Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 2:26-35

1 Wafalme 2:26-35 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Solomoni akamwambia kuhani Abiathari, “Ondoka uende shambani kwako, huko Anathothi; unastahili kufa wewe! Lakini sasa, sitakuua kwa sababu ulilishughulikia sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu ulipokuwa na baba yangu Daudi, ukateswa pamoja naye.” Basi, mfalme Solomoni akamfukuza Abiathari, asiwe kuhani wa Mwenyezi-Mungu; hivyo likatimia neno alilosema Mwenyezi-Mungu huko Shilo, juu ya Eli na ukoo wake. Yoabu alipopata habari, alikimbilia hemani mwa Mungu na kushikilia pembe za madhabahu; kwa maana alikuwa amemwunga mkono Adoniya na si Absalomu. Mfalme Solomoni aliposikia kwamba Yoabu yumo katika hema la Mungu na kwamba amesimama madhabahuni, alimtuma Benaya mwana wa Yehoyada, akisema, “Nenda ukampige.” Basi, Benaya akaenda katika hema la Mungu, akamwambia Yoabu, “Mfalme ameamuru utoke nje.” Yoabu akajibu, “Mimi sitoki; nitakufa papa hapa.” Benaya akarudi kwa mfalme na kumweleza alivyojibu Yoabu. Solomoni akasema, “Fanya alivyosema; umuue na kumzika. Hivyo, mimi na wazawa wengine wote wa Daudi hatutalaumiwa kwa vitendo vya Yoabu vya kuwaua watu wasio na hatia. Mungu atamwadhibu Yoabu kwa mauaji hayo aliyoyafanya bila baba yangu kuwa na habari. Yeye aliwaua watu wawili ambao walikuwa wa maana zaidi kuliko yeye, pia walimzidi kwa wema; aliwaua Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda. Adhabu ya mauaji hayo itakuwa juu ya Yoabu na wazawa wake milele. Bali Mwenyezi-Mungu atawapa ufanisi daima, Daudi na wazawa wake watakaokalia kiti chake cha enzi.” Basi, Benaya mwana wa Yehoyada, akaenda hemani, akamuua Yoabu ambaye alizikwa shambani mwake, nyikani. Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada, kuwa jemadari wa jeshi mahali pa Yoabu, na Sadoki akawa kuhani mahali pa Abiathari.

1 Wafalme 2:26-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tena, mfalme akamwambia Abiathari kuhani, Nenda Anathothi mashambani kwako; kwa kuwa wastahili kufa; ila leo sikuui, kwa sababu wewe ulichukua sanduku la Bwana mbele ya Daudi baba yangu, na kwa sababu wewe uliteswa kwa mateso yote ya baba yangu. Hivyo Sulemani akamtoa Abiathari asiwe kuhani wa BWANA; ili alitimize neno la BWANA, alilonena juu ya nyumba ya Eli katika Shilo. Tena, habari zikamfikia Yoabu; kwa maana Yoabu alikuwa amemfuata Adonia, ingawa hakumfuata Absalomu. Yoabu akakimbilia Hemani kwa BWANA, akazishika pembe za madhabahu. Akaambiwa mfalme Sulemani ya kwamba, Yoabu amekimbilia Hemani kwa BWANA, naye, tazama, yuko madhabahuni. Ndipo Sulemani akamtuma Benaya, mwana wa Yehoyada, akisema, Nenda, umuue. Basi Benaya akaja Hemani kwa BWANA, akamwambia, Mfalme asema hivi, Njoo utoke. Naye akajibu, La, sivyo; ila nitakufa papa hapa. Naye Benaya akamletea mfalme habari, akisema, Hivi ndivyo alivyonena Yoabu, na ndivyo alivyonijibu. Mfalme akamwambia, Fanya alivyonena, umpige, ukamzike; ili uniondolee mimi na nyumba ya babangu damu aliyoimwaga Yoabu bure. Naye BWANA atamrudishia damu yake kichwani pake mwenyewe, kwa kuwa aliwapiga watu wawili wenye haki, na wema kuliko yeye, akawaua kwa upanga, wala babangu Daudi hakujua habari hiyo; yaani Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa, mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda. Hivyo damu yao itarudi kichwani pa Yoabu, na kichwani pa wazao wake hata milele; ila kwa Daudi, na kwa wazao wake, na kwa nyumba yake, na kwa kiti chake cha enzi, kutakuwa na amani hata milele kutoka kwa BWANA. Ndipo Benaya, mwana wa Yehoyada, akapanda, akampiga, akamwua; naye akazikwa katika nyumba yake mwenyewe iliyoko nyikani. Kisha mfalme akamweka Benaya, mwana wa Yehoyada, mahali pake juu ya jeshi; na Sadoki, kuhani, mfalme akamweka mahali pa Abiathari.

1 Wafalme 2:26-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tena, mfalme akamwambia Abiathari kuhani, Enenda Anathothi mashambani kwako; kwa kuwa wastahili kufa; ila leo sikuui, kwa sababu wewe ulichukua sanduku la Bwana mbele ya Daudi baba yangu, na kwa sababu wewe uliteswa kwa mateso yote ya baba yangu. Hivyo Sulemani akamtoa Abiathari asiwe kuhani wa BWANA; ili alitimize neno la BWANA, alilonena juu ya nyumba ya Eli katika Shilo. Tena, habari zikamfikia Yoabu; kwa maana Yoabu alikuwa amemfuata Adonia, ingawa hakumfuata Absalomu. Yoabu akakimbilia Hemani kwa BWANA, akazishika pembe za madhabahu. Akaambiwa mfalme Sulemani ya kwamba, Yoabu amekimbilia Hemani kwa BWANA, naye, tazama, yuko madhabahuni. Ndipo Sulemani akamtuma Benaya, mwana wa Yehoyada, akisema, Enenda, umpige. Basi Benaya akaja Hemani kwa BWANA, akamwambia, Mfalme asema hivi, Njoo utoke. Naye akajibu, La, sivyo; ila nitakufa papa hapa. Naye Benaya akamletea mfalme habari, akisema, Hivi ndivyo alivyonena Yoabu, na ndivyo alivyonijibu. Mfalme akamwambia, Fanya alivyonena, umpige, ukamzike; ili uniondolee mimi na nyumba ya babangu damu aliyoimwaga Yoabu bure. Naye BWANA atamrudishia damu yake kichwani pake mwenyewe, kwa kuwa aliwapiga watu wawili wenye haki, na wema kuliko yeye, akawaua kwa upanga, wala babangu Daudi hakujua habari hiyo; yaani Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa, mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda. Hivyo damu yao itarudi kichwani pa Yoabu, na kichwani pa wazao wake hata milele; ila kwa Daudi, na kwa wazao wake, na kwa nyumba yake, na kwa kiti chake cha enzi, kutakuwa na amani hata milele kutoka kwa BWANA. Ndipo Benaya, mwana wa Yehoyada, akapanda, akampiga, akamwua; naye akazikwa katika nyumba yake mwenyewe iliyoko nyikani. Kisha mfalme akamweka Benaya, mwana wa Yehoyada, mahali pake juu ya jeshi; na Sadoki, kuhani, mfalme akamweka mahali pa Abiathari.

1 Wafalme 2:26-35 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mfalme akamwambia kuhani Abiathari, “Nenda huko Anathothi katika mashamba yako. Wewe unastahili kufa, lakini sitakuua sasa, kwa sababu ulilichukua Sanduku la BWANA Mwenyezi mbele ya Daudi baba yangu na ulishiriki taabu zote za baba yangu.” Hivyo Solomoni akamwondoa Abiathari kwenye ukuhani wa BWANA, akilitimiza neno la BWANA alilokuwa amenena huko Shilo kuhusu nyumba ya Eli. Habari zilipomfikia Yoabu, ambaye alikuwa amefanya shauri baya na Adoniya, lakini sio na Absalomu, alikimbilia kwenye hema la BWANA na kushika pembe za madhabahu. Mfalme Solomoni akaambiwa kuwa Yoabu amekimbilia kwenye hema la BWANA naye alikuwa kando ya madhabahu. Basi Solomoni akamwagiza Benaya mwana wa Yehoyada: “Nenda ukamuue!” Ndipo Benaya akaingia kwenye hema la BWANA na kumwambia Yoabu, “Mfalme anasema, ‘Toka nje!’ ” Lakini akajibu, “La! Nitafia hapa hapa.” Benaya akamwarifu mfalme, “Hivi ndivyo Yoabu alivyonijibu.” Kisha mfalme akamwamuru Benaya, “Fanya kama asemavyo. Muue na kumzika, ili uniondolee mimi na nyumba ya baba yangu dhambi ya damu isiyokuwa na hatia ile Yoabu aliyoimwaga. BWANA atamlipiza kwa ajili ya damu aliyoimwaga, kwa sababu pasipo Daudi baba yangu kujua, aliwashambulia watu wawili na kuwaua kwa upanga. Wote wawili, Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda, walikuwa watu wazuri na wanyofu kuliko yeye. Hatia ya damu yao na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na wazao wake milele. Lakini kwa Daudi na uzao wake, nyumba yake na kiti chake cha ufalme, iwepo amani ya BWANA milele.” Basi Benaya mwana wa Yehoyada akakwea, akampiga na kumuua Yoabu, naye akazikwa katika nchi yake mwenyewe katika jangwa. Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada juu ya jeshi kwenye nafasi ya Yoabu na kumweka kuhani Sadoki badala ya Abiathari.