Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 20:1-11

1 Wafalme 20:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya jeshi lake lote; nao walikuwapo wafalme thelathini na wawili pamoja naye, na farasi, na magari: akakwea akauhusuru Samaria, akaupiga vita. Akatuma wajumbe kwa Ahabu mfalme wa Israeli, mjini, akamwambia, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi. Fedha yako na dhahabu yako ni zangu mimi; na wakezo na wanao, walio wema, ni wangu. Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Ni kama ulivyosema, bwana wangu, mfalme; mimi ni wako, na vyote nilivyo navyo. Wajumbe wakarudi tena, wakasema, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi, Hakika nimetuma kwako kusema, Fedha yako, na dhahabu yako, na wake zako, na wanao, utanitolea mimi; lakini kesho kama wakati huu nitatuma kwako watumwa wangu, ili watazame-tazame nyumba yako na nyumba za watumwa wako; na itakuwa kila kipendezacho machoni pako watakitia mikononi mwao, na kukichukua. Ndipo mfalme wa Israeli, akawaita wazee wote wa nchi, akasema, Angalieni, nawaomba, mwone, kwamba huyu ataka madhara; maana ametuma kwangu kutaka wake zangu na watoto wangu; na fedha yangu na dhahabu yangu, sikumkatalia. Wakamwambia wazee wote na watu wote, Usisikie, wala usikubali. Kwa hiyo akawaambia wale wajumbe wa Ben-hadadi, Mwambieni bwana wangu mfalme, Kila uliyotuma kumtakia mtumwa wako kwanza, nitafanya, ila neno hili siwezi kulifanya. Basi wajumbe wakaenda zao, wakamrudishia maneno hayo. Ndipo Ben-hadadi akatuma kwake, akasema, Miungu wanifanyie hivi na kuzidi, yakiwa mavumbi ya Samaria yatatosha makonzi ya watu wote walio miguuni pangu. Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Mwambieni, Avaaye asijisifu kama avuaye.

1 Wafalme 20:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Ben-hadadi mfalme wa Aramu, alikusanya jeshi lake lote; aliungwa mkono na wafalme wengine thelathini na wawili pamoja na farasi na magari yao ya kukokotwa. Aliuendea mji wa Samaria akauzingira na kuushambulia. Kisha, akatuma wajumbe wake mjini kwa mfalme Ahabu wa Israeli, wakamwambia, “Mfalme Ben-hadadi asema hivi: ‘Fedha na dhahabu yako yote ni mali yangu; wake zako warembo na watoto wako pia ni wangu.’” Naye mfalme wa Israeli akajibu, “Bwana wangu mfalme, ulivyosema ni sawa: Mimi ni wako, na vyote nilivyo navyo ni vyako.” Baadaye, wajumbe hao wakamrudia tena Ahabu, wakamwambia, “Mfalme Ben-hadadi asema hivi: ‘Nilikutumia ujumbe unipe dhahabu, fedha, wake zako pamoja na watoto wako. Sasa, kesho wakati kama huu, nitatuma watumishi wangu waje kuisaka ikulu na nyumba za watumishi wako, wachukue kila kitu unachothamini.’” Ndipo Ahabu mfalme wa Israeli, akawaita viongozi wote wa nchi, akawaambia, “Sasa, oneni jinsi jamaa huyu anavyotaka kututaabisha! Ametuma ujumbe kwamba anataka wake zangu, watoto wangu, dhahabu na fedha yangu. Nami sikumkatalia!” Wazee na watu wote wakamwambia, “Usimjali wala usikubali.” Basi, Ahabu akawaambia wajumbe wa Ben-hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme hivi: ‘Niko radhi kutimiza matakwa yako ya kwanza, lakini haya ya pili sikubali hata kidogo.’” Hapo, wajumbe hao wakaenda zao na kumhabarisha tena mfalme Ben-hadadi. Ben-hadadi akamtumia Ahabu ujumbe huu: “Miungu na waniulie mbali, nakuapia, ikiwa huko Samaria kutabakia mavumbi ya kutosha gao moja kwa kila mmoja wa watu wangu wengi!” Mfalme Ahabu wa Israeli akajibu, “Mwambieni mfalme Ben-hadadi kwamba shujaa hujisifu baada ya vita, si kabla!”

1 Wafalme 20:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi, Ben-hadadi mfalme wa Aramu akakusanya jeshi lake lote; nao walikuwapo wafalme thelathini na wawili pamoja naye, na farasi, na magari: akakwea akauhusuru Samaria, akaupiga vita. Akatuma wajumbe kwa Ahabu mfalme wa Israeli, mjini, akamwambia, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi. Fedha yako na dhahabu yako ni zangu mimi; na wakezo na wanao, walio wema, ni wangu. Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Ni kama ulivyosema, bwana wangu, mfalme; mimi ni wako, na vyote nilivyo navyo. Wajumbe wakarudi tena, wakasema, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi, Hakika nimetuma kwako kusema, Fedha yako, na dhahabu yako, na wake zako, na wanao, utanitolea mimi; lakini kesho kama wakati huu nitatuma kwako watumwa wangu, ili wachunguze nyumba yako na nyumba za watumwa wako; na itakuwa kila kipendezacho machoni pako watakitia mikononi mwao, na kukichukua. Ndipo mfalme wa Israeli, akawaita wazee wote wa nchi, akasema, Angalieni, nawaomba, mwone, kwamba huyu ataka madhara; maana ametuma kwangu kutaka wake zangu na watoto wangu; na fedha yangu na dhahabu yangu, sikumkatalia. Wakamwambia wazee wote na watu wote, Usisikie, wala usikubali. Kwa hiyo akawaambia wale wajumbe wa Ben-hadadi, Mwambieni bwana wangu mfalme, Kila uliyotuma kumtakia mtumwa wako kwanza, nitafanya, ila neno hili siwezi kulifanya. Basi wajumbe wakaenda zao, wakamrudishia maneno hayo. Ndipo Ben-hadadi akatuma kwake, akasema, Miungu wanifanyie hivi na kuzidi, yakiwa mavumbi ya Samaria yatatosha makonzi ya watu wote walio miguuni pangu. Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Mwambieni, Avaaye asijisifu kama avuaye.

1 Wafalme 20:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati huu, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akakusanya jeshi lake lote. Akifuatana na wafalme thelathini na wawili wakiwa na farasi na magari ya vita, akakwea kuuzingira kwa jeshi Samaria na kuishambulia. Akawatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Fedha yako na dhahabu ni yangu, nao wake zako walio wazuri sana na watoto ni wangu.’ ” Mfalme wa Israeli akajibu, “Iwe kama usemavyo, bwana wangu mfalme. Mimi na vyote nilivyo navyo ni mali yako.” Wale wajumbe wakaja tena na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Nimetuma kutaka fedha yako na dhahabu, wake zako na watoto wako. Lakini kesho wakati kama huu, nitawatuma maafisa wangu kukagua jumba lako la kifalme na nyumba za maafisa wako. Watatwaa kitu unachokithamini nao watakichukua.’ ” Mfalme wa Israeli akawaita wazee wote wa nchi na akawaambia, “Tazama jinsi mtu huyu anavyochokoza! Wakati alipotuma apelekewe wake zangu na watoto wangu, fedha zangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.” Wazee na watu wote wakajibu, “Usimsikilize, wala usiyakubali matakwa yake.” Kwa hiyo akawajibu wajumbe wa Ben-Hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme, ‘Mtumishi wako atafanya yote uliyoyadai mwanzoni, lakini dai hili la sasa siwezi kulitekeleza.’ ” Wakaondoka na kupeleka jibu kwa Ben-Hadadi. Kisha Ben-Hadadi akatuma ujumbe mwingine kwa Ahabu, kusema “Miungu iniletee maafa, tena makubwa zaidi, ikiwa vumbi la Samaria litatosheleza konzi moja ya kila mtu ya wale wafuatanao nami.” Mfalme wa Israeli akajibu, “Mwambieni, ‘Yule anayevaa mavazi ya vita asije akajisifu kama yule anayevua.’ ”