1 Wakorintho 15:1-11
1 Wakorintho 15:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Sasa, ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema niliyowahubirieni, nanyi mkaipokea na kusimama imara ndani yake. Kwa njia yake mnaokolewa, ikiwa mnayazingatia maneno niliyowahubirieni, na kama kuamini kwenu hakukuwa bure. Mimi niliwakabidhi nyinyi mambo muhimu sana ambayo mimi niliyapokea: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na Maandiko Matakatifu; kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kufuatana na Maandiko Matakatifu; kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili. Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya 500 kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa. Baadaye alimtokea Yakobo kisha akawatokea mitume wote. Baada ya wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama mtu aliyezaliwa kabla ya wakati. Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume, na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu. Lakini, kwa neema yake Mungu, nimekuwa kama nilivyo, na neema yake kwangu haikuwa bure. Mimi nimefanya kazi kuliko wote; si mimi hasa, ila ni neema ya Mungu ifanyayo kazi pamoja nami. Lakini hata hivyo, iwe wao ndio wahubirio au mimi nihubiriye, haidhuru, hiki ndicho tunachohubiri, na hiki ndicho mnachoamini.
1 Wakorintho 15:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile Injili niliyowahubiria; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiria isipokuwa mliamini bure. Kwa maana niliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo Maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo Maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Kumi na Wawili; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu nililiudhi kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nilizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Basi kama ni mimi, au kama ni wao, ndivyo tuhubirivyo na ndivyo mlivyoamini.
1 Wakorintho 15:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.
1 Wakorintho 15:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama. Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili. Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yasemavyo Maandiko, ya kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama yasemavyo Maandiko, na kwamba alimtokea Kefa, kisha akawatokea wale kumi na wawili. Baadaye akawatokea wale ndugu waumini zaidi ya 500 kwa pamoja, ambao wengi wao bado wako hai, ingawa wengine wamelala. Ndipo akamtokea Yakobo na kisha mitume wote. Mwisho wa wote, akanitokea mimi pia, ambaye ni kama aliyezaliwa si kwa wakati wake. Kwa maana mimi ndiye mdogo kuliko mitume wote, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami. Hivyo basi, kama ilikuwa mimi au wao, hili ndilo tunalohubiri, na hili ndilo mliloamini.