1 Yohane 1:1-10
1 Yohane 1:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Tunawajulisha lile lililokuwepo tangu mwanzo, lile tulilosikia, ambalo tumeliona kwa macho yetu, ambalo tumelitazama na kuligusa kwa mikono yetu, kuhusu Neno la uzima. Uzima huo ulidhihirishwa; nasi tumeuona na kuushuhudia, nasi twawatangazia uzima wa milele, ambao ulikuwa pamoja na Baba, nao ukadhihirishwa kwetu. Twawatangazia lile tuliloliona na kulisikia, ili nanyi mwe na ushirika nasi. Na ushirika wetu hasa ni pamoja na Baba na Mwanawe, Yesu Kristo. Tunaandika mambo haya ili furaha yetu ipate kuwa timilifu. Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lolote. Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli. Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.
1 Yohane 1:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Habari hii yahusu Neno la uhai lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe. Uhai huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uhai huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu. Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni nyinyi pia, ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo. Tunawaandikia nyinyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike. Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake. Tukisema kwamba tuna umoja naye, na papo hapo tunaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo wala hatuishi kwa ukweli kwa maneno na matendo. Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi, tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe, na ukweli haumo ndani yetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote. Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.
1 Yohane 1:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kuhusu Neno la uzima; (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena tunashuhudia, na kuwahubiria ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu); hilo tuliloliona na kulisikia, tunawahubiria na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo. Na haya tunayaandika, ili furaha yetu itimizwe. Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lolote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba tunashirikiana naye, huku tukienenda katika giza, tunasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda katika nuru, kama yeye alivyo katika nuru, tunashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe, wala kweli haimo ndani yetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kututakasa na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, tunamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo ndani yetu.
1 Yohane 1:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima; (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu); hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo. Na haya twayaandika, ili furaha yetu itimizwe. Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.