1 Wafalme 10:1-8
1 Wafalme 10:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Malkia wa Sheba aliposikia sifa za Solomoni, kwa sababu ya jina la Mwenyezi-Mungu, alimwendea Solomoni ili kumjaribu kwa maswali magumu. Aliwasili akiwa amefuatana na msafara wa watu pamoja na ngamia waliobeba manukato, zawadi nyingi sana na vito vya thamani. Naye Solomoni akayajibu maswali yote; hapakuwa na swali lolote lililomshinda. Malkia wa Sheba alishangaa sana alipoiona hekima yote ya Solomoni, na nyumba aliyokuwa ameijenga; tena alipoona chakula kilicholetwa mezani mwake, jinsi maofisa walivyoketi mezani, jinsi watumishi walivyohudumu na walivyovalia, pia wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa ambazo alizitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, aliduwaa na kushangaa mno. Basi, akamwambia mfalme, “Mambo yote niliyosikia nchini kwangu kuhusu kazi zako na hekima yako ni kweli! Lakini sikuweza kuamini habari hizo mpaka nilipofika na kujionea mwenyewe. Kumbe sikuambiwa hata nusu yake; hekima yako na fanaka zako vimepita habari nilizopewa. Wana bahati wake zako! Wana bahati hawa watumishi wako ambao wanakuhudumia daima na kusikiliza hekima yako!
1 Wafalme 10:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la BWANA, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo. Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno aliloshindwa mfalme asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga, na chakula cha mezani pake, na maofisa wake walivyokaa, na kuhudumu kwao wahudumu wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na sadaka zake za kuteketezwa ambazo alizitoa katika nyumba ya BWANA, roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako.
1 Wafalme 10:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Solomoni na uhusiano wake na jina la BWANA, akaja kumjaribu kwa maswali magumu. Alifika Yerusalemu akiwa na msafara mkubwa sana: pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani; alikuja kwa Solomoni na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake. Solomoni akamjibu maswali yake yote, hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwa mfalme asiweze kumwelezea. Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika hekalu la BWANA, alipatwa na mshangao. Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli. Lakini sikuamini mambo haya hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia. Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wasimamao mbele yako daima na kusikia hekima yako!
1 Wafalme 10:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la BWANA, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo. Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga, na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya BWANA, roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako.