1 Wafalme 14:12-20
1 Wafalme 14:12-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Ahiya akamwambia mkewe Yeroboamu, “Haya inuka, uende zako nyumbani. Mara tu utakapoingia mjini, mwanao atakufa. Watu wote wa Israeli watafanya matanga na kumzika. Walakini, ni huyo tu wa jamaa ya Yeroboamu atakayezikwa, kwani ni yeye tu wa jamaa ya Yeroboamu aliyepata kumpendeza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Tena leo hii, Mwenyezi-Mungu ataweka mfalme mwingine katika Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Naam, tangu sasa, Mwenyezi-Mungu atawapiga watu wa Israeli, nao watatikisika kama unyasi unavyotikiswa mtoni. Atawangoa kutoka nchi hii nzuri aliyowapa babu zao, na kuwatawanya mbali, ngambo ya mto Eufrate, kwa sababu wamemkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa kujitengenezea sanamu za Ashera, mungu wa kike. Mwenyezi-Mungu ataitupa Israeli kwa sababu ya dhambi alizotenda Yeroboamu, na kuwafanya watu wa Israeli pia watende dhambi.” Hapo, mkewe Yeroboamu akaondoka, akashika safari mpaka Tirza. Mara tu alipofika mlangoni, mtoto akafa. Watu wote wa Israeli wakamzika na kufanya matanga kama alivyosema Mwenyezi-Mungu, kwa njia ya nabii Ahiya, mtumishi wake. Matendo mengine ya mfalme Yeroboamu, jinsi alivyopigana vita na alivyotawala, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Yeroboamu alitawala kwa muda wa miaka ishirini na miwili, halafu akafariki, na Nadabu, mwanawe, akatawala mahali pake.
1 Wafalme 14:12-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi ondoka, urudi nyumbani kwako; na miguu yako itakapoingia mjini huyo kijana atakufa. Na Israeli wote watamlilia, na kumzika, kwa maana ndiye peke yake wa Yeroboamu atakayeingia kaburini; kwa sababu limeonekana ndani yake jambo lililo jema kwa BWANA, Mungu wa Israeli, nyumbani mwa Yeroboamu. Tena Bwana atajiinulia mfalme wa Israeli atakayeiharibu nyumba ya Yeroboamu siku ile; na nini tena hata sasa? Kwa kuwa BWANA atawapiga Israeli kama manyasi yatikiswavyo majini; naye atawang'oa Israeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, naye atawatawanya ng'ambo ya Mto; kwa sababu wamejitengenezea Maashera yao, wakimkasirisha BWANA. Naye atawatoa Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu, aliyoyakosa, ambayo kwa hayo amewakosesha Israeli. Basi mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda zake, akafika Tirza; naye alipofika kizingitini kwa nyumba, huyo kijana akafa. Israeli wote wakamzika, wakamlilia; sawasawa na neno la BWANA, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Ahiya nabii. Na mambo yake Yeroboamu yaliyosalia, ya kupigana na ya kutawala, tazama, yameandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli. Na siku alizotawala Yeroboamu zilikuwa miaka ishirini na miwili; akalala na babaze, naye Nadabu mwanawe akatawala mahali pake.
1 Wafalme 14:12-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi ondoka, urudi nyumbani kwako; na miguu yako itakapoingia mjini huyo kijana atakufa. Na Israeli wote watamlilia, na kumzika, kwa maana ndiye peke yake wa Yeroboamu atakayeingia kaburini; kwa sababu limeonekana ndani yake jambo lililo jema kwa BWANA, Mungu wa Israeli, nyumbani mwa Yeroboamu. Tena Bwana atajiinulia mfalme wa Israeli atakayeiharibu nyumba ya Yeroboamu siku ile; na nini tena hata sasa? Kwa kuwa BWANA atawapiga Israeli kama manyasi yatikiswavyo majini; naye atawang’oa Israeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, naye atawatawanya ng’ambo ya Mto; kwa sababu wamejifanyia maashera yao, wakimkasirisha BWANA. Naye atawatoa Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu, aliyoyakosa, ambayo kwa hayo amewakosesha Israeli. Basi mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda zake, akafika Tirza; naye alipofika kizingitini kwa nyumba, huyo kijana akafa. Israeli wote wakamzika, wakamlilia; sawasawa na neno la BWANA, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Ahiya nabii. Na mambo yake Yeroboamu yaliyosalia, ya kupigana na ya kutawala, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli. Na siku alizotawala Yeroboamu zilikuwa miaka ishirini na miwili; akalala na babaze, naye Nadabu mwanawe akatawala mahali pake.
1 Wafalme 14:12-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kukuhusu wewe, rudi nyumbani. Wakati utakapotia mguu katika mji wako, kijana atakufa. Israeli yote itamwombolezea na kumzika. Kwa sababu ni yeye pekee wa nyumba ya Yeroboamu atakayezikwa, kwa sababu ni yeye peke yake ndani ya nyumba ya Yeroboamu ambaye BWANA, Mungu wa Israeli, ameona kitu chema kwake. “BWANA atajiinulia mwenyewe mfalme juu ya Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Siku ndiyo hii! Nini? Naam, hata sasa hivi. Naye BWANA ataipiga Israeli, hata iwe kama unyasi unaosukwasukwa juu ya maji. Ataingʼoa Israeli kutoka nchi hii nzuri aliyowapa baba zao na kuwatawanya ngʼambo ya Mto Frati, kwa sababu wamemghadhibisha BWANA kwa kutengeneza nguzo za Ashera Naye atawaacha Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu aliyoyatenda na kusababisha Israeli kuyatenda.” Kisha mke wa Yeroboamu akainuka, akaondoka kwenda Tirsa. Mara alipokanyaga kizingiti cha mlango, kijana akafa. Wakamzika na Israeli yote ikamwombolezea, kama BWANA alivyokuwa amesema kupitia mtumishi wake, nabii Ahiya. Matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, vita vyake na jinsi alivyotawala, vimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. Yeroboamu akawatawala kwa miaka ishirini na miwili, kisha akalala na baba zake. Naye Nadabu mwanawe akawa mfalme baada yake.