1 Wafalme 20:12-22
1 Wafalme 20:12-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, Ben-hadadi alipolisikia neno hilo, naye alikuwa akinywa, yeye na wafalme, mabandani, aliwaambia watumwa wake, Jipangeni. Wakajipanga juu ya mji. Na tazama, nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli, akasema, BWANA asema hivi, Je! Umeona makutano haya yote walio wengi? Angalia, nitawatia leo mkononi mwako; nawe utajua ya kuwa ndimi BWANA. Ahabu akanena, Kwa nani? Akasema, BWANA asema hivi, Kwa vijana wa watawala wa majimbo. Ndipo akanena, Ni nani atakayepanga vita? Naye akajibu, Ni wewe. Ndipo akawakusanya vijana wa watawala wa majimbo, nao walikuwa mia mbili thelathini na wawili; kisha baada ya hao akawakusanya watu wote, wana wa Israeli wote, nao walikuwa elfu saba. Wakatoka wakati wa adhuhuri. Lakini Ben-hadadi alikuwa akinywa hata kulewa mabandani, yeye na wale wafalme thelathini na wawili waliomsaidia. Wakatoka wale vijana wa watawala wa majimbo wakitangulia; na Ben-hadadi akatuma watu, nao wakamwambia, Wako watu wametoka katika Samaria. Akasema, Kwamba wametoka kwa amani, wakamateni wa hai; au kwamba wametoka kwa vita, wakamateni wa hai. Basi wakatoka mjini hao vijana wa watawala wa majimbo, na jeshi nyuma yao. Wakapiga kila mmoja mtu wake; Washami wakakimbia, na Israeli wakawafuatia; Ben-hadadi mfalme wa Shamu akaokoka amepanda farasi, pamoja na wapandao farasi. Mfalme wa Israeli akatoka, akawapiga farasi na magari, akawapiga Washami pigo kubwa. Naye yule nabii akamjia mfalme wa Israeli, akamwambia, Nenda, kusanya nguvu zako, ujue, na kuangalia ufanyavyo; kwa maana mwakani mfalme wa Shamu atakuja juu yako.
1 Wafalme 20:12-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Ben-hadadi alipokea ujumbe huu wa Ahabu wakati yeye na wafalme waliomwunga mkono walipokuwa mahemani mwao wanakunywa. Basi, akayaweka majeshi yake katika hali ya tahadhari, kuushambulia mji. Wakati huohuo, nabii mmoja akamwendea Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Unaona wingi wa majeshi haya? Leo hii nitawatia mikononi mwako, nawe utatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.’” Naye Ahabu akauliza, “Kwa msaada wa nani?” Nabii akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa msaada wa vijana wanaotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya.’” Naye mfalme akauliza, “Ni nani atakayeanza kupigana?” Nabii akajibu, “Wewe!” Basi, mfalme Ahabu akakagua vijana waliotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya, jumla yao watu 232. Kisha akakagua jeshi la Israeli, wanajeshi 7,000. Basi, mnamo adhuhuri, wakati Ben-hadadi na wale wafalme wenzake thelathini na wawili waliomwunga mkono walipokuwa mahemani mwao wakinywa na kulewa, mashambulizi yakaanza. Wale vijana waliotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya, wakatangulia. Wakati huo, Ben-hadadi alikuwa amekwisha peleka askari wa doria, nao wakampa habari kwamba kulikuwa na kundi la watu waliokuja kutoka Samaria. Ben-hadadi akawaambia, “Wakamateni wakiwa hai. Hata kama wanakuja kwa vita au kwa amani.” Basi, wale vijana waliotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya, wakaongoza mashambulizi, huku, nyuma yao, wanafuata wanajeshi wa Israeli. Kila mmoja wao akamuua adui mmoja. Watu wa Aramu wakatimua mbio, nao askari wa Israeli wakawafuatilia; lakini Ben-hadadi, mfalme wa Aramu, akiwa amepanda farasi, akatoroka na baadhi ya askari wapandafarasi. Basi, mfalme wa Israeli akashinda vita, akateka farasi na magari ya kukokotwa mengi, na kuwaua watu wa Aramu kwa wingi. Kisha, yule nabii akamwendea mfalme wa Israeli, akamwambia, “Jiandae upya ufikirie vizuri la kufanya. Mwakani, mfalme wa Aramu atakuja kupambana nawe tena.”
1 Wafalme 20:12-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, Ben-hadadi alipolisikia neno hilo, naye alikuwa akinywa, yeye na wafalme, mabandani, aliwaambia watumwa wake, Jipangeni. Wakajipanga juu ya mji. Na tazama, nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli, akasema, BWANA asema hivi, Je! Umeona makutano haya yote walio wengi? Angalia, nitawatia leo mkononi mwako; nawe utajua ya kuwa ndimi BWANA. Ahabu akanena, Kwa nani? Akasema, BWANA asema hivi, Kwa vijana wa maliwali wa majimbo. Ndipo akanena, Ni nani atakayepanga vita? Naye akajibu, Ni wewe. Ndipo akawaandika vijana wa maliwali wa majimbo, nao walikuwa mia mbili thelathini na wawili; kisha baada ya hao akawaandika watu wote, wana wa Israeli wote, nao walikuwa elfu saba. Wakatoka wakati wa adhuhuri. Lakini Ben-hadadi alikuwa akinywa hata kulewa mabandani, yeye na wale wafalme thelathini na wawili waliomsaidia. Wakatoka wale vijana wa maliwali wa majimbo wakitangulia; na Ben-hadadi akatuma watu, nao wakamwambia, Wako watu wametoka katika Samaria. Akasema, Kwamba wametoka kwa amani, wakamateni wa hai; au kwamba wametoka kwa vita, wakamateni wa hai. Basi wakatoka mjini hao vijana wa maliwali wa majimbo, na jeshi nyuma yao. Wakapiga kila mmoja mtu wake; Washami wakakimbia, na Israeli wakawafuatia; Ben-hadadi mfalme wa Shamu akaokoka amepanda farasi, pamoja na wapandao farasi. Mfalme wa Israeli akatoka, akawapiga farasi na magari, akawapiga Washami pigo kubwa. Naye yule nabii akamjia mfalme wa Israeli, akamwambia, Enenda, kusanya nguvu zako, ujue, na kuangalia ufanyavyo; kwa maana mwakani mfalme wa Shamu atakuja juu yako.
1 Wafalme 20:12-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ben-Hadadi alisikia ujumbe huu wakati ambapo yeye na wafalme walikuwa wanakunywa katika mahema yao, na akawaamuru watu wake, “Jiandaeni kushambulia.” Kwa hiyo wakajiandaa kuushambulia mji. Wakati ule ule nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo BWANA: ‘Je, unaona jeshi hili kubwa? Nitalitia mkononi mwako leo, nawe ndipo utajua kwamba mimi ndimi BWANA.’ ” Ahabu akauliza, “Ni nani atakayefanya hili?” Nabii akamjibu, “Hivi ndivyo asemavyo BWANA: ‘Maafisa vijana majemadari wa majimbo watafanya hili.’ ” Akauliza, “Ni nani atakayeanzisha vita?” Nabii akamjibu, “Ni wewe.” Kwa hiyo Ahabu akawaita maafisa vijana majemadari wa majimbo, wanaume 232. Kisha akawakusanya Waisraeli wote waliobaki, jumla yao 7,000. Wakaondoka wakati wa adhuhuri, Ben-Hadadi na wale wafalme thelathini na wawili walioungana naye walipokuwa katika mahema yao wakilewa. Maafisa vijana majemadari wa majimbo waliondoka kwanza. Wakati huu Ben-Hadadi alikuwa amewatuma wapelelezi, ambao walileta taarifa kusema kwamba, “Askari wanasonga mbele kutoka Samaria.” Akasema, “Ikiwa wamekuja kwa amani, wakamate wakiwa hai; ikiwa wamekuja kwa vita, wakamate wakiwa hai.” Wale maafisa vijana majemadari wa majimbo wakatoka nje ya mji jeshi likiwa nyuma yao, kila mmoja akamuua adui yake. Hii ilisababisha Waaramu kukimbia, huku Waisraeli wakiwafuatia. Lakini Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akatoroka akiwa amepanda farasi wake pamoja na baadhi ya wapanda farasi wake. Mfalme wa Israeli akasonga mbele na kushinda farasi na magari ya vita na kusababisha hasara kubwa kwa Waaramu. Baadaye nabii akaja kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Jiandae vizuri ufikirie la kufanya, kwa sababu mwakani mfalme wa Aramu atakuja kukushambulia tena.”