1 Wakorintho 7:1-7
1 Wakorintho 7:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Yahusu sasa mambo yale mliyoandika: Naam, ni vizuri kama mtu haoi; lakini kwa sababu ya hatari ya uzinzi, basi, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. Mume atimize wajibu alio nao kwa mkewe, naye mke atimize wajibu alio nao kwa mumewe. Mke hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mumewe anayo; hali kadhalika naye mume, hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mkewe anayo. Msinyimane haki zenu, isipokuwa kama mnaafikiana kufanya hivyo kwa kitambo tu, ili mpate nafasi nzuri ya kusali. Kisha rudianeni tena mara, ili Shetani asije akawajaribuni kwa sababu ya udhaifu wenu. Ninayowaambieni sasa ni mawaidha, si amri. Ningependa watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mmoja anacho kipaji chake kutoka kwa Mungu; mmoja kipaji hiki na mwingine kile.
1 Wakorintho 7:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi kuhusu mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkarudiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu. Lakini nasema hayo, kwa kutoa idhini yangu, si kwa amri. Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi.
1 Wakorintho 7:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu. Lakini nasema hayo, kwa kutoa idhini yangu, si kwa amri. Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi.
1 Wakorintho 7:1-7 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Basi kuhusu mambo yale mliyoyaandika: “Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke.” Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe. Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe. Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda, ili mweze kujitoa kwa maombi. Kisha mrudiane tena, ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi. Nasema haya kama ushauri na si amri. Laiti watu wangekuwa kama mimi nilivyo. Lakini kila mtu amepewa kipawa chake kutoka kwa Mungu, mmoja ana kipawa cha namna hii na mwingine ana cha namna ile.