Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 19:9-21

1 Wafalme 19:9-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Huko, akafika penye pango, akakaa humo. Mara neno la Mwenyezi-Mungu likamjia: “Elia! Unafanya nini hapa?” Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda, waniue!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda ukasimame mlimani, mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mwenyezi-Mungu akapita na kuuvumisha upepo mkali ambao uliporomosha milima na kuvunja miamba. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika upepo huo. Upepo ukapita, kukawa na tetemeko la ardhi. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika tetemeko la ardhi. Tetemeko likapita, kukawa na moto. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika moto huo. Baada ya moto, pakatokea sauti ndogo, tulivu. Basi, Elia aliposikia sauti hiyo, alijifunika uso kwa joho lake, akatoka na kusimama mlangoni mwa pango. Hapo, akasikia sauti, “Elia! Unafanya nini hapa?” Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda waniue!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa kupitia njia ya jangwani mpaka Damasko. Utakapofika, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu. Naye Yehu, mwana wa Nimshi, mpake mafuta awe mfalme wa Israeli. Elisha, mwana wa Shafati, wa Abel-mehola, utampaka mafuta awe nabii mahali pako. Basi, yeyote atakayenusurika upanga wa Hazaeli, Yehu atamuua, na yeyote atakayenusurika upanga wa Yehu, Elisha atamuua. Lakini, nitaacha hai watu 7,000 nchini Israeli, ambao hawajamwinamia Baali, wala kuibusu sanamu yake.” Elia akaondoka, akamkuta Elisha, mwana wa Shafati, analima. Hapo, palikuwa na jozi kumi na mbili za ng'ombe wanalima, na jozi ya Elisha ilikuwa ya nyuma kabisa. Basi, Elia akavua joho lake na kumtupia. Hapo, Elisha akawaacha ng'ombe wake, akamfuata Elia mbio na kumwambia, “Niruhusu kwanza niende kumpa baba yangu na mama yangu busu la kwaheri, kisha nikufuate.” Elia akamjibu, “Nenda! Kwani nimekuzuia?” Basi, Elisha akamwacha Elia, akairudia jozi yake ya ng'ombe, akawachinja ng'ombe hao na kuwapika akitumia miti ya nira kama kuni, akawapa watu, wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Elia na kuwa mtumishi wake.

1 Wafalme 19:9-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Huko akaingia katika pango, akalala humo usiku ule. BWANA Nalo neno la BWANA likamjia, kusema, “Unafanya nini hapa, Eliya?” Akajibu, “Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote. Waisraeli wamelikataa Agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi, mimi peke yangu, niliyebaki, nao sasa wananitafuta ili waniangamize.” BWANA akasema, “Toka nje ukasimame juu ya mlima mbele za BWANA, kwa kuwa BWANA yu karibu kupita hapo.” Kisha upepo mwingi na wenye nguvu ukapasua milima ile na kuvunjavunja miamba mbele za BWANA, lakini BWANA hakuwamo katika ule upepo. Baada ya upepo palikuwa na tetemeko la nchi, lakini BWANA hakuwamo kwenye lile tetemeko. Baada ya tetemeko la nchi ukaja moto, lakini BWANA hakuwamo katika ule moto. Baada ya moto ikaja sauti ya utulivu ya kunongʼona. Eliya alipoisikia, akafunika uso kwa vazi lake, akatoka na kusimama kwenye mdomo wa pango. Kisha ile sauti ikamwambia, “Eliya, unafanya nini hapa?” Akajibu, “Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote. Waisraeli wamelikataa Agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi, mimi peke yangu, niliyebaki, nao sasa wananitafuta ili waniangamize.” BWANA akamwambia, “Rudi kwa njia uliyoijia, uende kwenye Jangwa la Dameski. Wakati utakapofika huko, mtie Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu Pia mtie mafuta Yehu mwana wa Nimshi awe mfalme wa Israeli, na umtie Elisha mwana wa Shafati kutoka Abel-Mehola mafuta awe nabii badala yako. Yehu atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Hazaeli, naye Elisha atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Yehu. Hata sasa nimeweka akiba watu elfu saba katika Israeli, wote ambao hawajampigia Baali magoti, na wote ambao midomo yao haijambusu.” Hivyo Eliya akaondoka kutoka huko na kumkuta Elisha mwana wa Shafati. Alikuwa akilima kwa jozi kumi na mbili za maksai, na yeye mwenyewe aliongoza ile jozi ya kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akamrushia vazi lake. Kisha Elisha akawaacha maksai wake, akamkimbilia Eliya, akamwambia, “Niruhusu nikawabusu baba yangu na mama yangu, halafu nitafuatana nawe.” Eliya akajibu, “Rudi zako, kwani nimekutendea nini?” Basi Elisha akamwacha Eliya, naye akarudi. Akachukua ile jozi yake ya maksai na kuwachinja. Akaipika ile nyama kwa kutumia miti ya nira kama kuni na kuwapa watu, nao wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Eliya, akamtumikia.

1 Wafalme 19:9-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la BWANA likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya BWANA Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe. Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za BWANA. Na tazama, BWANA akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunjavunja miamba mbele za BWANA; lakini BWANA hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini BWANA hakuwamo katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini BWANA hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu. Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya BWANA, Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe. BWANA akamwambia, Nenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako. Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua. Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu. Basi, akaondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng'ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake. Naye akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Nenda, urudi; ni nini niliyokutendea? Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng'ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng'ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia.

1 Wafalme 19:9-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la BWANA likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya BWANA Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe. Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za BWANA. Na tazama, BWANA akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za BWANA; lakini BWANA hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini BWANA hakuwamo katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini BWANA hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu. Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya BWANA, Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe. BWANA akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako. Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua. Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu. Basi, akaondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng’ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake. Naye akawaacha ng’ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Enenda, urudi; ni nini niliyokutendea? Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng’ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng’ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia.