1 Wakorintho 3:1-9
1 Wakorintho 3:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu mlio na huyo Roho. Nilipaswa kusema nanyi kama watu wa kidunia, kama watoto wachanga katika maisha ya Kikristo. Ilinibidi kuwalisheni kwa maziwa, na si kwa chakula kigumu, kwani hamkuwa tayari kukipokea. Hata sasa hamko tayari. Maana bado nyinyi ni watu wa kidunia. Je, si kweli kwamba bado uko wivu na ugomvi kati yenu? Mambo hayo yanaonesha wazi kwamba nyinyi bado ni watu wa kidunia, mnaishi mtindo wa kidunia. Mmoja wenu anaposema, “Mimi ni wa Paulo”, na mwingine, “Mimi ni wa Apolo”, je, hiyo haionyeshi kwamba mnaishi bado kama watu wa dunia hii tu? Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Sisi ni watumishi tu ambao tuliwaleteeni nyinyi imani. Kila mmoja wetu anafanya kazi aliyopewa na Bwana. Mimi nilipanda mbegu, Apolo akamwagilia maji; lakini aliyeiotesha mbegu ni Mungu. Wa maana si yule aliyepanda mbegu, au yule aliyemwagilia maji; wa maana ni Mungu aliyeiwezesha mbegu kuota. Yule aliyepanda na yule aliyemwagilia maji wote ni sawa, ingawa kila mmoja atapokea tuzo lake kufuatana na jitihada yake mwenyewe. Maana sisi ni ndugu, wafanyakazi pamoja na Mungu; na nyinyi ni shamba lake; nyinyi ni jengo lake.
1 Wakorintho 3:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Niliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe kulingana na taabu yake mwenyewe. Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.
1 Wakorintho 3:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.
1 Wakorintho 3:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwilini, kama watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa, wala si chakula kigumu, kwa kuwa hamkuwa tayari kwa hicho chakula. Naam, hata sasa hamko tayari. Ninyi bado ni watu wa mwilini. Kwa kuwa bado kuna wivu na magombano miongoni mwenu, je, ninyi si watu wa mwilini? Je, si mwaendelea kama watu wa kawaida? Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” na mwingine, “Mimi ni wa Apolo,” je, ninyi si wanadamu wa kawaida? Kwani, Apolo ni nani? Naye Paulo ni nani? Ni watumishi tu ambao kupitia wao mliamini, kama vile Bwana alivyompa kila mtu huduma yake. Mimi nilipanda mbegu, Apolo akatia maji, lakini Mungu ndiye aliikuza. Hivyo mwenye kupanda na mwenye kutia maji si kitu, bali Mungu peke yake ambaye huifanya ikue. Apandaye mbegu ana lengo sawa na yule atiaye maji na kila mmoja atalipwa kulingana na kazi yake. Kwa kuwa sisi tu watendakazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, jengo la Mungu.