1 Wakorintho 12:4-31
1 Wakorintho 12:4-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho avitoaye ni mmoja. Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana anayetumikiwa ni mmoja. Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote. Kila mtu hupewa mwangaza wa Roho kwa faida ya wote. Roho humpa mmoja ujumbe wa hekima, na mwingine ujumbe wa elimu, apendavyo Roho huyohuyo. Roho huyohuyo humpa mmoja imani, na humpa mwingine kipaji cha kuponya; humpa mmoja kipaji cha kufanya miujiza, mwingine kipaji cha kusema ujumbe wa Mungu, mwingine kipaji cha kubainisha vipaji vitokavyo kwa Roho na visivyo vya Roho; humpa mmoja kipaji cha kusema lugha ngeni, na mwingine kipaji cha kuzifafanua. Hizo zote ni kazi za Roho huyohuyo mmoja, ambaye humpa kila mtu kipaji tofauti, kama apendavyo mwenyewe. Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na viungo hivyo vyote – ingawaje ni vingi – hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia kwa Kristo. Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja. Mwili hauna kiungo kimoja tu, bali una viungo vingi. Kama mguu ungejisemea: “Kwa kuwa mimi si mkono, basi mimi si mali ya mwili,” je, ungekoma kuwa sehemu ya mwili? La hasha! Kama sikio lingejisemea: “Kwa vile mimi si jicho, basi mimi si mali ya mwili,” je, kwa hoja hiyo lingekoma kuwa sehemu ya mwili? La! Kama mwili wote ungekuwa jicho, sikio lingekuwa wapi? Na kama mwili wote ungekuwa sikio, mtu angewezaje kunusa? Lakini kama ilivyo, Mungu alizipanga sehemu hizo tofauti katika mwili kama alivyopenda. Kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Ukweli ni kwamba, sehemu za mwili ni nyingi, lakini mwili ni mmoja. Basi, jicho haliwezi kuuambia mkono: “Sikuhitaji wewe,” wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: “Siwahitaji nyinyi.” Zaidi ya hayo, inaonekana kwamba sehemu zile za mwili zinazoonekana kuwa ni dhaifu ndizo zilizo muhimu zaidi. Tena, viungo vile tunavyovifikiria kuwa havistahili heshima kubwa, ndivyo tunavyovitunza kwa uangalifu zaidi; viungo vya mwili ambavyo havionekani kuwa vizuri sana, huhifadhiwa zaidi, ambapo viungo vingine havihitaji kushughulikiwa. Mungu mwenyewe ameuweka mwili katika mpango, akakipa heshima zaidi kiungo kile kilichopungukiwa heshima, ili kusiweko na utengano katika mwili, bali viungo vyote vishughulikiane. Kama kiungo kimoja kinaumia viungo vyote huumia pamoja nacho. Kiungo kimoja kikisifiwa viungo vingine vyote hufurahi pamoja nacho. Basi, nyinyi nyote ni mwili wa Kristo; kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo. Mungu ameweka katika kanisa: Kwanza mitume, pili manabii, tatu waalimu; kisha ameweka wale wenye kipaji cha kufanya miujiza, kuponya na kusaidia; viongozi na wenye kusema lugha ngeni. Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote ni wenye kipaji cha kufanya miujiza? Je, wote ni wenye kipaji cha kuponya? Je, wote ni wenye kipaji cha kusema lugha ngeni? Je, wote hufafanua lugha? Muwe basi, na tamaa ya kupata vipaji muhimu zaidi. Nami sasa nitawaonesheni njia bora zaidi kuliko hizi zote.
1 Wakorintho 12:4-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi kuna karama tofauti; bali Roho ni yeye yule. Tena kuna huduma tofauti, na Bwana ni yeye yule. Kisha kuna uwezo tofauti wa kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine fasiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wagiriki; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Unakuwa si wa mwili kwa sababu hiyo? Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si wa mwili; je! Linakuwa si la mwili kwa sababu hiyo? Kama mwili wote ukiwa jicho, kuko wapi kusikia? Kama wote ni sikio kuko wapi kunusa? Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka. Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja. Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vinahitajiwa zaidi. Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile tunavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana. Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa; ili kusiwe na mgawanyiko katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe. Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na kila mmoja wenu akiwa kiungo cha mwili huo. Na Mungu ameweka wengine katika kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, aina za usaidizi, maongozi na aina za lugha. Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri? Jitahidini sana kupata karama zilizo kuu. Na nitawaonesheni njia iliyo bora zaidi.
1 Wakorintho 12:4-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo? Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo? Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa? Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka. Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja. Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana. Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa; ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe. Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake. Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri? Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.
1 Wakorintho 12:4-31 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule. Kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni yule yule. Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote. Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya kwa huyo Roho mmoja. Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingine bado, tafsiri za lugha. Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo. Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi, navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja, vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja wote tulibatizwa katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wayunani, kama ni watumwa au watu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Basi mwili si kiungo kimoja, bali ni viungo vingi. Kama mguu ungesema, “Kwa kuwa mimi si mkono basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya huo mguu usiwe sehemu ya mwili. Na kama sikio lingesema, “Kwa kuwa mimi si jicho, basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya hilo sikio lisiwe sehemu ya mwili. Kama mwili wote ungelikuwa jicho, kusikia kungekuwa wapi? Au kama mwili wote ungelikuwa sikio, kunusa kungekuwa wapi? Lakini kama ilivyo, Mungu ameweka viungo katika mwili, kila kimoja kama alivyopenda. Kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Kama ulivyo, una viungo vingi, lakini mwili ni mmoja. Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sina haja nawe!” Wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu, “Sina haja na ninyi!” Lakini badala yake, vile viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu, ndivyo ambavyo ni vya muhimu sana. Navyo vile viungo tunavyoviona havina heshima, ndivyo tunavipa heshima maalum. Vile viungo vya mwili ambavyo havina uzuri, tunavipa heshima ya pekee; wakati vile viungo vyenye uzuri havihitaji utunzaji wa pekee. Lakini Mungu ameviweka pamoja viungo vya mwili na akavipa heshima zaidi vile vilivyopungukiwa, ili pasiwe na mafarakano katika mwili, bali viungo vyote vihudumiane kwa usawa kila kimoja na mwenzake. Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho, kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Sasa ninyi ni mwili wa Kristo na kila mmoja wenu ni sehemu ya huo mwili. Mungu ameweka katika kanisa, kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, pia karama za kuponya, karama za kusaidiana, karama za uongozi, aina mbalimbali za lugha. Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote wanatenda miujiza? Je, wote wana karama ya kuponya? Je, wote hunena kwa lugha mpya? Je, wote wanatafsiri? Basi tamanini sana karama zilizo kuu. Nami nitawaonyesha njia iliyo bora zaidi.