1 Wafalme 10:13-29
1 Wafalme 10:13-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme Solomoni naye alimpatia malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na alichotaka; pamoja na vitu vingine ambavyo Solomoni alimpa kutokana na ukarimu wake wa kifalme. Basi malkia akarudi nchini kwake pamoja na watumishi wake. Kila mwaka, Solomoni alipelekewa dhahabu kilo 22,000. Kiasi hicho si pamoja na dhahabu aliyopata kwa wafanyabiashara na wachuuzi, kwa wafalme wote wa Arabia na wakuu wa mikoa ya Israeli. Mfalme Solomoni alitengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao kilo 7 za dhahabu. Alitengeneza ngao ndogondogo 300 kwa dhahabu iliyofuliwa, kila ngao kilo 1.5; halafu mfalme akaziweka katika jengo lililoitwa Nyumba ya Msitu wa Lebanoni. Vilevile mfalme alitengeneza kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakipaka dhahabu safi kabisa. Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita. Sehemu ya juu ilikuwa imeviringwa na kiliwekewa mahali pa kuegemeza mkono pande zake mbili; na sanamu za simba wawili zimesimama moja kando ya mahali hapo pa kuegemeza mkono. Kulikuwa pia na sanamu kumi na mbili za simba zimesimama, moja mwishoni mwa kila ngazi. Kiti kama hicho hakijawahi kutengenezwa katika ufalme wowote ule. Vyombo vyote vya kunywea divai vya mfalme Solomoni vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vilivyokuwa katika Nyumba ya Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi; hakuna kilichotengenezwa kwa madini ya fedha kwani madini ya fedha haikuthaminiwa kuwa kitu wakati huo. Kwa kuwa mfalme Solomoni alikuwa na msafara wa meli za Tarshishi zilizokuwa zikisafiri pamoja na meli za Hiramu, kila mwaka wa tatu meli hizo za Tarshishi zilimletea mfalme dhahabu, fedha, pembe, nyani na tausi. Hivyo, mfalme Solomoni aliwapita wafalme wote duniani kwa mali na hekima. Watu wa nchi zote walikuwa na hamu ya kumwendea Solomoni ili kusikiliza hekima yake ambayo Mungu alikuwa amemjalia. Kila mmoja wao alimletea zawadi: Vyombo vya fedha, vya dhahabu, mavazi, manemane, manukato, farasi na nyumbu. Zawadi hizi alizipokea kila mwaka. Solomoni alikusanya magari ya farasi na wapandafarasi, alikuwa na magari ya farasi 1,400 na wapandafarasi 12,000 ambao aliwaweka katika miji yenye vituo vya magari ya farasi, na huko Yerusalemu. Basi, Solomoni alifanya madini ya fedha katika Yerusalemu kuwa kitu cha kawaida kama mawe, na mbao za mierezi zilikuwa nyingi kama mbao za mikuyu ya Shefela. Solomoni aliagiza farasi kutoka Misri, na pia kutoka Kilikia ambako wafanyabiashara wake waliuziwa na watu wa Kilikia. Gari moja la kukokotwa liliweza kununuliwa huko Misri kwa fedha ipatayo kilo 7, na farasi mmoja aliweza kugharimu fedha kilo 2. Wafanyabiashara wa mfalme walisafirisha magari na farasi hao na kuwauzia wafalme wote wa Wahiti na wa Wasiria.
1 Wafalme 10:13-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya hayo aliyopewa na Sulemani kwa ukarimu wake wa kifalme. Basi, akarudi akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake. Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita, zaidi ya faida ya wachuuzi, na bidhaa ya wafanya biashara, na ya wafalme wote wa hao waliochanganyika, na ya watawala wa nchi. Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; kila ngao moja ilipata shekeli mia sita za dhahabu. Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kila kigao kimoja kilipata mane tatu za dhahabu. Mfalme akaviweka katika nyumba ya msitu wa Lebanoni. Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi. Kiti kile kilikuwa na ngazi sita, na juu yake kimeviringana nyuma; na mikono huku na huko mahali pa kuketi, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono. Na simba kumi na wawili wamesimama juu ya ngazi sita huku na huko; wala hakikufanyika kwa mkono wake katika ufalme wowote. Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; hakuna vya fedha, fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani. Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu za Tarshishi baharini pamoja na merikebu za Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi. Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima. Ulimwengu wote ukamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni. Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka. Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu moja mia nne, na wapandao farasi elfu kumi na mbili, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu. Mfalme akafanya fedha humo Yerusalemu kuwa kama mawe, na mierezi akaifinya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi. Nao farasi aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi, kila kundi na thamani yake. Tena gari huja kutoka katika Misri kwa shekeli mia sita za fedha, na farasi mmoja kwa mia moja na hamsini; hivyo basi watu wakawaletea wafalme wote wa Wahiti, na wafalme wa Shamu, mikononi mwao.
1 Wafalme 10:13-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya hayo aliyopewa na Sulemani kwa ukarimu wake wa kifalme. Basi, akarudi akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake. Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita, zaidi ya faida ya wachuuzi, na bidhaa ya wafanya biashara, na ya wafalme wote wa hao waliochanganyika, na ya maliwali wa nchi. Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; kila ngao moja ilipata shekeli mia sita za dhahabu. Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kila kigao kimoja kilipata mane tatu za dhahabu. Mfalme akaviweka katika nyumba ya mwitu wa Lebanoni. Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi. Kiti kile kilikuwa na daraja sita, na juu yake kimeviringana nyuma; na mikono huko na huko mahali pa kuketi, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono. Na simba kumi na wawili wamesimama juu ya daraja sita huko na huko; wala hakikufanyika kwa mkono wake katika ufalme wo wote. Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; hakuna vya fedha, fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani. Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu za Tarshishi baharini pamoja na merikebu za Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi. Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima. Ulimwengu wote ukamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni. Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka. Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu na mia nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu. Mfalme akafanya fedha humo Yerusalemu kuwa kama mawe, na mierezi akaifinya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi. Nao farasi aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi, kila kundi na thamani yake. Tena gari huja kutoka katika Misri kwa shekeli mia sita za fedha, na farasi mmoja kwa mia hamsini; vivyo watu wakawaletea wafalme wote wa Wahiti, na wafalme wa Shamu, mikononi mwao.
1 Wafalme 10:13-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mfalme Solomoni akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, kando na vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake. Uzito wa dhahabu ambayo Solomoni alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta 666, mbali na mapato kutoka kwa wafanyabiashara na wachuuzi, na kutoka kwa wafalme wote wa Kiarabu na watawala wa nchi. Mfalme Solomoni akatengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli 600 Akatengeneza pia ngao ndogo 300 za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni. Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi. Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na egemeo la nyuma lilikuwa la mviringo kwa juu. Pande zote za kiti kulikuwa na mahali pa kuegemeza mikono, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono. Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wowote. Vikombe vyote vya Mfalme Solomoni vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo siku za Solomoni. Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara baharini zilizokuwa zikiandamana na meli za Hiramu. Kwa mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wakubwa na wadogo. Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia. Dunia yote ikatafuta kukutana na Solomoni ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake. Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja alileta zawadi: vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezi, farasi na nyumbu. Solomoni akakusanya magari ya vita na farasi. Alikuwa na magari 1,400 na farasi 12,000, ambayo aliyaweka katika miji ya magari na mengine akawa nayo huko Yerusalemu. Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu vilimani. Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue. Wafanyabiashara wa mfalme waliwanunua kutoka Kue. Waliagiza magari kutoka Misri kwa bei ya shekeli 600 za fedha na farasi kwa shekeli 150. Pia waliwauza nje kwa wafalme wote wa Wahiti na wa Waaramu.