1 Wakorintho 13:8-13
1 Wakorintho 13:8-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nilisema kama mtoto mchanga, nilifahamu kama mtoto mchanga, nilifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.
1 Wakorintho 13:8-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Upendo hauna kikomo kamwe. Kama kuna vipaji vya kutangaza ujumbe wa Mungu, hivyo vitatoweka siku moja; kama ni vipaji vya kusema lugha ngeni, vitakoma; kama kuna elimu, nayo itapita. Maana ujuzi wetu si kamili, na kipaji chetu cha kutangaza neno la Mungu si kamili. Lakini kile kilicho kikamilifu kitakapofika, vyote visivyo vikamilifu vitatoweka. Nilipokuwa mtoto mchanga nilisema kitoto, nilifahamu kitoto, nilifikiri kitoto. Lakini sasa, maadamu mimi ni mtu mzima, mambo ya kitoto nimeyaacha. Tunachoona sasa ni kama tu sura hafifu katika kioo, lakini hapo baadaye tutaona uso kwa uso. Sasa ninajua kiasi fulani tu, lakini hapo baadaye nitajua yote kikamilifu, kama vile Mungu anavyonijua mimi. Sasa yanadumu haya matatu: Imani, tumaini na upendo; lakini lililo kuu kupita yote ni upendo.
1 Wakorintho 13:8-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.
1 Wakorintho 13:8-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu na tunatoa unabii kwa sehemu. Lakini ukamilifu ukija, yale yasiyo kamili hutoweka. Nilipokuwa mtoto, nilisema kama mtoto, niliwaza kama mtoto, nilifikiri kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima niliacha mambo ya kitoto. Kwa maana sasa tunaona taswira kama kwa kioo, lakini wakati huo tutaona wazi. Sasa nafahamu kwa sehemu, wakati huo nitafahamu kikamilifu, kama vile mimi ninavyofahamika kikamilifu. Basi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.