubwa, yaliyo bora kwa kujengea msingi wa nyumba yaliyochongwa kwa ajili ya Hekalu. Mafundi wa Solomoni, wa Hiramu na watu wa Gebali walikata na kuandaa mbao na mawe kwa ajili ya ujenzi wa Hekalu.