Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 1:1-53

1 Wafalme 1:1-53 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate joto. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate joto Basi wakatafuta msichana mzuri katika nchi yote ya Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. Naye msichana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; lakini mfalme hakumjua. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akatakabari, akasema, Mimi nitakuwa mfalme. Akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, na watu hamsini wapige mbio mbele yake. Tena baba yake hakumchukiza wakati wowote kwa kusema, Mbona umefanya hivi? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu. Akashauriana na Yoabu, mwana wa Seruya, na Abiathari, kuhani; nao wakamsaidia Adonia, wakamfuata. Ila Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Nathani, nabii, na Shimei, na Rei, na mashujaa wa Daudi, hao hawakuwa pamoja na Adonia. Adonia akatoa sadaka ya kondoo, ng'ombe na ndama wanono, karibu na jiwe la Zohelethi, lililo karibu na chemchemi Enrogeli; akawaita ndugu zake wote, wana wa mfalme, na watu wote wa Yuda, watumishi wa mfalme; ila nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Sulemani ndugu yake hakuwaalika. Ndipo Nathani akamwambia Bathsheba, mamaye Sulemani, akasema, Je! Hukusikia ya kuwa Adonia, mwana wa Hagithi, amekuwa mfalme, na bwana wetu Daudi hana habari? Haya basi, nikupe shauri, tafadhali, upate kuiokoa roho yako, na roho ya mwanao Sulemani. Nenda uingie ndani kwa mfalme Daudi, ukamwambie, Je! Hukuniapia mimi mjakazi wako, Ee mfalme, bwana wangu, kusema, Hakika yake Sulemani mwana wako atamiliki baada yangu, na kuketi katika kiti changu cha enzi? Mbona basi anamiliki Adonia? Tazama, wakati ule utakapokuwa katika kusema na mfalme, mimi nami nitaingia nyuma yako, na kuyahakikisha maneno yako. Basi Bathsheba akaingia ndani kwa mfalme, ndani ya chumba chake; naye mfalme alikuwa mzee sana; na Abishagi, Mshunami, alikuwa akimtumikia mfalme. Bathsheba akainama, akamsujudia mfalme. Naye mfalme akamwuliza, Wataka nini? Akamwambia, Bwana wangu, uliniapia mimi mjakazi wako kwa BWANA, Mungu wako, ya kwamba, bila shaka Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, yeye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi. Na sasa, angalia, Adonia anamiliki; na wewe, bwana wangu mfalme, huna habari. Tena amechinja ng'ombe, na vinono, na kondoo tele, na kuwaita wana wa mfalme wote pia, na Abiathari, kuhani, na Yoabu, jemadari wa jeshi. Ila Sulemani, mtumishi wako, huyu hakumwita. Ee mfalme, bwana wangu, macho ya Israeli wote yanakuelekea wewe, kwamba uwaambie ni nani atakayeketi katika kiti chako cha enzi baada yako, Ee mfalme, bwana wangu. Ama sivyo itakuwa, bwana wangu mfalme atakapolala pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Sulemani tutahesabiwa kuwa wahalifu. Basi tazama, alipokuwa katika kusema na mfalme, Nathani, nabii, aliingia. Wakamwambia mfalme wakasema, Tazama, Nathani, nabii. Naye alipoingia ndani mbele ya mfalme, akamsujudia kifudifudi. Nathani akasema, Ee mfalme, bwana wangu, je! Wewe umesema ya kwamba, Adonia atamiliki baada yangu, ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi? Maana leo ameshuka, na kuchinja ng'ombe, na vinono, na kondoo tele, naye amewaita wana wote wa mfalme, na majemadari wa jeshi, na Abiathari, kuhani; na tazama, wanakula na kunywa mbele yake, wakisema, Na aishi mfalme Adonia! Lakini mimi, mtumishi wako, na Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Sulemani, mtumishi wako, hakutuita sisi. Je! Bwana wangu mfalme ndiye aliyelitenda jambo hili, bila kutujulisha sisi watumishi wako ni nani atakayeketi katika kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme baada yake? Ndipo mfalme Daudi akajibu, akasema, Niitieni Bathsheba. Basi akaingia ndani kwa mfalme, akasimama mbele ya mfalme. Naye mfalme akaapa, akasema, BWANA aishivyo, aliyenikomboa roho yangu katika shida zote, hakika yake nitafanya leo kama vile nilivyokuapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli, nikasema, Kwa yakini Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, naye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi badala yangu. Ndipo Bathsheba akainama kifudifudi, akamsujudia mfalme, akasema, Bwana wangu mfalme Daudi na aishi milele. Naye mfalme Daudi akasema, Niitie Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada. Nao wakaingia ndani mbele ya mfalme. Naye mfalme akawaambia, Twaeni pamoja nanyi watumishi wa bwana wenu, mkampandishe Sulemani mwanangu juu ya nyumbu wangu mimi mkamteremshe mpaka Gihoni; kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na wamtie mafuta huko, awe mfalme juu ya Israeli; kapigeni panda, mkaseme, Mfalme Sulemani na aishi! Kisha pandeni juu nyuma yake, naye atakuja ili aketi katika kiti changu cha enzi; kwa maana atakuwa mfalme badala yangu; ndiye niliyemweka awamiliki Israeli na Yuda. Basi Benaya, mwana wa Yehoyada, akamjibu mfalme, akasema, Amina; BWANA, Mungu na bwana wangu mfalme, na aseme vivyo hivyo. Kama vile BWANA alivyokuwa pamoja na bwana wangu mfalme, kadhalika na awe pamoja na Sulemani, na kufanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi. Basi wakashuka Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha Sulemani juu ya nyumbu wa mfalme Daudi, wakampeleka mpaka Gihoni. Na Sadoki, kuhani, akatwaa ile pembe ya mafuta katika Hema, akamtia Sulemani mafuta. Nao wakapiga panda; na watu wote wakasema, Na aishi Mfalme Sulemani! Kisha watu wote wakapanda juu nyuma yake, watu wakapiga mazomari, wakafurahi kwa shangwe kuu mno, hata nchi ikapasuka kwa sauti zao. Basi Adonia, na wageni wote waliokuwa pamoja naye, wakasikia hayo walipokuwa wamekwisha kula. Naye Yoabu aliposikia sauti ya panda alisema, Za nini kelele hizi za mji uliotaharuki? Naye alipokuwa katika kunena, tazama Yonathani, mwana wa Abiathari kuhani, akafika. Naye Adonia akasema, Karibu; maana wewe u mtu mwema, unaleta habari njema. Naye Yonathani akajibu, akamwambia Adonia, Hakika bwana wetu mfalme Daudi amemtawaza Sulemani. Tena mfalme alipeleka pamoja naye Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha juu ya nyumbu wa mfalme. Kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, wakamtia mafuta huko Gihoni, ili awe mfalme. Nao wamepanda juu kutoka huko wakifurahi, hata mji ukavuma. Ndizo kelele zile mlizozisikia. Na tena, Sulemani ameketi katika kiti cha enzi cha ufalme. Na tena, watumishi wa mfalme walifika, ili wambariki bwana wetu mfalme Daudi, wakisema, Mungu wako na alikuze jina la Sulemani kuliko jina lako, na kukifanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti chako. Naye mfalme akainama chini juu ya kitanda chake. Na tena, mfalme akasema hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenipa leo hivi mtu wa kuketi katika kiti changu cha enzi, nayo macho yangu yakiwa yanaona hayo. Ndipo wageni wote waliokuwa pamoja na Adonia wakaogopa, wakaondoka, wakaenda zao kila mtu njia yake. Adonia naye akaogopa mbele ya Sulemani; akaondoka, akaenda, akazishika pembe za madhabahu. Akaambiwa Sulemani, kusema, Tazama, Adonia amwogopa mfalme Sulemani; kwani, tazama, amezishika pembe za madhabahu, akisema, Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hataniua mimi mtumwa wake kwa upanga. Sulemani Akasema, Akionekana kuwa mtu wa kweli, hata unywele wake mmoja hautaanguka chini; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa. Basi mfalme Sulemani akatuma watu, wakamteremsha toka madhabahuni. Naye akaja, akamwinamia mfalme Sulemani; naye Sulemani akamwambia, Nenda nyumbani kwako.

1 Wafalme 1:1-53 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mfalme Daudi alipokuwa mzee umri ukiwa umesogea, hakuweza kupata joto hata walipomfunika kwa nguo. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, “Turuhusu tumtafute kijana mwanamwali bikira amhudumie mfalme na kumtunza. Anaweza kulala pembeni mwake ili bwana wetu mfalme apate joto.” Kisha wakatafuta katika Israeli yote ili kumpata msichana mzuri wa sura na wakampata Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. Msichana huyo alikuwa mzuri sana wa sura, akamtunza mfalme na kumhudumia, lakini mfalme hakufanya naye tendo la ndoa. Basi Adoniya, ambaye mama yake alikuwa Hagithi, akajigamba na kusema, “Mimi nitakuwa mfalme.” Hivyo akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, pamoja na watu hamsini wa kumtangulia wakikimbia. (Baba yake hakuwa ameingilia na kumuuliza, “Kwa nini unafanya hivyo?” Alikuwa pia kijana mzuri sana wa sura, na alizaliwa baada ya Absalomu.) Adoniya akashauriana pamoja na Yoabu mwana wa Seruya na kuhani Abiathari, nao wakamsaidia. Lakini kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada, Nathani nabii, Shimei, Rei na walinzi maalum wa Daudi hawakujiunga na Adoniya. Ndipo Adoniya akatoa dhabihu ya kondoo, ngʼombe na ndama walionona kwenye Jiwe la Zohelethi karibu na En-Rogeli. Akawaalika ndugu zake wote, wana wa mfalme na wanaume wote wa Yuda waliokuwa maafisa wa mfalme, lakini hakumwalika nabii Nathani, Benaya, walinzi maalum wa mfalme, wala ndugu yake Solomoni. Ndipo Nathani akamuuliza Bathsheba, mama yake Solomoni, “Je, hujasikia kwamba Adoniya, mwana wa Hagithi, amekuwa mfalme pasipo bwana wetu Daudi kujua jambo hili? Sasa basi, acha nikushauri jinsi utakavyookoa uhai wako mwenyewe na uhai wa mwanao Solomoni. Ingia kwa Mfalme Daudi na umwambie, ‘Bwana wangu mfalme, je hukuniapia mimi mtumishi wako: “Hakika mwanao Solomoni atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi juu ya kiti changu cha ufalme”? Kwa nini basi Adoniya amekuwa mfalme?’ Utakapokuwa ukizungumza na mfalme, nitaingia na kuthibitisha hayo uliyoyasema.” Hivyo Bathsheba akaenda kumwona mfalme chumbani mwake mahali ambapo Abishagi, Mshunami, alikuwa akimhudumia, naye mfalme alikuwa mzee sana. Bathsheba akasujudu na kupiga magoti mbele ya mfalme. Mfalme akauliza, “Ni nini hiki unachotaka?” Akamwambia, “Bwana wangu, wewe mwenyewe uliniapia mimi mtumishi wako kwa BWANA Mungu wako kwamba: ‘Solomoni Mwanao atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme.’ Lakini sasa Adoniya amekuwa mfalme, nawe, bwana wangu mfalme huna habari kuhusu jambo hilo. Ametoa dhabihu idadi kubwa ya ngʼombe, ndama walionona na kondoo, naye amewaalika wana wa mfalme wote, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini hakumwalika Solomoni mtumishi wako. Bwana wangu mfalme, macho ya Israeli yote yanakutazama wewe wajue kutoka kwako kuwa ni nani atakayeketi katika kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake. Kama sivyo, mara tu bwana wangu mfalme atakapopumzishwa pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Solomoni tutatendewa kama wahalifu.” Alipokuwa angali anazungumza na mfalme, nabii Nathani akafika. Wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Kisha akaenda mbele ya mfalme na kumsujudia hadi uso wake ukagusa ardhi. Nathani akasema, “Je, bwana wangu mfalme, umetangaza kuwa Adoniya atakuwa mfalme baada yako na kwamba ataketi kwenye kiti chako cha ufalme? Leo ameshuka na kutoa dhabihu idadi kubwa ya ngʼombe, ndama walionona na kondoo. Amewaalika wana wote wa mfalme, jemadari wa jeshi na kuhani Abiathari. Sasa hivi, wanakula na kunywa pamoja naye wakisema, ‘Aishi maisha marefu, Mfalme Adoniya!’ Lakini mimi mtumishi wako, kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada na mtumishi wako Solomoni hakutualika. Je, hili ni jambo ambalo bwana wangu mfalme amelifanya pasipo kuwajulisha watumishi wake ili wapate kujua ni nani atakayeketi kwenye kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake?” Ndipo Mfalme Daudi akasema, “Mwite Bathsheba, aingie ndani.” Hivyo akaingia mbele ya mfalme na kusimama mbele yake. Ndipo mfalme akaapa: “Hakika kama BWANA aishivyo, ambaye ameniokoa kutoka kila taabu, hakika nitatekeleza leo kile nilichokuapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli: Mwanao Solomoni atakuwa mfalme baada yangu, naye ataketi kwenye kiti changu cha ufalme baada yangu.” Kisha Bathsheba akasujudu akipiga magoti mbele ya mfalme uso wake ukigusa ardhi akasema, “Bwana wangu Mfalme Daudi na aishi milele!” Mfalme Daudi akasema, “Mwite kuhani Sadoki ndani, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada.” Walipofika mbele ya mfalme, akawaambia: “Wachukueni watumishi wa bwana wenu pamoja nanyi na mkamkalishe mwanangu Solomoni juu ya nyumbu wangu mwenyewe mkamteremshe hadi Gihoni. Huko kuhani Sadoki na nabii Nathani wamtie mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Pigeni tarumbeta na mpaze sauti, ‘Mfalme Solomoni aishi maisha marefu!’ Kisha mtapanda pamoja naye, atakuja na kuketi kwenye kiti changu cha ufalme na kutawala badala yangu. Nimemweka awe mtawala juu ya Israeli na Yuda.” Benaya mwana wa Yehoyada akamjibu mfalme, “Amen! BWANA, Mungu wa bwana wangu mfalme, na aseme vivyo hivyo. Kama vile BWANA alivyokuwa na bwana wangu mfalme, vivyo hivyo na awe na Solomoni kukifanya kiti chake cha utawala kuwa kikuu kuliko kile cha bwana wangu Mfalme Daudi!” Hivyo kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi wakampandisha Solomoni juu ya nyumbu wa Mfalme Daudi, nao wakamsindikiza hadi Gihoni. Kuhani Sadoki akachukua pembe ya mafuta kutoka kwenye hema takatifu na kumtia Solomoni mafuta. Kisha wakapiga tarumbeta na watu wote wakapaza sauti wakisema, “Mfalme Solomoni aishi maisha marefu!” Na watu wote wakakwea wakimfuata, wakipiga filimbi na kushangilia sana, hata ardhi ikatikisika kwa ile sauti. Adoniya pamoja na wageni wote waliokuwa pamoja naye wakasikia sauti hiyo walipokuwa wakimalizia karamu yao. Waliposikia sauti ya tarumbeta, Yoabu akauliza, “Nini maana ya makelele yote haya katika mji?” Hata alipokuwa anasema, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akafika. Adoniya akasema, “Ingia ndani. Mtu mstahiki kama wewe ni lazima alete habari njema.” Yonathani akajibu, “La hasha! Mfalme Daudi bwana wetu amemfanya Solomoni kuwa mfalme. Mfalme amemtuma pamoja naye kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme, nao kuhani Sadoki na nabii Nathani wamemtia mafuta kuwa mfalme huko Gihoni. Kuanzia hapo wameendelea kushangilia na sauti zimeenea pote mjini. Hizo ndizo kelele unazosikia. Zaidi ya hayo, Solomoni ameketi juu ya kiti chake cha ufalme. Pia, maafisa wa mfalme wamekuja ili kumtakia heri bwana wetu Mfalme Daudi wakisema, ‘Mungu wako na alifanye jina la Solomoni kuwa mashuhuri kuliko lako na kiti chake cha ufalme kiwe na ukuu kuliko chako!’ Naye mfalme akasujudu akiabudu kitandani mwake na kusema, ‘Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye ameruhusu macho yangu kuona mrithi juu ya kiti changu cha ufalme leo hii.’ ” Katika hili, wageni wote wa Adoniya wakainuka kwa mshtuko wa hofu na kutawanyika. Lakini Adoniya kwa kumwogopa Solomoni, akaenda na kushika pembe za madhabahu. Kisha Solomoni akaambiwa, “Adoniya anamwogopa Mfalme Solomoni na ameshikilia pembe za madhabahu. Anasema, ‘Mfalme Solomoni na aniapie leo kwamba hatamuua mtumishi wake kwa upanga.’ ” Solomoni akajibu, “Kama akijionyesha kuwa mtu mstahiki, hakuna unywele wake utakaoanguka juu ya ardhi, lakini kama uovu ukionekana ndani yake, atakufa.” Ndipo Mfalme Solomoni akawatuma watu, nao wakamshusha kutoka madhabahuni. Naye Adoniya akaja akamwinamia Mfalme Solomoni, naye Solomoni akamwambia, “Nenda nyumbani kwako.”

1 Wafalme 1:1-53 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Daudi, wakati alipokuwa mzee sana, watumishi wake walimfunika kwa mablanketi, lakini hata hivyo, hakuweza kupata joto. Kwa hivyo wakamwambia, “Bwana wetu mfalme, afadhali tukutafutie msichana akutumikie na kukutunza; alale pamoja nawe kusudi akupatie joto.” Basi, wakatafutatafuta msichana mzuri kote nchini Israeli. Akapatikana msichana mmoja mzuri aitwaye Abishagi, Mshunami; wakamleta kwa mfalme. Msichana huyo, alikuwa mzuri sana. Basi, akaanza kumtumikia na kumtunza mfalme; lakini mfalme hakulala naye. Wakati huo, Adoniya, mwana wa Daudi na Hagithi, akaanza kujigamba kwamba yeye ndiye atakayekuwa mfalme. Basi, akajitayarishia magari ya kukokotwa, wapandafarasi na wapiga mbio hamsini wa kumtangulia na kumshangilia. Lakini baba yake, Daudi, hakuwa amemkemea mwanawe hata mara moja na kumwuliza kwa nini alikuwa amefanya hivyo. Adoniya, ama kwa hakika, alikuwa mwenye sura ya kupendeza sana; na alikuwa amemfuata Absalomu kwa kuzaliwa. Adoniya akashauriana na Yoabu mwana wa Seruya, na kuhani Abiathari; nao wakamfuata na kumuunga mkono. Lakini kuhani Sadoki, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na nabii Nathani na Shimei, Rei pamoja na walinzi wa Daudi, hawakumuunga mkono Adoniya. Siku moja, Adoniya alitoa sadaka ya kondoo, ng'ombe na ndama wanono kwenye Jiwe la Nyoka, karibu na chemchemi iitwayo Enrogeli. Akawaalika kwenye karamu ya sadaka hiyo ndugu zake wote, yaani wana wengine wa mfalme, na watumishi wote wa mfalme waliokuwa wa kabila la Yuda. Lakini, nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Solomoni ndugu yake hakuwaalika. Hapo, Nathani akamwendea Bathsheba mama yake Solomoni, akamwuliza, “Je, hujasikia kwamba Adoniya, mwanawe Hagithi, amejinyakulia mamlaka ya ufalme na bwana wetu Daudi hana habari? Basi, kama ukitaka kuyaokoa maisha yako na ya mwanao Solomoni, nakushauri hivi: Mwendee mfalme Daudi, umwulize, ‘Je, bwana wangu mfalme, hukuniapia mimi mtumishi wako ukisema, “Mwana wako Solomoni atatawala mahali pangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?” Imekuwaje basi, sasa Adoniya anatawala?’ Na utakapokuwa bado unaongea na mfalme, mimi nitaingia na kuyathibitisha maneno yako.” Basi, Bathsheba alimwendea mfalme chumbani mwake (wakati huo mfalme alikuwa mzee sana, naye Abishagi, Mshunami alikuwa akimhudumia). Bathsheba aliinama, akamsujudia mfalme, naye mfalme akamwuliza, “Unataka nini?” Bathsheba akamjibu, “Bwana wangu, uliniapia mimi mtumishi wako mbele ya Bwana Mungu wako, ukisema: ‘Mwana wako Solomoni atatawala baada yangu, na ataketi juu ya kiti changu cha enzi.’ Sasa, tazama, Adoniya anatawala ingawa wewe bwana wangu mfalme hujui kuhusu hayo. Ametoa sadaka ya ng'ombe, ya vinono, na kondoo wengi, na kuwaita wana wote wa mfalme, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini mtumishi wako Solomoni hakumkaribisha. Na sasa, bwana wangu mfalme, Waisraeli wote wanakungojea, ili uwaambie yule atakayeketi juu ya kiti chako baada yako, bwana wangu mfalme. La sivyo, itatokea ya kwamba, wakati ambapo wewe bwana wangu, mfalme, utakapofariki mimi pamoja na mwanangu Solomoni tutahesabika kama wenye hatia.” Wakati Bathsheba alipokuwa akizungumza na mfalme, nabii Nathani aliingia ikulu. Nao watu wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Naye alipomfikia mfalme, alimwinamia mfalme mpaka uso ukafika chini udongoni. Ndipo Nathani aliposema, “Bwana wangu, je, ulisema, ‘Adoniya atatawala baada yangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?’ Kwa maana leo ameteremka, akatoa sadaka ya ng'ombe, vinono na kondoo wengi na amewakaribisha wana wa mfalme, Yoabu jemadari wa jeshi, na kuhani Abiathari, na, tazama, wanakula na kunywa mbele yake, na kusema, ‘Uishi mfalme Adoniya!’ Lakini hakunialika mimi, mtumishi wako wala kuhani Sadoki, wala Benaya mwana wa Yehoyada na mtumishi wako Solomoni. Je, yote haya umeyafanya wewe bwana wangu, mfalme, bila kuwaambia watumishi wako mtu atakayekaa juu ya kiti chako cha enzi baada yako?” Naye mfalme Daudi akajibu, “Niitie Bathsheba.” Bathsheba alimwendea mfalme na kusimama mbele yake. Halafu mfalme aliapa akisema, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, aliyekomboa roho yangu katika taabu nyingi, kama nilivyokuapia mbele za Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nikisema, ‘Mwanao Solomoni atatawala baada yangu, na kwamba atakaa juu ya kiti changu cha enzi badala yangu,’ ndivyo nitakavyofanya leo.” Ndipo Bathsheba alipoinama mpaka chini, akamsujudia mfalme, na kusema “Bwana wangu, mfalme Daudi, aishi milele!” Kisha mfalme Daudi akasema, “Niitie kuhani Sadoki, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada.” Nao wakamjia mfalme. Naye mfalme akawaambia, “Nenda na watumishi wangu mimi bwana wako, umpandishe mwanangu Solomoni juu ya nyumbu wangu, umpeleke Gihoni; halafu umruhusu kuhani Sadoki na nabii Nathani wampake mafuta kuwa mfalme wa Israeli; baadaye pigeni tarumbeta na kusema, ‘Mfalme Solomoni aishi!’ Nanyi mtamfuata, naye atakuja na kuketi juu ya kiti changu cha enzi badala yangu; nami nimemteua kuwa mtawala juu ya Israeli na juu ya Yuda.” Ndipo Benaya mwana wa Yehoyada alipomjibu mfalme, “Amina! Bwana Mungu wa bwana wangu mfalme, na anene vivyo hivyo. Kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa na bwana wangu mfalme, awe pia na Solomoni, na akikuze kiti chake cha enzi kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi.” Basi, kuhani Sadoki, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada, na Wakerethi na Wapelethi, wote walishuka wakampandisha Solomoni kwenye nyumbu wa mfalme Daudi, na kumpeleka mpaka Gihoni. Kisha kuhani Sadoki alichukua pembe za mafuta kutoka hemani na kumpaka mafuta Solomoni kuwa mfalme. Kisha walipiga tarumbeta; na watu wote wakasema, “Aishi mfalme Solomoni!” Halafu watu wote walimfuata, wakipiga mazomari, wakafurahi kwa shangwe kubwa, hata nchi ikatikisika kwa sauti zao. Basi, Adoniya pamoja na wageni waliokuwa naye walisikia hao watu walipomaliza sherehe. Naye Yoabu aliposikia sauti ya tarumbeta alisema, “Makelele hayo mjini ni ya nini?” Alipokuwa akisema, kumbe, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akaingia; kisha Adoniya akasema, “Karibu, kwani wewe u mtu mwema; unaleta habari njema.” Ndipo Yonathani alipomjibu Adoniya, “Hapana, kwa sababu mfalme Daudi amemtawaza Solomoni kuwa mfalme; naye mfalme amempeleka pamoja na kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada na Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme, kisha kuhani Sadoki na nabii Nathani wamemtia mafuta kuwa mfalme kule Gihoni; halafu wametoka hapo wakifurahi; ndicho kisa cha makelele hayo unayosikia. Sasa Solomoni anaketi juu ya kiti cha kifalme. Zaidi ya hayo, watumishi wa mfalme walikuja kumpongeza bwana wetu mfalme Daudi wakisema, ‘Mungu wako alifanye jina la Solomoni kuwa maarufu kuliko lako; pia akikuze kiti chake cha enzi kuliko kiti chako.’ Halafu mfalme akainama kitandani, na kuomba akisema, ‘Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, ambaye amemfanya mzawa wangu kuwa mfalme mahali pangu, na ambaye amenipa maisha hata nimeyaona haya.’” Basi, wageni wa Adoniya wakaogopa sana, wakaondoka na kutawanyika. Naye Adoniya, kwa kuwa alimwogopa Solomoni, akakimbilia katika hema la Mwenyezi-Mungu akazishika pembe za madhabahu apate kusalimika. Mfalme Solomoni akapata habari kwamba Adoniya alikuwa amekimbilia hemani, na kwamba anashikilia pembe za madhabahu akisema, “Sitaondoka hapa mpaka mfalme Solomoni atakaponihakikishia kwamba hataamuru niuawe.” Mfalme Solomoni akasema, “Nikimwona kuwa mwaminifu basi, hatapata madhara yoyote. Lakini nikimwona kuwa mwovu, lazima afe.” Basi, mfalme Solomoni akaagiza Adoniya aitwe kutoka hemani, aje kwake. Adoniya akafika mbele ya mfalme, akainama kwa heshima. Mfalme akamwambia, “Nenda zako nyumbani.”

1 Wafalme 1:1-53 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate moto. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate moto. Basi wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote mwa Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. Naye kijana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; walakini mfalme hakumjua. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akatakabari, akasema, Mimi nitakuwa mfalme. Akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, na watu hamsini wapige mbio mbele yake. Tena baba yake hakumchukiza wakati wo wote kwa kusema, Mbona umefanya hivi? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu. Akashauriana na Yoabu, mwana wa Seruya, na Abiathari, kuhani; nao wakamsaidia Adonia, wakamfuata. Ila Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Nathani, nabii, na Shimei, na Rei, na mashujaa wa Daudi, hao hawakuwa pamoja na Adonia. Adonia akachinja kondoo, na ng’ombe, na vinono, karibu na jiwe la Zohelethi, lililo karibu na chemchemi Rogeli; akawaita ndugu zake wote, wana wa mfalme, na watu wote wa Yuda, watumishi wa mfalme; ila Nathani, nabii, na Benaya, na mashujaa, na Sulemani nduguye, hakuwaita hao. Ndipo Nathani akamwambia Bath-sheba, mamaye Sulemani, akasema, Je! Hukusikia ya kuwa Adonia, mwana wa Hagithi, anamiliki, na bwana wetu Daudi hana habari? Haya basi, nikupe shauri, tafadhali, upate kuiokoa roho yako, na roho ya mwanao Sulemani. Enenda uingie ndani kwa mfalme Daudi, ukamwambie, Je! Hukuniapia mimi mjakazi wako, Ee mfalme, bwana wangu, kusema, Hakika yake Sulemani mwana wako atamiliki baada yangu, na kuketi katika kiti changu cha enzi? Mbona basi anamiliki Adonia? Tazama, wakati ule utakapokuwa katika kusema na mfalme, mimi nami nitaingia nyuma yako, na kuyahakikisha maneno yako. Basi Bath-sheba akaingia ndani kwa mfalme, ndani ya chumba chake; naye mfalme alikuwa mzee sana; na Abishagi, Mshunami, alikuwa akimtumikia mfalme. Bath-sheba akainama, akamsujudia mfalme. Naye mfalme akamwuliza, Wataka nini? Akamwambia, Bwana wangu, uliniapia mimi mjakazi wako kwa BWANA, Mungu wako, ya kwamba, bila shaka Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, yeye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi. Na sasa, angalia, Adonia anamiliki; na wewe, bwana wangu mfalme, huna habari. Tena amechinja ng’ombe, na vinono, na kondoo tele, na kuwaita wana wa mfalme wote pia, na Abiathari, kuhani, na Yoabu, jemadari wa jeshi. Ila Sulemani, mtumishi wako, huyu hakumwita. Ee mfalme, bwana wangu, macho ya Israeli wote yanakuelekea wewe, kwamba uwaambie ni nani atakayeketi katika kiti chako cha enzi baada yako, Ee mfalme, bwana wangu. Ama sivyo itakuwa, bwana wangu mfalme atakapolala pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Sulemani tutahesabiwa kuwa wahalifu. Basi tazama, alipokuwa katika kusema na mfalme, Nathani, nabii, aliingia. Wakamwambia mfalme wakasema, Tazama, Nathani, nabii. Naye alipoingia ndani mbele ya mfalme, akamsujudia kifudifudi. Nathani akasema, Ee mfalme, bwana wangu, je! Wewe umesema ya kwamba, Adonia atamiliki baada yangu, ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi? Maana leo ameshuka, na kuchinja ng’ombe, na vinono, na kondoo tele, naye amewaita wana wote wa mfalme, na majemadari wa jeshi, na Abiathari, kuhani; na tazama, wanakula na kunywa mbele yake, wakisema, Na aishi mfalme Adonia! Walakini mimi, mimi mtumishi wako, na Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Sulemani, mtumishi wako, hakutuita sisi. Je! Bwana wangu mfalme ndiye aliyelitenda jambo hili, bila kutujulisha sisi watumishi wako ni nani atakayeketi katika kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme baada yake? Ndipo mfalme Daudi akajibu, akasema, Niitieni Bath-sheba. Basi akaingia ndani kwa mfalme, akasimama mbele ya mfalme. Naye mfalme akaapa, akasema, BWANA aishivyo, aliyenikomboa roho yangu katika shida zote, hakika yake nitafanya leo kama vile nilivyokuapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli, nikasema, Kwa yakini Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, naye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi badala yangu. Ndipo Bath-sheba akainama kifudifudi, akamsujudia mfalme, akasema, Bwana wangu mfalme Daudi na aishi milele. Naye mfalme Daudi akasema, Niitie Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada. Nao wakaingia ndani mbele ya mfalme. Naye mfalme akawaambia, Twaeni pamoja nanyi watumishi wa bwana wenu, mkampandishe Sulemani mwanangu juu ya nyumbu wangu mimi mkamtelemshe mpaka Gihoni; kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na wamtie mafuta huko, awe mfalme juu ya Israeli; kapigeni panda, mkaseme, Mfalme Sulemani na aishi! Kisha pandeni juu nyuma yake, naye atakuja ili aketi katika kiti changu cha enzi; kwa maana atakuwa mfalme badala yangu; ndiye niliyemweka awamiliki Israeli na Yuda. Basi Benaya, mwana wa Yehoyada, akamjibu mfalme, akasema, Amina; BWANA, Mungu na bwana wangu mfalme, na aseme vivyo hivyo. Kama vile BWANA alivyokuwa pamoja na bwana wangu mfalme, kadhalika na awe pamoja na Sulemani, na kufanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi. Basi wakashuka Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha Sulemani juu ya nyumbu wa mfalme Daudi, wakampeleka mpaka Gihoni. Na Sadoki, kuhani, akatwaa ile pembe ya mafuta katika Hema, akamtia Sulemani mafuta. Nao wakapiga panda; na watu wote wakasema, Mfalme Sulemani na aishi! Kisha watu wote wakapanda juu nyuma yake, watu wakapiga mazomari, wakafurahi furaha kubwa mno, hata nchi ikapasuka kwa sauti zao. Basi Adonia, na wageni wote waliokuwa pamoja naye, wakasikia hayo walipokuwa wamekwisha kula. Naye Yoabu aliposikia sauti ya panda alisema, Za nini kelele hizi za mji uliotaharuki? Naye alipokuwa katika kunena, tazama Yonathani, mwana wa Abiathari kuhani, akafika. Naye Adonia akasema, Karibu; maana wewe u mtu mwema, unaleta habari njema. Naye Yonathani akajibu, akamwambia Adonia, Hakika bwana wetu mfalme Daudi amemtawaza Sulemani. Tena mfalme alipeleka pamoja naye Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha juu ya nyumbu wa mfalme. Kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, wakamtia mafuta huko Gihoni, ili awe mfalme. Nao wamepanda juu kutoka huko wakifurahi, hata mji ukavuma. Ndizo kelele zile mlizozisikia. Na tena, Sulemani ameketi katika kiti cha enzi cha ufalme. Na tena, watumishi wa mfalme walifika, ili wambariki bwana wetu mfalme Daudi, wakisema, Mungu wako na alikuze jina la Sulemani kuliko jina lako, na kukifanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti chako. Naye mfalme akainama chini juu ya kitanda chake. Na tena, mfalme akasema hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenipa leo hivi mtu wa kuketi katika kiti changu cha enzi, nayo macho yangu yakiwa yanaona hayo. Ndipo wageni wote waliokuwa pamoja na Adonia wakaogopa, wakaondoka, wakaenda zao kila mtu njia yake. Adonia naye akaogopa mbele ya Sulemani; akaondoka, akaenda, akazishika pembe za madhabahu. Akaambiwa Sulemani, kusema, Tazama, Adonia amwogopa mfalme Sulemani; kwani, tazama, amezishika pembe za madhabahu, akisema, Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hataniua mimi mtumwa wake kwa upanga. Akasema Sulemani, Akionekana kuwa mtu wa kweli, hata unywele mmoja wake hautaanguka chini; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa. Basi mfalme Sulemani akatuma watu, wakamtelemsha toka madhabahuni. Naye akaja, akamwinamia mfalme Sulemani; naye Sulemani akamwambia, Enenda nyumbani kwako.