1 Yohane 5:13-21
1 Yohane 5:13-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Nawaandikieni mpate kujua kwamba mnao uhai wa milele nyinyi mnaoamini kwa jina la Mwana wa Mungu. Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya matakwa yake, yeye hutusikiliza. Yeye hutusikiliza kila tunapomwomba; na kwa vile tunajua kwamba yeye hutusikiliza kila tunapomwomba, twajua pia kwamba hutupatia yote tunayomwomba. Mtu akimwona ndugu yake ametenda dhambi isiyompeleka kwenye kifo, anapaswa kumwombea kwa Mungu, naye Mungu atampatia uhai. Nasema jambo hili kuhusu wale waliotenda dhambi ambazo si za kifo. Lakini ipo dhambi yenye kumpeleka mtu kwenye kifo, nami sisemi kwamba mnapaswa kumwomba Mungu kwa ajili ya hiyo. Kila tendo lisilo adilifu ni dhambi, lakini kuna dhambi isiyompeleka mtu kwenye kifo. Tunajua kwamba kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, kwa sababu Mwana wa Mungu humlinda salama, na yule Mwovu hawezi kumdhuru. Tunajua kwamba sisi ni wake Mungu ingawa ulimwengu wote unatawaliwa na yule Mwovu. Twajua pia kwamba Mwana wa Mungu amekuja, akatupa elimu ili tumjue Mungu wa kweli; tuishi katika muungano na Mungu wa kweli – katika muungano na Mwanae, Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na huu ndio uhai wa milele. Watoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu!
1 Yohane 5:13-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu. Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tunapoomba chochote, tunajua kwamba tumetimiziwa zile haja tulizomwomba. Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo. Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti. Tunajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi. Tunajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu. Nasi tunajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele. Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu kutoka kwa sanamu.
1 Yohane 5:13-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu. Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo. Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti. Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi. Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu. Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele. Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.
1 Yohane 5:13-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nawaandikia mambo haya ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu ili mpate kujua ya kuwa mnao uzima wa milele. Huu ndio ujasiri tulio nao tunapomkaribia Mungu, kwamba kama tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Nasi kama tunajua atusikia, lolote tuombalo, tunajua ya kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba. Kama mtu akimwona ndugu yake akitenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo. Ninamaanisha wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo. Jambo lolote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti. Tunajua ya kuwa yeye aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, bali aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hawezi kumdhuru. Sisi twajua kuwa tu watoto wa Mungu na ya kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu. Nasi pia twajua ya kwamba Mwana wa Mungu amekuja, naye ametupa sisi ufahamu ili tupate kumjua yeye aliye Kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye Kweli, yaani, ndani ya Yesu Kristo Mwanawe. Yeye ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele. Watoto wapendwa, jilindeni nafsi zenu kutokana na sanamu. Amen.