1 Wakorintho 9:1-14
1 Wakorintho 9:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Je, mimi si mtu huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Je, nyinyi si matokeo ya kazi yangu kwa ajili ya Bwana? Hata kama kwa watu wengine mimi si mtume, lakini walau kwenu nyinyi mimi ni mtume. Nyinyi ni uthibitisho wa utume wangu kwa sababu ya kuungana kwenu na Bwana. Hoja yangu kwa wale wanaonipinga ndiyo hii: Je, hatuna haki ya kula na kunywa? Je, hatuna ruhusa kumchukua mke Mkristo katika ziara zetu, kama vile wafanyavyo mitume wengine, ndugu zake Bwana, na pia Kefa? Au ni mimi tu na Barnaba ambao tunapaswa kujipatia maslahi yetu kwa kufanya kazi? Je, mwanajeshi gani anayelipia utumishi wake jeshini? Mkulima gani asiyekula matunda ya shamba lake la mizabibu? Mchungaji gani asiyekunywa maziwa ya mifugo yake? Je, nasema mambo haya kibinadamu tu? Je, sheria nayo haisemi hivyo? Imeandikwa katika sheria: “Usimfunge kinywa ng'ombe anapopura nafaka.” Je, ndio kusema Mungu anajishughulisha na ng'ombe? Je, hakuwa anatufikiria sisi aliposema hivyo? Naam, haya yaliandikwa kwa ajili yetu; maana yule anayelima na yule anayevuna, wote wawili wana haki ya kutumaini kupata sehemu ya mavuno. Ikiwa sisi tumepanda mbegu ya kiroho kati yenu, je, ni jambo kubwa tukichuma kwenu faida ya kidunia? Ikiwa wengine wanayo haki ya kutazamia hayo kutoka kwenu, je, sisi hatuna haki zaidi kuliko hao? Lakini, sisi hatukuitumia haki hiyo. Badala yake, tumestahimili kila kitu ili tusiiwekee kizuizi chochote Habari Njema ya Kristo. Je, hamjui kwamba wanaotumikia hekaluni hupata chakula chao hekaluni, na kwamba wanaotoa sadaka madhabahuni hupata sehemu ya hiyo sadaka? Bwana aliagiza vivyo hivyo; wahubiri wa Habari Njema wapate riziki zao kutokana nayo.
1 Wakorintho 9:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Je! Mimi siko huru? Mimi si mtume? Mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Ninyi si kazi yangu katika Bwana? Kwa maana ikiwa mimi si mtume kwa wengine, lakini ni mtume kwenu ninyi; kwa maana ninyi ndinyi mhuri wa utume wangu katika Bwana. Hilo ndilo jawabu langu kwa wale wanaoniuliza. Je! Hatuna uwezo wa kula na kunywa? Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu, kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa? Au je! Ni mimi peke yangu na Barnaba tusio na uwezo wa kutofanya kazi? Ni askari gani aendaye vitani wakati wowote kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi? Je! Ninanena hayo kwa kibinadamu? Au torati nayo haisemi yayo hayo? Kwa maana katika Torati ya Musa imeandikwa, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Je! Hapo Mungu aangalia mambo ya ng'ombe? Au yamkini anena hayo kwa ajili yetu? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu; kwa kuwa alimaye nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini, naye apuraye nafaka ni haki yake kutumaini kupata sehemu yake. Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini? Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo. Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiayo madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.
1 Wakorintho 9:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Je! Mimi si huru? Mimi si mtume? Mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Ninyi si kazi yangu katika Bwana? Kwa maana ikiwa mimi si mtume kwa wengine, lakini ni mtume kwenu ninyi; kwa maana ninyi ndinyi muhuri ya utume wangu katika Bwana. Hilo ndilo jawabu langu kwa wale wanaoniuliza. Je! Hatuna uwezo wa kula na kunywa? Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu, kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa? Au je! Ni mimi peke yangu na Barnaba tusio na uwezo wa kutokufanya kazi? Ni askari gani aendaye vitani wakati wo wote kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi? Je! Ninanena hayo kwa kibinadamu? Au torati nayo haisemi yayo hayo? Kwa maana katika torati ya Musa imeandikwa, Usimfunge kinywa ng’ombe apurapo nafaka. Je! Hapo Mungu aangalia mambo ya ng’ombe? Au yamkini anena hayo kwa ajili yetu? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu; kwa kuwa alimaye nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini, naye apuraye nafaka ni haki yake kutumaini kupata sehemu yake. Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini? Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo. Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.
1 Wakorintho 9:1-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Je, mimi si huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Isa, Bwana wetu? Je, ninyi si matunda ya kazi yangu katika Bwana? Hata kama mimi si mtume kwa wengine, hakika mimi ni mtume kwenu, kwa maana ninyi ni muhuri wa utume wangu katika Bwana Isa. Huu ndio utetezi wangu kwa hao wanaokaa kunihukumu. Je, hatuna haki ya kula na kunywa? Je, hatuna haki ya kusafiri na mke anayeamini, kama wanavyofanya mitume wengine na ndugu zake Bwana Isa na Kefa? Au ni mimi na Barnaba tu inatubidi kufanya kazi ili tuweze kupata mahitaji yetu? Ni askari yupi aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye shamba la mizabibu na asile matunda yake? Ni nani achungaye kundi na asipate maziwa yake. Je, nasema mambo haya katika mtazamo wa kibinadamu tu? Je, Torati haisemi vivyo hivyo? Kwa maana imeandikwa katika Torati ya Musa: “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka.” Je, Mungu hapa anahusika na ng’ombe? Je, Mungu hasemi haya hasa kwa ajili yetu? Hakika yameandikwa kwa ajili yetu, kwa sababu mtu anapolima na mpuraji akapura nafaka, wote wanapaswa kufanya hivyo wakiwa na tumaini la kushiriki mavuno. Je, ikiwa sisi tulipanda mbegu ya kiroho miongoni mwenu, itakuwa ni jambo kubwa iwapo tutavuna vitu vya mwili kutoka kwenu? Kama wengine wana haki ya kupata msaada kutoka kwenu, isingepasa tuwe na haki hiyo hata zaidi? Lakini sisi hatukutumia haki hii. Kinyume chake, tunavumilia kila kitu ili tusije tukazuia Injili ya Al-Masihi. Je, hamjui kwamba, watu wafanyao kazi hekaluni hupata chakula chao kutoka hekaluni, nao wale wahudumiao madhabahuni hushiriki kile kitolewacho madhabahuni? Vivyo hivyo, Bwana Isa ameamuru kwamba wale wanaohubiri Injili wapate riziki yao kutokana na Injili.