1 Wakorintho 15:42-49
1 Wakorintho 15:42-49 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndivyo ilivyo kuhusu ufufuo wa wafu. Kama vile mbegu, mwili huzikwa ardhini ukiwa katika hali ya kuharibika, lakini hufufuliwa katika hali ya kutoharibika. Huzikwa katika hali duni, hufufuliwa katika hali tukufu; huzikwa katika hali dhaifu, hufufuliwa ukiwa wenye nguvu. Unapozikwa ni mwili wa kawaida, unapofufuliwa ni mwili wa kiroho. Kuna mwili wa kawaida na kutakuwa na mwili wa kiroho. Maana Maandiko yasema: “Mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe mwenye uhai;” lakini Adamu wa mwisho ni Roho awapaye watu uhai. Lakini unaotangulia kuwako si ule mwili wa kiroho, ila ule mwili wa kawaida, kisha ule mwili wa kiroho. Adamu wa kwanza aliumbwa kwa udongo, alitoka ardhini; mtu wa pili alitoka mbinguni. Wote walio wa dunia wako kama huyo mtu aliyeumbwa kwa udongo; wale walio wa mbinguni wako kama yule aliyetoka mbinguni. Kama vile tulivyofanana na yule aliyeumbwa kwa udongo, vivyo hivyo tutafanana na huyo aliyetoka mbinguni.
1 Wakorintho 15:42-49 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hivyo ndivyo ilivyo kwa kiyama ya wafu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutoharibika; hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu; hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko. Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa kiumbe aliye hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha. Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni. Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.
1 Wakorintho 15:42-49 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kadhalika na kiyama ya watu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika; hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu; hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko. Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha. Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni. Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.
1 Wakorintho 15:42-49 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati wa ufufuo wa wafu. Ule mwili wa kuharibika uliopandwa, utafufuliwa usioharibika, unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu, unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu, unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho. Kama kuna mwili wa asili, basi kuna mwili wa kiroho pia. Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima. Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho. Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni. Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni. Kama vile tulivyochukua mfano wa mtu wa ardhini, ndivyo tutakavyochukua mfano wa yule mtu aliyetoka mbinguni.