1 Wafalme 16:29-34
1 Wafalme 16:29-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ahabu mwana wa Omri akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala Israeli akiwa Samaria kwa miaka ishirini na miwili. Ahabu mwana wa Omri akafanya maovu zaidi machoni mwa BWANA kuliko yeyote aliyewatangulia. Kama vile haikutosha kuishi kama Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti wa Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, naye akaanza kumtumikia Baali na kumwabudu. Akajenga madhabahu kwa ajili ya Baali katika hekalu la Baali lile alilolijenga huko Samaria. Pia Ahabu akatengeneza nguzo ya Ashera na kufanya mengi ili kumkasirisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko walivyofanya wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. Katika wakati wa Ahabu, Hieli, Mbetheli, akaijenga upya Yeriko. Aliweka misingi yake kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza Abiramu, na kuweka malango yake kwa gharama ya mwanawe mdogo Segubu, kulingana na neno la BWANA alilosema kupitia Yoshua mwana wa Nuni.
1 Wafalme 16:29-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ahabu mwana wa Omri, alianza kutawala Israeli. Alitawala huko Samaria kwa muda wa miaka ishirini na miwili. Ahabu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kuliko wafalme wote waliomtangulia. Tena, licha ya kuiga mwenendo mbaya wa Yeroboamu mwana wa Nebati, Ahabu alimwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni; akamtumikia na kumwabudu Baali. Alimjengea Baali hekalu huko Samaria, na ndani yake akatengeneza madhabahu ya kumtambikia. Hali kadhalika, alitengeneza sanamu ya Ashera mungu wa kike. Ahabu alitenda maovu mengi, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu Mungu wa Israeli zaidi ya wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. Wakati wa utawala wake, Hieli kutoka Betheli, aliujenga upya mji wa Yeriko. Na sawa kabisa na neno la Mwenyezi-Mungu alilonena kwa njia ya Yoshua mwana wa Nuni, Hieli alifiwa na mzaliwa wake wa kwanza Abiramu, wakati wa kuiweka misingi ya Yeriko, akafiwa pia na mwanawe mdogo Segubu, wakati wa kuyaweka malango yake.
1 Wafalme 16:29-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ahabu mwana wa Omri alianza kutawala juu ya Israeli katika mwaka wa thelathini na nane wa Asa mfalme wa Yuda; akatawala Ahabu mwana wa Omri juu ya Israeli katika Samaria miaka ishirini na miwili. Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kuliko wote waliomtangulia. Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia. Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria. Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.
1 Wafalme 16:29-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)