1 Wakorintho 9:9-18
1 Wakorintho 9:9-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Imeandikwa katika sheria: “Usimfunge kinywa ng'ombe anapopura nafaka.” Je, ndio kusema Mungu anajishughulisha na ng'ombe? Je, hakuwa anatufikiria sisi aliposema hivyo? Naam, haya yaliandikwa kwa ajili yetu; maana yule anayelima na yule anayevuna, wote wawili wana haki ya kutumaini kupata sehemu ya mavuno. Ikiwa sisi tumepanda mbegu ya kiroho kati yenu, je, ni jambo kubwa tukichuma kwenu faida ya kidunia? Ikiwa wengine wanayo haki ya kutazamia hayo kutoka kwenu, je, sisi hatuna haki zaidi kuliko hao? Lakini, sisi hatukuitumia haki hiyo. Badala yake, tumestahimili kila kitu ili tusiiwekee kizuizi chochote Habari Njema ya Kristo. Je, hamjui kwamba wanaotumikia hekaluni hupata chakula chao hekaluni, na kwamba wanaotoa sadaka madhabahuni hupata sehemu ya hiyo sadaka? Bwana aliagiza vivyo hivyo; wahubiri wa Habari Njema wapate riziki zao kutokana nayo. Lakini, mimi sikutumia hata mojawapo ya haki hizo. Na wala siandiki nijipatie haki hizo; kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kumfanya yeyote aone kwamba najisifu bure. Ikiwa ninaihubiri injili, hilo si jambo la kujivunia; hilo ni jukumu nililopewa. Na, ole wangu kama sitaihubiri injili! Ningekuwa nimeichagua kazi hii kwa hiari, basi, ningetazamia malipo; lakini maadamu naifanya ikiwa ni wajibu, hiyo ina maana kwamba ni jukumu nililopewa nitekeleze. Mshahara wangu ni kitu gani, basi? Mshahara wangu ni fursa ya kuihubiri Habari Njema bure, bila kudai haki ninazostahili kwa kuihubiri.
1 Wakorintho 9:9-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana katika Torati ya Musa imeandikwa, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Je! Hapo Mungu aangalia mambo ya ng'ombe? Au yamkini anena hayo kwa ajili yetu? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu; kwa kuwa alimaye nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini, naye apuraye nafaka ni haki yake kutumaini kupata sehemu yake. Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini? Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo. Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiayo madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili. Lakini mimi sikutumia mambo hayo hata moja. Wala siyaandiki hayo ili iwe hivyo kwangu mimi; maana ni heri nife kuliko mtu awaye yote abatilishe huku kujisifu kwangu. Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili. Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa ninapohubiri, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.
1 Wakorintho 9:9-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana katika torati ya Musa imeandikwa, Usimfunge kinywa ng’ombe apurapo nafaka. Je! Hapo Mungu aangalia mambo ya ng’ombe? Au yamkini anena hayo kwa ajili yetu? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu; kwa kuwa alimaye nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini, naye apuraye nafaka ni haki yake kutumaini kupata sehemu yake. Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini? Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo. Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili. Lakini mimi sikutumia mambo hayo hata moja. Wala siyaandiki hayo ili iwe hivyo kwangu mimi; maana ni heri nife kuliko mtu awaye yote abatilishe huku kujisifu kwangu. Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili. Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.
1 Wakorintho 9:9-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa maana imeandikwa katika Sheria ya Mose: “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka.” Je, Mungu hapa anahusika na ngʼombe? Je, Mungu hasemi haya hasa kwa ajili yetu? Hakika yameandikwa kwa ajili yetu, kwa sababu mtu anapolima na mpuraji akapura nafaka, wote wanapaswa kufanya hivyo wakiwa na tumaini la kushiriki mavuno. Je, ikiwa sisi tulipanda mbegu ya kiroho miongoni mwenu, itakuwa ni jambo kubwa iwapo tutavuna vitu vya mwili kutoka kwenu? Kama wengine wana haki ya kupata msaada kutoka kwenu, isingepasa tuwe na haki hiyo hata zaidi? Lakini sisi hatukutumia haki hii. Kinyume chake, tunavumilia kila kitu ili tusije tukazuia Injili ya Kristo. Je, hamjui kwamba, watu wafanyao kazi hekaluni hupata chakula chao kutoka hekaluni, nao wale wahudumiao madhabahuni hushiriki kile kitolewacho madhabahuni? Vivyo hivyo, Bwana ameamuru kwamba wale wanaohubiri Injili wapate riziki yao kutokana na Injili. Lakini sijatumia hata mojawapo ya haki hizi. Nami siandiki haya nikitumaini kwamba mtanifanyia mambo hayo. Heri nife kuliko mtu yeyote kuninyima huku kujisifu kwangu. Lakini ninapohubiri Injili siwezi kujisifu maana ninalazimika kuhubiri. Ole wangu nisipoihubiri Injili! Nikihubiri kwa hiari, ninayo thawabu. Lakini kama si kwa hiari, basi ninachofanya ni kutekeleza tu uwakili niliowekewa. Basi je, thawabu yangu ni nini? Thawabu yangu ni hii: Ya kwamba katika kuhubiri Injili niitoe bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.