1 Wakorintho 12:1-11
1 Wakorintho 12:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, ndugu zangu, kuhusu karama za roho, sitaki mkose kufahamu. Mwajua ya kuwa mlipokuwa watu wa Mataifa, mlichukuliwa kufuata sanamu zisizonena, kama mlivyoongozwa. Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi kuna karama tofauti; bali Roho ni yeye yule. Tena kuna huduma tofauti, na Bwana ni yeye yule. Kisha kuna uwezo tofauti wa kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine fasiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.
1 Wakorintho 12:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, kuhusu vipaji vya kiroho, napenda mfahamu vizuri mambo haya: Mnajua kwamba, kabla ya kuongoka kwenu, mlitawaliwa na kupotoshwa na sanamu tupu. Basi, jueni kwamba mtu yeyote anayeongozwa na Roho wa Mungu hawezi kusema: “Yesu alaaniwe!” Hali kadhalika, mtu yeyote hawezi kusema: “Yesu ni Bwana,” asipoongozwa na Roho Mtakatifu. Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho avitoaye ni mmoja. Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana anayetumikiwa ni mmoja. Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote. Kila mtu hupewa mwangaza wa Roho kwa faida ya wote. Roho humpa mmoja ujumbe wa hekima, na mwingine ujumbe wa elimu, apendavyo Roho huyohuyo. Roho huyohuyo humpa mmoja imani, na humpa mwingine kipaji cha kuponya; humpa mmoja kipaji cha kufanya miujiza, mwingine kipaji cha kusema ujumbe wa Mungu, mwingine kipaji cha kubainisha vipaji vitokavyo kwa Roho na visivyo vya Roho; humpa mmoja kipaji cha kusema lugha ngeni, na mwingine kipaji cha kuzifafanua. Hizo zote ni kazi za Roho huyohuyo mmoja, ambaye humpa kila mtu kipaji tofauti, kama apendavyo mwenyewe.
1 Wakorintho 12:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, ndugu zangu, kwa habari ya karama za roho, sitaki mkose kufahamu. Mwajua ya kuwa mlipokuwa watu wa Mataifa, mlichukuliwa kufuata sanamu zisizonena, kama mlivyoongozwa. Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.
1 Wakorintho 12:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi ndugu zangu, kuhusu karama za rohoni, sitaki mkose kufahamu. Mnajua kwamba mlipokuwa watu wasiomjua Mungu, kwa njia moja au ingine mlishawishika na kupotoshwa mkielekezwa kwa sanamu zisizonena. Kwa hiyo nawaambieni ya kuwa hakuna mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu na alaaniwe.” Pia hakuna mtu awezaye kusema, “Yesu ni Bwana,” isipokuwa ameongozwa na Roho Mtakatifu. Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule. Kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni yule yule. Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote. Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya kwa huyo Roho mmoja. Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingine bado, tafsiri za lugha. Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo.