Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 11:17-34

1 Wakorintho 11:17-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Nikiwa bado nawapeni maagizo haya, siwezi hata kidogo kuwapa nyinyi hongera kuhusu haya yafuatayo: Mikutano yenu nyinyi waumini yaleta hasara zaidi kuliko faida. Awali ya yote, nasikia kwamba mnapokutana pamoja hutokea mafarakano kati yenu. Nami naamini kiasi, maana ni lazima fikira tofauti ziweko miongoni mwenu, ili wale walio thabiti wapate kutambulikana. Kweli mnakutana, lakini si kwa ajili ya kula Karamu ya Bwana! Maana mnapokula kila mmoja hukikalia chakula chake mwenyewe, hata hutokea kwamba baadhi yenu wana njaa, na wengine wamelewa! Je, hamwezi kula na kunywa nyumbani kwenu! Au je, mnalidharau kanisa la Mungu na kuwaaibisha hao wasio na kitu? Niwaambie nini? Niwasifu? La hasha! Si kuhusu jambo hili. Maana mimi nilipokea kwa Bwana yale maagizo niliyowaachieni: Kwamba, usiku ule Bwana Yesu alipotolewa, alitwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akasema: “Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa kunikumbuka.” Vivyo hivyo, baada ya kula, akatwaa kikombe cha divai, akasema: “Hiki ni kikombe cha agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu. Fanyeni hivi, kila mnapokunywa, kwa kunikumbuka.” Maana kila mnapokula mkate huu na kukinywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja. Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana. Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho; maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe. Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa. Kama tungejichunguza wenyewe vizuri hatungeadhibiwa hivyo. Lakini tunapohukumiwa na Bwana, tunafunzwa tuwe na nidhamu, ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu. Kwa hiyo, ndugu zangu, mnapokutana kula Karamu ya Bwana, kila mmoja amngoje mwenzake. Na kama kuna yeyote aliye na njaa, na ale nyumbani kwake, ili kukutana kwenu kusisababishe hukumu. Lakini, kuhusu yale mambo mengine, nitawapeni maelezo nitakapokuja.

1 Wakorintho 11:17-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara. Kwa maana kwanza mnapokutanika kanisani nasikia kuna migawanyiko kwenu; nami kwa kiasi fulani naamini; kwa maana lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu. Basi mnapokutanika pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana; kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo. Kwa maana mimi nilipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio wagonjwa na dhaifu, na watu kadhaa wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa. Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia. Kwa hiyo, ndugu zangu, mnapokutanika mpate kula, ngojaneni; mtu akiwa na njaa, na ale nyumbani kwake; msipate kukutanika kwa hukumu. Na hayo yaliyosalia nikija nitayatengeneza.

1 Wakorintho 11:17-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara. Kwa maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki; kwa maana lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu. Basi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana; kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo. Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa. Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia. Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojaneni; mtu akiwa na njaa, na ale nyumbani kwake; msipate kukutanika kwa hukumu. Na hayo yaliyosalia nijapo nitayatengenez

1 Wakorintho 11:17-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi katika maagizo yafuatayo, siwezi kuwasifu, kwa sababu mkutanikapo si kwa ajili ya faida bali kwa hasara. Kwanza, mnapokutana kama kanisa, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo. Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonyesha ni nani anayekubaliwa na Mungu. Mkutanikapo pamoja si chakula cha Bwana mnachokula, kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine. Mmoja hukaa njaa na mwingine analewa. Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kanisa la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu juu ya jambo hili? La, hasha! Kwa maana mimi nilipokea kutoka kwa Bwana yale niliyowapa ninyi, kwamba Bwana Yesu, usiku ule aliposalitiwa, alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru, akaumega, akasema, “Huu ndio mwili wangu, uliotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.” Maana kila mlapo mkate huu na kunywea kikombe hiki, mnatangaza mauti ya Bwana mpaka ajapo. Kwa hiyo, mtu yeyote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana. Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe. Kwa maana mtu yeyote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana, hula na kunywa hukumu juu yake mwenyewe. Hii ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni wagonjwa na dhaifu na wengine wenu hata wamekufa. Lakini kama tungejichunguza wenyewe tusingehukumiwa. Tunapohukumiwa na Bwana, tunaadibishwa ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu. Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo pamoja ili kula, mngojane. Kama mtu akiwa na njaa, ale nyumbani kwake ili mkutanapo pamoja msije mkahukumiwa. Nami nitakapokuja nitawapa maelekezo zaidi.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha