Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 5:1-12

1 Wafalme 5:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Naye mfalme Hiramu wa Tiro, aliyekuwa rafiki ya Daudi, alipopata habari kwamba Solomoni amekuwa mfalme mahali pa baba yake, alituma watumishi kwake. Ndipo Solomoni akampelekea Hiramu ujumbe huu: “Wajua kwamba baba yangu Daudi hakuweza kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, hekalu la kumwabudia, kwa sababu ya kukumbana na vita vingi dhidi ya maadui wa nchi jirani mpaka hapo Mwenyezi-Mungu alipompatia ushindi. Lakini sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, amenijalia amani pande zote. Sina adui wala taabu. Basi, nimeamua kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nyumba ya kumwabudia. Na hii ni sawa kabisa kama Mwenyezi-Mungu alivyomwahidi baba yangu akisema: ‘Mwanao ambaye nitamfanya aketi katika kiti chako cha enzi, atanijengea nyumba!’ Sasa basi, uwaamuru watu wako wanikatie mierezi ya Lebanoni. Watu wangu watajiunga na watu wako katika kazi hiyo, nami nitawalipa watumishi wako kadiri utakavyosema; kwani kama ujuavyo, hakuna yeyote mwenye ujuzi wa kukata miti kama nyinyi Wasidoni.” Hiramu alifurahi sana alipopata ujumbe huu wa Solomoni, akasema, “Mwenyezi-Mungu asifiwe wakati huu, kwa kumpa Daudi mwana mwenye hekima atawale taifa hili kubwa.” Kisha, Hiramu alimpelekea Solomoni ujumbe, akisema, “Nimepokea ujumbe wako, nami niko tayari kutimiza mahitaji yako kuhusu mbao za mierezi na za miberoshi. Watu wangu watasomba magogo na kuyateremsha kutoka Lebanoni mpaka baharini na kuyafunga mafungumafungu yaelee juu ya maji mpaka mahali utakaponielekeza. Huko, yatafunguliwa, nawe utayapokea. Kwa upande wako, wewe utanipa chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwangu.” Basi, Hiramu alimpa Solomoni mbao zote za aina ya mierezi na miberoshi alizohitaji, naye Solomoni akampa Hiramu ngano madebe 240,000, na mafuta safi madebe 200 kila mwaka, kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake. Basi, Mwenyezi-Mungu akampa Solomoni hekima kama alivyomwahidi. Kukawa na amani kati ya Solomoni na Hiramu; wakafanya mkataba kati yao.

1 Wafalme 5:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo Hiramu, mfalme wa Tiro, akawatuma watumishi wake kwa Sulemani; kwani alikuwa amesikia ya kwamba wamemtia mafuta awe mfalme mahali pa baba yake. Kwa maana Hiramu alikuwa akimpenda Daudi siku zote. Basi Sulemani akatuma watu kwa Hiramu, akasema, Wajua kuwa Daudi baba yangu hakuweza kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wake, kwa sababu ya vita vilivyomzunguka pande zote, hata BWANA alipowatia watu chini ya nyayo zake. Ila leo BWANA, Mungu wangu, amenipa amani kila upande; hakuna adui, wala tukio baya. Nami, tazama, nakusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, kama BWANA alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu. Basi uamuru wanikatie mierezi ya Lebanoni; na watumishi wangu watafuatana na watumishi wako; na ujira wa watumishi wako nitakupa kama utakavyosema; kwa kuwa wajua ya kwamba hakuna kwetu mtu ajuaye kukata miti kama Wasidoni. Ikawa, Hiramu aliposikia maneno yake Sulemani, alifurahi sana, akasema, Na ahimidiwe BWANA leo, aliyempa Daudi mwana mwenye akili juu ya watu hawa walio wengi. Hiramu akatuma watu kwa Sulemani, akasema, Nimeusikia ujumbe ulionitumia; nami nitafanya kila ulitakalo kuhusu miti ya mierezi, na miti ya miberoshi. Watumishi wangu wataishusha toka Lebanoni mpaka baharini; nami nitaiendesha baharini, ikifungwa pamoja, mpaka mahali utakaponiagiza, huko nitaifungua ili wewe uichukue; ndivyo utakavyoitimiza haja yangu, ukiwapa chakula watu wa nyumbani mwangu. Basi Hiramu akampa Sulemani miti ya mierezi na miti ya miberoshi kadiri alivyotaka. Sulemani akampa Hiramu kori elfu ishirini za ngano, chakula cha watu wake, na kori ishirini za mafuta safi. Ndizo Sulemani alizompa Hiramu mwaka kwa mwaka. BWANA akampa Sulemani hekima, kama alivyomwahidia. Ikawa amani kati yao Hiramu na Sulemani; wakafanya mikataba kati yao wawili.

1 Wafalme 5:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo Hiramu, mfalme wa Tiro, akawatuma watumishi wake kwa Sulemani; kwani alikuwa amesikia ya kwamba wamemtia mafuta awe mfalme mahali pa baba yake. Kwa maana Hiramu alikuwa akimpenda Daudi siku zote. Basi Sulemani akatuma watu kwa Hiramu, akasema, Umemjua Daudi baba yangu jinsi asivyoweza kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wake, kwa sababu ya vita vilivyomzunguka pande zote, hata BWANA alipowatia watu chini ya nyayo zake. Ila leo BWANA, Mungu wangu, amenipa amani kila upande; hakuna adui, wala tukio baya. Nami, tazama, nakusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, kama BWANA alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu. Basi uamuru wanikatie mierezi ya Lebanoni; na watumishi wangu watafuatana na watumishi wako; na ujira wa watumishi wako nitakupa kama utakavyosema; kwa kuwa wajua ya kwamba hakuna kwetu mtu ajuaye kukata miti kama Wasidoni. Ikawa, Hiramu aliposikia maneno yake Sulemani, alifurahi sana, akasema, Na ahimidiwe BWANA leo, aliyempa Daudi mwana mwenye akili juu ya watu hawa walio wengi. Hiramu akatuma watu kwa Sulemani, akasema, Nimeyasikia yale uliyoniletea; nami nitafanya kila ulitakalo katika habari ya miti ya mierezi, na miti ya miberoshi. Watumishi wangu wataishusha toka Lebanoni mpaka baharini; nami nitaiendesha baharini, ikifungwa pamoja, mpaka mahali utakaponiagiza, huko nitaifungua ili wewe uichukue; ndivyo utakavyoitimiza haja yangu, ukiwapa chakula watu wa nyumbani mwangu. Basi Hiramu akampa Sulemani miti ya mierezi na miti ya miberoshi kadiri alivyotaka. Sulemani akampa Hiramu kori ishirini elfu za ngano, chakula cha watu wake, na kori ishirini za mafuta safi. Ndizo Sulemani alizompa Hiramu mwaka kwa mwaka. BWANA akampa Sulemani hekima, kama alivyomwahidia. Ikawa amani kati yao Hiramu na Sulemani; wakafanyana maagano pamoja hao wawili.

1 Wafalme 5:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hiramu mfalme wa Tiro aliposikia kuwa Solomoni ametiwa mafuta awe mfalme mahali pa Daudi baba yake, akatuma wajumbe kwa Solomoni, kwa sababu Hiramu siku zote alikuwa na uhusiano mzuri wa kirafiki na Daudi. Solomoni akapeleka ujumbe huu kwa Hiramu: “Unajua kwamba kwa sababu ya vita vilivyopiganwa dhidi ya baba yangu Daudi kutoka pande zote, hakuweza kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA Mungu wake, hadi BWANA alipowaweka adui zake chini ya miguu yake. Lakini sasa BWANA Mungu wangu amenipa utulivu kila upande hakuna adui wala maafa. Kwa hiyo, ninakusudia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wangu, kama BWANA alivyomwambia baba yangu Daudi, wakati aliposema, ‘Mwanao nitakayemweka kwenye kiti cha ufalme mahali pako, ndiye atajenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’ “Hivyo toa amri ili mierezi ya Lebanoni ikatwe kwa ajili yangu. Watu wangu watafanya kazi na watu wako, nami nitawalipa watu wako kwa ujira wowote utakaoupanga. Unajua kwamba hatuna mtu yeyote mwenye ustadi katika kukata miti kama Wasidoni.” Hiramu aliposikia ujumbe wa Solomoni, akafurahishwa sana akasema, “Ahimidiwe BWANA leo, kwa kuwa amempa Daudi mwana mwenye hekima kutawala juu ya taifa hili kubwa.” Hiramu akatuma neno kwa Solomoni: “Nimepokea ujumbe ulionipelekea na nitafanya yote unayohitaji katika kukupatia magogo ya mierezi na misunobari. Watu wangu watayakokota kutoka Lebanoni hadi kwenye bahari, nami nitayafunga mafungu mafungu yaelee juu ya maji hadi utakapoelekeza. Huko nitayatenganisha, nawe utaweza kuyachukua. Wewe utakidhi haja yangu kwa kunipatia chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwangu.” Kwa njia hii Hiramu akampa Solomoni miti yote ya mierezi na magogo ya misunobari kama alivyohitaji, naye Solomoni akampa Hiramu kori 20,000 za ngano kama chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake, pamoja na mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa bathi 20,000. Solomoni aliendelea kumfanyia Hiramu hivyo mwaka baada ya mwaka. BWANA akampa Solomoni hekima, kama alivyomwahidi. Palikuwepo na uhusiano wa amani kati ya Hiramu na Solomoni, na wote wawili wakafanya mkataba.