1 Wafalme 16:15-20
1 Wafalme 16:15-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Zimri alitawala huko Israeli kutoka Tirza kwa muda wa siku saba. Huo ulikuwa mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Basi, watu wa Israeli walikuwa wamepiga kambi kuuzingira mji wa Gibethoni wa Wafilisti, na majeshi ya watu wa Israeli waliposikia kwamba Zimri alikuwa amekula njama, akamuua mfalme, wote wakamtawaza Omri, amiri jeshi wao, kuwa mfalme wa Israeli siku hiyohiyo. Omri na majeshi yake akaondoka Gibethoni, akaenda na kuuzingira mji wa Tirza. Zimri alipoona kwamba mji umezingirwa, aliingia ngomeni, ndani ya ikulu, akaichoma moto, naye akafia humo. Jambo hilo lilifanyika kwa sababu ya dhambi alizotenda alifanya maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamwiga Yeroboamu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Matendo mengine ya Zimri na njama aliyokula, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.
1 Wafalme 16:15-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala muda wa siku saba huko Tirza. Basi, watu walikuwa wametua kambini kupigana na Gibethoni, ulio wa Wafilisti. Na hao watu waliokuwako kambini wakasikia habari ya kwamba Zimri amekula njama, tena amemwua mfalme; kwa hiyo Israeli wote wakamfanya Omri, jemadari wa jeshi, awe mfalme juu ya Israeli siku ile kambini. Omri akapanda kutoka Gibethoni, na Israeli wote pamoja naye, wakauhusuru Tirza. Ikawa Zimri alipoona ya kuwa mji umetwaliwa, akaingia ngomeni mwa nyumba ya mfalme, akaiteketeza nyumba ya mfalme juu yake kwa moto, akafa; kwa sababu ya makosa aliyoyakosa, akifanya mabaya machoni pa BWANA, kwa kuiendea njia ya Yeroboamu na makosa yake aliyoyafanya akiwakosesha Israeli. Na mambo yote ya Zimri yaliyosalia na fitina yake aliyoifanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?
1 Wafalme 16:15-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala huko Tirsa siku saba. Jeshi lilikuwa limepiga kambi karibu na Gibethoni, mji wa Wafilisti. Wakati Waisraeli waliokuwa kambini waliposikia kuwa Zimri alikuwa amefanya hila mbaya dhidi ya mfalme na kumuua, wakamtangaza Omri, jemadari wa jeshi, kuwa mfalme wa Israeli siku iyo hiyo huko kambini. Ndipo Omri na Waisraeli wote pamoja naye wakaondoka Gibethoni na kuizingira Tirsa. Wakati Zimri alipoona kuwa mji umechukuliwa, alikwenda ndani ya ngome ya jumba la kifalme na kulichoma moto jumba la kifalme na kujiteketeza ndani yake. Kwa hiyo akafa, kwa sababu ya dhambi alizofanya, akitenda maovu machoni pa BWANA na kuenenda katika njia za Yeroboamu na katika dhambi alizofanya na kusababisha Israeli kuzifanya. Kwa matukio mengine ya utawala wa Zimri, na uasi alioutenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
1 Wafalme 16:15-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala muda wa siku saba huko Tirza. Basi, watu walikuwa wametua maragoni kupigana na Gibethoni, ulio wa Wafilisti. Na hao watu waliokuwako maragoni wakasikia habari ya kwamba Zimri amefanya fitina, tena amempiga mfalme; kwa hiyo Israeli wote wakamfanya Omri, jemadari wa jeshi, awe mfalme juu ya Israeli siku ile maragoni. Omri akapanda kutoka Gibethoni, na Israeli wote pamoja naye, wakauhusuru Tirza. Ikawa Zimri alipoona ya kuwa mji umetwaliwa, akaingia ngomeni mwa nyumba ya mfalme, akaiteketeza nyumba ya mfalme juu yake kwa moto, akafa; kwa sababu ya makosa aliyoyakosa, akifanya mabaya machoni pa BWANA, kwa kuiendea njia ya Yeroboamu na makosa yake aliyoyafanya akiwakosesha Israeli. Na mambo yote ya Zimri yaliyosalia na fitina yake aliyoifanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?