1 Wakorintho 13:1-13
1 Wakorintho 13:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Hata kama nikinena lugha za watu na hata za malaika, lakini kama sina upendo mimi nimekuwa tu kama sauti ya debe tupu au kengele. Tena, naweza kuwa na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, nikafahamu siri zote na kujua kila kitu; naweza kuwa na imani yote hata nikaweza kuihamisha milima, lakini kama sina upendo mimi si kitu. Nikitoa mali yangu yote na kuwapa maskini, na tena nikiutoa mwili wangu uchomwe, kama sina upendo hiyo hainifai chochote. Mwenye upendo huvumilia, hufadhili; mwenye upendo hana wivu, hajidai, wala hajivuni. Mwenye upendo hakosi adabu, hatafuti faida yake binafsi, wala hana wepesi wa hasira; haweki kumbukumbu ya mabaya, hafurahii uovu, bali hufurahia ukweli. Mwenye upendo huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote. Upendo hauna kikomo kamwe. Kama kuna vipaji vya kutangaza ujumbe wa Mungu, hivyo vitatoweka siku moja; kama ni vipaji vya kusema lugha ngeni, vitakoma; kama kuna elimu, nayo itapita. Maana ujuzi wetu si kamili, na kipaji chetu cha kutangaza neno la Mungu si kamili. Lakini kile kilicho kikamilifu kitakapofika, vyote visivyo vikamilifu vitatoweka. Nilipokuwa mtoto mchanga nilisema kitoto, nilifahamu kitoto, nilifikiri kitoto. Lakini sasa, maadamu mimi ni mtu mzima, mambo ya kitoto nimeyaacha. Tunachoona sasa ni kama tu sura hafifu katika kioo, lakini hapo baadaye tutaona uso kwa uso. Sasa ninajua kiasi fulani tu, lakini hapo baadaye nitajua yote kikamilifu, kama vile Mungu anavyonijua mimi. Sasa yanadumu haya matatu: Imani, tumaini na upendo; lakini lililo kuu kupita yote ni upendo.
1 Wakorintho 13:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nilisema kama mtoto mchanga, nilifahamu kama mtoto mchanga, nilifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.
1 Wakorintho 13:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.
1 Wakorintho 13:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo. Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu. Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote. Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu na tunatoa unabii kwa sehemu. Lakini ukamilifu ukija, yale yasiyo kamili hutoweka. Nilipokuwa mtoto, nilisema kama mtoto, niliwaza kama mtoto, nilifikiri kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima niliacha mambo ya kitoto. Kwa maana sasa tunaona taswira kama kwa kioo, lakini wakati huo tutaona wazi. Sasa nafahamu kwa sehemu, wakati huo nitafahamu kikamilifu, kama vile mimi ninavyofahamika kikamilifu. Basi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.