Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 2:1-46

1 Wafalme 2:1-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujioneshe kuwa shujaa na hodari; uyashike mausia ya BWANA, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako; ili BWANA afanye imara neno lake alilonena kuhusu habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli. Na zaidi ya hayo, unajua alivyonitenda Yoabu, mwana wa Seruya, yaani, alivyowatenda majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri, mwana wa Neri, na Amasa, mwana wa Yetheri, ambao aliwaua, na kumwaga damu wakati wa amani akilipiza kisasi cha vita, mshipi akautia damu ya vita uliokuwa viunoni mwake, na viatu vilivyokuwa miguuni mwake. Kwa hiyo ufanye kama ilivyo hekima yako, wala usimwachie mvi zake kushukia Ahera kwa amani. Lakini uwafanyie mema wana wa Barzilai Mgileadi, wawe miongoni mwao walao mezani pako; kwa jinsi walivyonijilia nilipokuwa nimekimbia mbele ya Absalomu, ndugu yako. Hata, angalia, yuko pamoja nawe Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu, ndiye aliyenilaani kwa laana kuu siku ile nilipokwenda Mahanaimu; lakini akashuka kunilaki kule Yordani, nami nikamwapia kwa BWANA, nikamwambia, Mimi sitakuua kwa upanga. Basi kwa hiyo usimwachilie, kwa kuwa wewe u mtu wa akili; nawe utajua ikupasayo umtendee, na mvi zake utazishusha Ahera pamoja na damu. Basi Daudi akalala na babaze, akazikwa mjini mwa Daudi. Na siku alizotawala Daudi juu ya Israeli zilikuwa miaka arubaini; huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu. Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa imara sana. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akaja kwa Bathsheba mamaye Sulemani. Naye akasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akajibu, Kwa amani. Tena akasema, Nina jambo ninalotaka kukuambia. Naye akamwambia, Sema. Basi akasema, Wajua ya kwamba ufalme ulikuwa wangu, na Israeli wote wakaniwekea nyuso zao ili mimi nimiliki; lakini sasa ufalme umegeuka kuwa wake ndugu yangu; kwa maana ulikuwa wake kutoka kwa BWANA. Basi sasa nina haja moja ninayokuomba, usinikataze hiyo. Naye akamwambia, Sema. Akasema, Nakusihi nena na Sulemani, mfalme (kwa kuwa hawezi kukukatalia neno), kwamba anioze Abishagi, Mshunami. Naye Bathsheba akasema, Vema; nitasema na mfalme kwa ajili yako. Basi Bathsheba akaingia kwa mfalme Sulemani, aseme naye kwa ajili ya Adonia. Naye mfalme akainuka kwenda kumlaki, akamwinamia, akaketi katika kiti chake cha enzi; kisha akaagiza awekewe kiti cha enzi mamaye mfalme; naye akaketi mkono wake wa kulia. Ndipo akasema, Haja moja ndogo nakuomba; usinikatalie. Mfalme akamwambia, Omba, mama; kwa kuwa siwezi kukukatalia neno. Naye akasema, Nataka Adonia, ndugu yako, aozwe Abishagi, Mshunami. Mfalme Sulemani akajibu, akamwambia mamaye, Na mbona wamtakia Adonia Abishagi, Mshunami? Umtakie na ufalme pia; kwa kuwa yeye ni ndugu yangu mkubwa; naam, umtakie yeye, na Abiathari kuhani, na Yoabu mwana wa Seruya. Ndipo mfalme Sulemani akaapa kwa BWANA, akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, isipokuwa Adonia amenena neno hili juu ya uhai wake mwenyewe. Basi kwa hiyo, BWANA aishivyo, aliyenithibitisha na kunikalisha katika kiti cha enzi cha Daudi baba yangu, akanifanyia nyumba, kama alivyoahidi, hakika atauawa leo hivi Adonia. Mfalme Sulemani akatuma kuwa jambo hilo liwe mkononi mwa Benaya mwana wa Yehoyada: naye akampiga, hata akafa. Tena, mfalme akamwambia Abiathari kuhani, Nenda Anathothi mashambani kwako; kwa kuwa wastahili kufa; ila leo sikuui, kwa sababu wewe ulichukua sanduku la Bwana mbele ya Daudi baba yangu, na kwa sababu wewe uliteswa kwa mateso yote ya baba yangu. Hivyo Sulemani akamtoa Abiathari asiwe kuhani wa BWANA; ili alitimize neno la BWANA, alilonena juu ya nyumba ya Eli katika Shilo. Tena, habari zikamfikia Yoabu; kwa maana Yoabu alikuwa amemfuata Adonia, ingawa hakumfuata Absalomu. Yoabu akakimbilia Hemani kwa BWANA, akazishika pembe za madhabahu. Akaambiwa mfalme Sulemani ya kwamba, Yoabu amekimbilia Hemani kwa BWANA, naye, tazama, yuko madhabahuni. Ndipo Sulemani akamtuma Benaya, mwana wa Yehoyada, akisema, Nenda, umuue. Basi Benaya akaja Hemani kwa BWANA, akamwambia, Mfalme asema hivi, Njoo utoke. Naye akajibu, La, sivyo; ila nitakufa papa hapa. Naye Benaya akamletea mfalme habari, akisema, Hivi ndivyo alivyonena Yoabu, na ndivyo alivyonijibu. Mfalme akamwambia, Fanya alivyonena, umpige, ukamzike; ili uniondolee mimi na nyumba ya babangu damu aliyoimwaga Yoabu bure. Naye BWANA atamrudishia damu yake kichwani pake mwenyewe, kwa kuwa aliwapiga watu wawili wenye haki, na wema kuliko yeye, akawaua kwa upanga, wala babangu Daudi hakujua habari hiyo; yaani Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa, mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda. Hivyo damu yao itarudi kichwani pa Yoabu, na kichwani pa wazao wake hata milele; ila kwa Daudi, na kwa wazao wake, na kwa nyumba yake, na kwa kiti chake cha enzi, kutakuwa na amani hata milele kutoka kwa BWANA. Ndipo Benaya, mwana wa Yehoyada, akapanda, akampiga, akamwua; naye akazikwa katika nyumba yake mwenyewe iliyoko nyikani. Kisha mfalme akamweka Benaya, mwana wa Yehoyada, mahali pake juu ya jeshi; na Sadoki, kuhani, mfalme akamweka mahali pa Abiathari. Tena, mfalme akatuma watu akamwita Shimei, akamwambia, Ujijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae ndani yake, wala usitoke humo kwenda mahali popote. Kwa kuwa siku ile ya kutoka kwako, na kuvuka kijito Kidroni, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe. Naye Shimei akamwambia mfalme, Neno hili ni jema; kama alivyosema bwana wangu mfalme, ndivyo atakavyofanya mtumwa wako. Basi Shimei akakaa Yerusalemu siku nyingi. Ikawa miaka mitatu ilipokwisha, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi, mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Wakamwambia Shimei, wakasema, Angalia, watumwa wako wako huko Gathi. Shimei akaondoka, akatandika punda wake, akaenda Gathi kwa Akishi, ili kuwatafuta watumwa wake. Akaenda Shimei, akawaleta watumwa wake toka Gathi. Naye Sulemani akaambiwa, ya kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu kwenda Gathi, na kurudi tena. Basi, mfalme akatuma watu, akamwita Shimei, akamwambia, Je! Sikukuapisha kwa BWANA, na kukushuhudia, kusema, Siku ile utakapotoka ukaenda mahali popote, ujue kwamba hakika utakufa? Nawe ukaniambia, Neno hili nililolisikia ni jema? Mbona basi hukukishika kiapo chako kwa BWANA, na amri niliyokuagiza? Tena, mfalme akamwambia Shimei, Umejua uovu wote uliouona moyoni mwako, uliomtenda Daudi baba yangu; basi kwa hiyo BWANA atakurudishia uovu wako kichwani pako mwenyewe. Ila mfalme Sulemani atakuwa amebarikiwa, na kiti cha enzi cha Daudi kitathibitika mbele za BWANA hata milele. Basi mfalme akamwamuru Benaya, mwana wa Yehoyada; naye akatoka, akampiga, hata akafa. Nao ufalme ukawa imara mkononi mwa Sulemani.

1 Wafalme 2:1-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya BWANA, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako; ili BWANA afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli. Na zaidi ya hayo, umejua alivyonitenda Yoabu, mwana wa Seruya, yaani, alivyowatenda majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri, mwana wa Neri, na Amasa, mwana wa Yetheri, ambao aliwaua, na kuimwaga damu ya vita wakati wa amani, akautia damu ya vita mshipi uliokuwa viunoni mwake, na viatu vilivyokuwa miguuni mwake. Kwa hiyo ufanye kama ilivyo hekima yako, wala usimwachie mvi zake kushukia Ahera kwa amani. Lakini uwafanyie mema wana wa Barzilai Mgileadi, wawe miongoni mwao walao mezani pako; kwa jinsi walivyonijilia nilipokuwa nimekimbia mbele ya Absalomu, ndugu yako. Hata, angalia, yuko pamoja nawe Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu, ndiye aliyenilaani kwa laana kuu siku ile nilipokwenda Mahanaimu; lakini akashuka kunilaki kule Yordani, nami nikamwapia kwa BWANA, nikamwambia, Mimi sitakuua kwa upanga. Basi kwa hiyo usimwachilie, kwa kuwa wewe u mtu wa akili; nawe utajua ikupasayo umtendee, na mvi zake utazishusha Ahera pamoja na damu. Basi Daudi akalala na babaze, akazikwa mjini mwa Daudi. Na siku alizotawala Daudi juu ya Israeli zilikuwa miaka arobaini; huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu. Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa imara sana. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akaja kwa Bath-sheba mamaye Sulemani. Naye akasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akajibu, Kwa amani. Tena akasema, Nina shauri ninalotaka kukuambia. Naye akamwambia, Sema. Basi akasema, Wajua ya kwamba ufalme ulikuwa wangu, na Israeli wote wakaniwekea nyuso zao ili nimiliki mimi; walakini sasa ufalme umegeuka kuwa wake ndugu yangu; kwa maana ulikuwa wake kutoka kwa BWANA. Basi sasa nina haja moja ninayokuomba, usinikataze hiyo. Naye akamwambia, Sema. Akasema, Nena, nakusihi, na Sulemani, mfalme, (kwa kuwa hawezi kukukataza neno), kwamba anioze Abishagi, Mshunami. Naye Bath-sheba akasema, Vema; nitasema na mfalme kwa ajili yako. Basi Bath-sheba akaingia kwa mfalme Sulemani, aseme naye kwa ajili ya Adonia. Naye mfalme akainuka kwenda kumlaki, akamwinamia, akaketi katika kiti chake cha enzi; kisha akaagiza awekewe kiti cha enzi mamaye mfalme; naye akaketi mkono wake wa kuume. Ndipo akasema, Haja moja ndogo nakuomba; usinikataze. Mfalme akamwambia, Omba, mama; kwa kuwa siwezi kukukataza neno. Naye akasema, Nataka Adonia, ndugu yako, aozwe Abishagi, Mshunami. Akajibu mfalme Sulemani akamwambia mamaye, Na mbona wamtakia Adonia Abishagi, Mshunami? Umtakie na ufalme pia; kwa kuwa yeye ni ndugu yangu mkubwa; naam, umtakie yeye, na Abiathari kuhani, na Yoabu mwana wa Seruya. Ndipo mfalme Sulemani akaapa kwa BWANA, akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, isipokuwa Adonia amenena neno hili juu ya uhai wake mwenyewe. Basi kwa hiyo, BWANA aishivyo, aliyenithibitisha na kunikalisha katika kiti cha enzi cha Daudi baba yangu, akanifanyia nyumba, kama alivyoahidi, hakika atauawa leo hivi Adonia. Mfalme Sulemani akatuma kwa mkono wa Benaya mwana wa Yehoyada: naye akampiga, hata akafa. Tena, mfalme akamwambia Abiathari kuhani, Enenda Anathothi mashambani kwako; kwa kuwa wastahili kufa; ila leo sikuui, kwa sababu wewe ulichukua sanduku la Bwana mbele ya Daudi baba yangu, na kwa sababu wewe uliteswa kwa mateso yote ya baba yangu. Hivyo Sulemani akamtoa Abiathari asiwe kuhani wa BWANA; ili alitimize neno la BWANA, alilonena juu ya nyumba ya Eli katika Shilo. Tena, habari zikamfikia Yoabu; kwa maana Yoabu alikuwa amemfuata Adonia, ingawa hakumfuata Absalomu. Yoabu akakimbilia Hemani kwa BWANA, akazishika pembe za madhabahu. Akaambiwa mfalme Sulemani ya kwamba, Yoabu amekimbilia Hemani kwa BWANA, naye, tazama, yuko madhabahuni. Ndipo Sulemani akamtuma Benaya, mwana wa Yehoyada, akisema, Enenda, umpige. Basi Benaya akaja Hemani kwa BWANA, akamwambia, Mfalme asema hivi, Njoo utoke. Naye akajibu, La, sivyo; ila nitakufa papa hapa. Naye Benaya akamletea mfalme habari, akisema, Hivi ndivyo alivyonena Yoabu, na ndivyo alivyonijibu. Mfalme akamwambia, Fanya alivyonena, umpige, ukamzike; ili uniondolee mimi na nyumba ya babangu damu aliyoimwaga Yoabu bure. Naye BWANA atamrudishia damu yake kichwani pake mwenyewe, kwa kuwa aliwapiga watu wawili wenye haki, na wema kuliko yeye, akawaua kwa upanga, wala babangu Daudi hakujua habari hiyo; yaani Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa, mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda. Hivyo damu yao itarudi kichwani pa Yoabu, na kichwani pa wazao wake hata milele; ila kwa Daudi, na kwa wazao wake, na kwa nyumba yake, na kwa kiti chake cha enzi, kutakuwa na amani hata milele kutoka kwa BWANA. Ndipo Benaya, mwana wa Yehoyada, akapanda, akampiga, akamwua; naye akazikwa katika nyumba yake mwenyewe iliyoko nyikani. Kisha mfalme akamweka Benaya, mwana wa Yehoyada, mahali pake juu ya jeshi; na Sadoki, kuhani, mfalme akamweka mahali pa Abiathari. Tena, mfalme akatuma watu akamwita Shimei, akamwambia, Ujijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae ndani yake, wala usitoke humo kwenda mahali po pote. Kwa kuwa siku ile ya kutoka kwako, na kuvuka kijito Kidroni, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe. Naye Shimei akamwambia mfalme, Neno hili ni jema; kama alivyosema bwana wangu mfalme, ndivyo atakavyofanya mtumwa wako. Basi Shimei akakaa Yerusalemu siku nyingi. Ikawa miaka mitatu ilipokwisha, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi, mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Wakamwambia Shimei, wakasema, Angalia, watumwa wako wako huko Gathi. Shimei akaondoka, akatandika punda wake, akaenda Gathi kwa Akishi, ili kuwatafuta watumwa wake. Akaenda Shimei, akawaleta watumwa wake toka Gathi. Naye Sulemani akaambiwa, ya kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu kwenda Gathi, na kurudi tena. Basi, mfalme akatuma watu, akamwita Shimei, akamwambia, Je! Sikukuapisha kwa BWANA, na kukushuhudia, kusema, Siku ile ya kutoka kwako ukienda mahali po pote, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa? Nawe ukaniambia, Neno hili nililolisikia ni jema? Mbona basi hukukishika kiapo cha BWANA, na amri niliyokuagiza? Tena, mfalme akamwambia Shimei, Umejua uovu wote uliouona moyoni mwako, uliomtenda Daudi baba yangu; basi kwa hiyo BWANA atakurudishia uovu wako kichwani pako mwenyewe. Ila mfalme Sulemani atakuwa amebarikiwa, na kiti cha enzi cha Daudi kitathibitika mbele za BWANA hata milele. Basi mfalme akamwamuru Benaya, mwana wa Yehoyada; naye akatoka, akampiga, hata akafa. Nao ufalme ukawa imara mkononi mwa Sulemani.

1 Wafalme 2:1-46 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Solomoni agizo. Akasema, “Mimi ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jionyeshe kuwa mwanaume, shika lile BWANA Mungu wako analokuagiza: Enenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote uendako, ili kwamba BWANA aweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na kama wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’ “Sasa wewe mwenyewe unafahamu lile Yoabu mwana wa Seruya alilonitendea, lile alilofanya kwa majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua, akimwaga damu yao wakati wa amani kama vile ni kwenye vita, tena akaipaka damu ile kwenye mkanda uliokuwa kiunoni mwake na viatu alivyovaa miguuni mwake. Shughulika naye kwa kadiri ya hekima yako, lakini usiache kichwa chake chenye mvi kishukie kaburi kwa amani. “Lakini uwaonyeshe wema wana wa Barzilai wa Gileadi na uwaruhusu wawe miongoni mwa wale walao mezani pako. Walisimama nami nilipomkimbia ndugu yako Absalomu. “Ukumbuke, unaye Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini kutoka Bahurimu, ambaye alinilaani kwa laana kali siku niliyokwenda Mahanaimu. Aliposhuka kunilaki huko Yordani, nilimwapia kwa BWANA: ‘Sitakuua kwa upanga!’ Lakini sasa, usidhani kwamba hana hatia. Wewe ni mtu wa hekima, utajua la kumtendea. Zishushe mvi zake kaburini kwa damu.” Kisha Daudi akapumzika pamoja na baba zake naye akazikwa katika Mji wa Daudi. Daudi alikuwa ametawala juu ya Israeli miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu. Kwa hiyo Solomoni akaketi katika kiti cha ufalme cha baba yake Daudi, nao utawala wake ukaimarika sana. Basi Adoniya, mwana wa Hagithi, akaenda kwa Bathsheba, mama yake Solomoni. Bathsheba akamuuliza, “Je, umekuja kwa amani?” Akajibu, “Ndiyo, kwa amani.” Kisha akaongeza, “Ninalo jambo la kukuambia.” Akajibu, “Waweza kulisema.” Akasema, “Kama unavyojua, ufalme ulikuwa wangu. Israeli wote waliniangalia mimi kama mfalme wao. Lakini mambo yalibadilika, ufalme umekwenda kwa ndugu yangu, kwa maana umemjia kutoka kwa BWANA. Sasa ninalo ombi moja ninalokuomba. Usinikatalie.” Bathsheba akasema, “Waweza kuliomba.” Kwa hiyo akaendelea kusema, “Tafadhali mwombe Mfalme Solomoni, anipatie Abishagi, Mshunami, awe mke wangu; hatakukatalia wewe.” Bathsheba akamjibu, “Vema sana, nitazungumza na mfalme kwa ajili yako.” Bathsheba alipokwenda kwa Mfalme Solomoni kuzungumza naye kwa ajili ya Adoniya, mfalme alisimama kumlaki mama yake, akamwinamia na kuketi kwenye kiti chake cha ufalme. Akaamuru kiti cha ufalme kuletwa kwa ajili ya mama yake mfalme, naye akaketi mkono wake wa kuume. Bathsheba akamwambia mfalme, “Ninalo ombi moja dogo la kukuomba; usinikatalie.” Mfalme akajibu, “Omba, mama yangu; sitakukatalia.” Akasema, “Mruhusu Abishagi, Mshunami, aolewe na ndugu yako Adoniya.” Mfalme Solomoni akamjibu mama yake, “Kwa nini uombe Abishagi, Mshunami, kwa ajili ya Adoniya? Ungeweza pia kuomba ufalme kwa ajili yake, kwani yeye ni ndugu yangu mkubwa: naam, kwa ajili yake, na kwa kuhani Abiathari na Yoabu mwana wa Seruya!” Mfalme Solomoni akaapa kwa BWANA, akasema: “Mungu na aniulie mbali, tena bila huruma, ikiwa Adoniya hatalipa kwa uhai wake kwa ajili ya ombi hili! Basi sasa, hakika kama BWANA aishivyo, yeye ambaye ameniimarisha salama kwenye kiti cha ufalme cha Daudi baba yangu, naye amenipa ufalme wa kudumu kama alivyoahidi, Adoniya atauawa leo!” Hivyo Mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adoniya akafa. Mfalme akamwambia kuhani Abiathari, “Nenda huko Anathothi katika mashamba yako. Wewe unastahili kufa, lakini sitakuua sasa, kwa sababu ulilichukua Sanduku la BWANA Mwenyezi mbele ya Daudi baba yangu na ulishiriki taabu zote za baba yangu.” Hivyo Solomoni akamwondoa Abiathari kwenye ukuhani wa BWANA, akilitimiza neno la BWANA alilokuwa amenena huko Shilo kuhusu nyumba ya Eli. Habari zilipomfikia Yoabu, ambaye alikuwa amefanya shauri baya na Adoniya, lakini sio na Absalomu, alikimbilia kwenye hema la BWANA na kushika pembe za madhabahu. Mfalme Solomoni akaambiwa kuwa Yoabu amekimbilia kwenye hema la BWANA naye alikuwa kando ya madhabahu. Basi Solomoni akamwagiza Benaya mwana wa Yehoyada: “Nenda ukamuue!” Ndipo Benaya akaingia kwenye hema la BWANA na kumwambia Yoabu, “Mfalme anasema, ‘Toka nje!’ ” Lakini akajibu, “La! Nitafia hapa hapa.” Benaya akamwarifu mfalme, “Hivi ndivyo Yoabu alivyonijibu.” Kisha mfalme akamwamuru Benaya, “Fanya kama asemavyo. Muue na kumzika, ili uniondolee mimi na nyumba ya baba yangu dhambi ya damu isiyokuwa na hatia ile Yoabu aliyoimwaga. BWANA atamlipiza kwa ajili ya damu aliyoimwaga, kwa sababu pasipo Daudi baba yangu kujua, aliwashambulia watu wawili na kuwaua kwa upanga. Wote wawili, Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda, walikuwa watu wazuri na wanyofu kuliko yeye. Hatia ya damu yao na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na wazao wake milele. Lakini kwa Daudi na uzao wake, nyumba yake na kiti chake cha ufalme, iwepo amani ya BWANA milele.” Basi Benaya mwana wa Yehoyada akakwea, akampiga na kumuua Yoabu, naye akazikwa katika nchi yake mwenyewe katika jangwa. Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada juu ya jeshi kwenye nafasi ya Yoabu na kumweka kuhani Sadoki badala ya Abiathari. Kisha mfalme akatuma ujumbe kwa Shimei na kumwambia, “Ujijengee nyumba huko Yerusalemu uishi huko, lakini usiende mahali pengine popote. Siku utakayoondoka kuvuka Bonde la Kidroni, uwe na hakika utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.” Shimei akamjibu mfalme, “Ulilolisema ni jema. Mtumishi wako atatenda kama bwana wangu mfalme alivyosema.” Naye Shimei akakaa Yerusalemu kwa muda mrefu. Lakini baada ya miaka mitatu, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi, naye Shimei akaambiwa, “Watumwa wako wako Gathi.” Kwa ajili ya hili, Shimei akatandika punda wake, akaenda kwa Akishi huko Gathi kuwatafuta watumwa wake. Basi Shimei akaondoka na kuwarudisha watumwa wake kutoka Gathi. Solomoni alipoambiwa kuwa Shimei ametoka Yerusalemu na kwenda Gathi na amekwisha kurudi, mfalme akamwita Shimei na kumwambia, “Je, sikukuapiza kwa BWANA na kukuonya kuwa, ‘Siku utakayoondoka kwenda mahali pengine popote, uwe na hakika utakufa?’ Wakati ule uliniambia, ‘Ulilolisema ni jema. Nitatii!’ Kwa nini basi hukutunza kiapo chako kwa BWANA na kutii amri niliyokupa?” Pia mfalme akamwambia Shimei, “Unajua katika moyo wako makosa uliyomtendea baba yangu Daudi. Sasa BWANA atakulipiza kwa ajili ya mabaya yako uliyotenda. Lakini Mfalme Solomoni atabarikiwa, na kiti cha ufalme cha Daudi kitakuwa imara mbele za BWANA milele.” Kisha mfalme akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka nje, akampiga Shimei na kumuua. Sasa ufalme ukawa umeimarika kikamilifu mikononi mwa Solomoni.

1 Wafalme 2:1-46 Biblia Habari Njema (BHN)

Daudi alipokaribia kufariki, alimwita mwanawe Solomoni, akampa wosia akisema, “Mwanangu, kama ilivyo kawaida kwa viumbe vyote kufa, siku zangu zimekwisha. Uwe imara na hodari. Timiza maagizo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ufuate njia zake na kushika masharti yake, amri zake, hukumu zake na kuheshimu maamuzi yake kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, ili upate kufanikiwa katika kila ufanyalo na kokote uendako, pia ili Mwenyezi-Mungu atimize ahadi yake aliyotoa aliponiambia kuwa, ikiwa wazawa wangu watatii amri zake na kumtumikia kwa uaminifu na kwa moyo wote, hakutakosekana mmoja wao kutawala Israeli nyakati zote. “Zaidi ya hayo, unajua pia yale aliyonitendea Yoabu, mwana wa Seruya; jinsi alivyowatendea majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua wakati wa amani akitaka kulipiza kisasi kwa mauaji waliyofanya wakati wa vita. Aliwaua watu wasiokuwa na hatia, nami nikachukua lawama kwa ajili ya vitendo vyake ambavyo vimeniletea mateso. Basi, wewe fanya kadiri ya hekima yako, ila tu usimwache afe kwa amani. “Lakini uwatendee mema wana wa Barzilai, Mgileadi, na uwatunze kwa ukarimu wawe kati ya wale wanaokula mezani pako; kwa sababu walinitendea mema wakati nilipomkimbia ndugu yako Absalomu. Pia, yupo Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini wa Bahurimu, ambaye aliniapiza na kunilaani vikali nilipokwenda Mahanaimu; lakini alipokuja kunilaki kwenye mto Yordani, nilimwapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu nikimwambia, ‘Sitakuua kwa upanga.’ Lakini wewe usimwache bila kumwadhibu. Wewe una hekima; utajua utakalomfanyia; ingawa yeye ana mvi, usimwache; muue ingawa ni mzee.” Daudi alifariki, akazikwa katika mji wake. Alikuwa ametawala Israeli kwa muda wa miaka arubaini; miaka saba akiwa Hebroni, na miaka thelathini na mitatu akiwa Yerusalemu. Basi, Solomoni akaketi katika kiti cha enzi mahali pa Daudi, baba yake; na ufalme wake ukaimarika. Baadaye, Adoniya mwana wa Hagithi, alimwendea Bathsheba, mama yake Solomoni. Bathsheba akamwuliza, “Je, unakuja kwa amani?” Adoniya akamjibu, “Ndiyo, nakuja kwa amani. Ila, nina jambo moja tu la kukuambia.” Bathsheba akamwambia, “Sema tu.” Adoniya akamwambia, “Unajua kwamba mimi ningalikuwa mfalme, na hata Israeli yote ilikuwa inanitazamia niwe mfalme. Lakini, mambo yakageuka na ndugu yangu akanipindua, kwani hayo ndio yaliyokuwa mapenzi yake Mwenyezi-Mungu. Sasa, ninalo ombi moja tu ambalo nakusihi usinikatalie.” Bathsheba akamwambia, “Sema tu.” Naye akasema, “Tafadhali, nakusihi umwombe mfalme Solomoni aniruhusu nimchukue Abishagi, yule Mshunami, awe mke wangu, kwa maana najua hatakukatalia wewe.” Bathsheba akamwambia, “Sawa; nitazungumza na mfalme kwa niaba yako.” Basi, Bathsheba akamwendea mfalme Solomoni kumweleza ombi la Adoniya. Mfalme akainuka kwenda kumlaki mama yake, akamwinamia. Halafu, akaketi katika kiti chake cha enzi, akaagiza mama yake aletewe kiti; naye akakaa upande wa kulia wa mfalme. Bathsheba akasema, “Nina ombi dogo tafadhali ulikubali, na ninakuomba usinikatalie.” Mfalme akamwambia, “Sema ombi lako mama yangu, kwa sababu sitakukatalia.” Naye akasema, “Mruhusu ndugu yako Adoniya amwoe Abishagi, huyo Mshunami.” Mfalme Solomoni akamwuliza mama yake, “Kwa nini unataka nimpe Abishagi? Hii ni sawa kabisa na kumtakia ufalme wangu! Kumbuka ya kwamba yeye ni kaka yangu mkubwa, na isitoshe, kuhani Abiathari na jemadari Yoabu mwana wa Seruya, wako upande wake!” Hapo mfalme Solomoni akaapa kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akisema, “Mungu na aniulie mbali ikiwa Adoniya hatakufa kwa sababu ya kutoa ombi hili! Sasa basi, kwa jina la Mwenyezi-Mungu aliye hai, aliyeniweka na kuniimarisha katika ufalme wa baba yangu Daudi, na aliyetimiza ahadi yake, akanipa enzi mimi na wazawa wangu, naapa kwamba hivi leo Adoniya atakufa!” Ndipo mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada; naye akamwendea Adoniya, akamuua. Mfalme Solomoni akamwambia kuhani Abiathari, “Ondoka uende shambani kwako, huko Anathothi; unastahili kufa wewe! Lakini sasa, sitakuua kwa sababu ulilishughulikia sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu ulipokuwa na baba yangu Daudi, ukateswa pamoja naye.” Basi, mfalme Solomoni akamfukuza Abiathari, asiwe kuhani wa Mwenyezi-Mungu; hivyo likatimia neno alilosema Mwenyezi-Mungu huko Shilo, juu ya Eli na ukoo wake. Yoabu alipopata habari, alikimbilia hemani mwa Mungu na kushikilia pembe za madhabahu; kwa maana alikuwa amemwunga mkono Adoniya na si Absalomu. Mfalme Solomoni aliposikia kwamba Yoabu yumo katika hema la Mungu na kwamba amesimama madhabahuni, alimtuma Benaya mwana wa Yehoyada, akisema, “Nenda ukampige.” Basi, Benaya akaenda katika hema la Mungu, akamwambia Yoabu, “Mfalme ameamuru utoke nje.” Yoabu akajibu, “Mimi sitoki; nitakufa papa hapa.” Benaya akarudi kwa mfalme na kumweleza alivyojibu Yoabu. Solomoni akasema, “Fanya alivyosema; umuue na kumzika. Hivyo, mimi na wazawa wengine wote wa Daudi hatutalaumiwa kwa vitendo vya Yoabu vya kuwaua watu wasio na hatia. Mungu atamwadhibu Yoabu kwa mauaji hayo aliyoyafanya bila baba yangu kuwa na habari. Yeye aliwaua watu wawili ambao walikuwa wa maana zaidi kuliko yeye, pia walimzidi kwa wema; aliwaua Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda. Adhabu ya mauaji hayo itakuwa juu ya Yoabu na wazawa wake milele. Bali Mwenyezi-Mungu atawapa ufanisi daima, Daudi na wazawa wake watakaokalia kiti chake cha enzi.” Basi, Benaya mwana wa Yehoyada, akaenda hemani, akamuua Yoabu ambaye alizikwa shambani mwake, nyikani. Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada, kuwa jemadari wa jeshi mahali pa Yoabu, na Sadoki akawa kuhani mahali pa Abiathari. Halafu mfalme akaagiza Shimei aitwe, akamwambia, “Jijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae hapa bila kwenda mahali pengine popote pale. Maana siku utakapotoka na kuvuka kijito Kidroni, nakuambia kweli utakufa, na kujilaumu wewe mwenyewe kwa kifo chako.” Shimei akajibu, “Vema mfalme. Nitafanya kama ulivyosema.” Basi, akakaa Yerusalemu muda mrefu. Lakini mwishoni mwa mwaka wa tatu, watumwa wawili wa Shimei walitoroka, wakaenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Habari zilipomfikia kwamba wako Gathi, Shimei alipanda punda wake, akaenda huko kuwatafuta, kwa mfalme Akishi. Basi, akafika, akawapata, akawarudisha nyumbani. Mfalme Solomoni alipopata habari kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu, akaenda Gathi na kurudi, alimwita Shimei na kumwambia, “Je, hukuniapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu kwamba hutatoka Yerusalemu, nami sikukuonya kwa dhati kwamba, hakika utakufa kama utathubutu kwenda nje? Nawe ulikubali, ukaniambia, ‘Vema, nitatii.’ Mbona basi, umevunja kiapo chako kwa Mwenyezi-Mungu na kutojali amri niliyokupa?” Mfalme aliendelea kumwambia Shimei, “Unayajua wazi maovu uliyomtendea baba yangu Daudi, na sasa, kwa sababu ya hayo, Mwenyezi-Mungu atakuadhibu. Lakini mimi atanibariki, na kiti cha enzi cha Daudi kitaimarishwa mbele ya Mwenyezi-Mungu milele.” Hapo, mfalme akamwamuru Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka, akampiga na kumuua Shimei. Basi, ufalme ukaimarika chini ya Solomoni.