1 Wakorintho 8:1-6
1 Wakorintho 8:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Yahusu sasa vyakula vilivyotambikiwa sanamu: Tunajua kwamba sisi sote tuna ujuzi, lakini ujuzi huo huwafanya watu wawe na majivuno; lakini mapendo hujenga. Anayefikiri kwamba anajua kitu, kwa kweli hajui chochote kama inavyompasa. Lakini anayempenda Mungu, huyo anajulikana naye. Kwa hiyo, kuhusu vyakula vilivyotambikiwa sanamu, twajua kwamba sanamu si kitu duniani; twajua kwamba Mungu ni mmoja tu. Hata kama viko vitu viitwavyo miungu duniani au mbinguni, na hata kama wako miungu na mabwana wengi, hata hivyo, kwetu sisi yuko Mungu mmoja tu; Baba, Muumba wa vyote, ambaye kwa ajili yake sisi tuko. Pia yuko Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa njia yake vitu vyote viliumbwa, na sisi twaishi kwa njia yake.
1 Wakorintho 8:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na kuhusu vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga. Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lolote bado, kama impasavyo kujua. Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo amejulikana naye. Basi kuhusu kuvila vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu. Kwa maana ijapokuwa wako waitwao miungu, ama mbinguni ama duniani, kama vile walivyoko miungu mingi na mabwana wengi; lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo.
1 Wakorintho 8:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na kwa habari ya vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga. Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua. Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo amejulikana naye. Basi kwa habari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu. Kwa maana ijapokuwa wako waitwao miungu, ama mbinguni ama duniani, kama vile walivyoko miungu mingi na mabwana wengi; lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo.
1 Wakorintho 8:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sasa kuhusu chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sisi sote tuna ujuzi.” Lakini ujuzi hujivuna, bali upendo hujenga. Mtu yeyote anayedhani kwamba anajua kitu, bado hajui kama impasavyo kujua. Lakini mtu ampendaye Mungu, hujulikana naye Mungu. Hivyo basi, kuhusu kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu: Tunajua kwamba “Sanamu si kitu chochote kabisa duniani,” na kwamba “Kuna Mungu mmoja tu.” Kwa kuwa hata kama wapo hao wanaoitwa miungu, kama wakiwa mbinguni au duniani (kama ilivyo kweli wapo “miungu” wengi na “mabwana” wengi), kwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi; na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa yeye vitu vyote vimekuwepo na kwa yeye tunaishi.